STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 17.2.2017
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa azma ya Benki ya NMB ya kuendelea kuziunga
mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha miradi ya
maendeleo katika jamii zitasaidia kuimarisha uchumi na kuleta tija kwa wananchi
Dk. Shein aliyasema
hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya NMB nchini Tanzania Bi Ineke
Bussemaker alipofika Ikulu mjini Zanzibar.
Katika maelezo yake,
Dk. Shein alisema kuwa Benki ya NMB imekuwa na mchango mkubwa katika kuzisaidia
sekta za maendeleo hapa nchini zikiwemo sekta ya afya, elimu na nyenginezo hatua
ambayo ni muhimu katika kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Dk. Shein alisema kuwa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikitekeleza miradi mbali mbali ya
maendeleo ambayo lengo ni kuwanufaisha wananchi pamoja na kukuza uchumi na kueleza
mikakati ya kuanzisha Mradi wa huduma ya afya kwa njia ya kimtandao e-Health.
Aidha, Dk. Shein
aliipongeza Benki hiyo kwa kuanzisha programu mbali mbali za kuwasaidia
wakulima wakiwemo wa zao la karafuu hapa
nchini na kueleza lengo la Serikali ni kuona zao la karafuu linaimarika na ndio
maana imekuwa ikichukua juhudi za makusudi ili kuhakikisha zao hilo linapata
sifa kimataifa.
Dk. Shein alizitaja
miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wakulima wa
karafuu, kuongeza uzalishaji wa miche, kuongeza bei ya zao hilo kwa wakulima sambamba
na kuanzishwa kwa mpango wa kuzipa utambulisho maalum (Branding), karafuu na
bidhaa za viungo vinavyozalishwa hapa Zanzibar.
Aliongeza kuwa hizo ni
hatua muhimu za kuliimarisha zao la karafuu na kuongeza usafirishaji wa bidhaa
zinazotokana na viungo nje ya nchi kwa lengo la kuongeza kipato cha wakulima na
wafanyabiashara pamoja na kuimarisha uchumi wa nchi.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alitumia fursa hiyo kumueleza Mkurugenzi Mkuu huyo wa NMB juhudi
zinazochukuliwa na Serikali katika kupambana na changamoto ya ajira kwa vijana
ikiwa ni pamoja na lengo la Serikali la kuanzisha uvuvi wa bahari kuu.
Alisema kuwa miongoni
mwa maeneo ya kuanzia katika changamoto hiyo ni katika sekta ya uvuvi hasa
ikizingatiwa kuwa visiwa vya Zanzibar vimezungukwa na bahari, hivyo alimueleza
Mkurugenzi huyo umuhimu kwa Benki yake kuisaidia sekta hiyo ili wavuvi waweze
kuvua katika bahari kuu pamoja na kutumia vifaa vya kisasa.
Pia, Dk. Shein
alimueleza Mkurugenzi huyo juhudi zinazochukuliwa na akina mama katika kilimo
cha mwani ambacho kimekuwa ni maarufu katika maeneo ya ukanda wa pwani Unguja
na Pemba licha ya wakulima hao kuuza kwa
bei ndogo bidhaa hiyo.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alimuhakikishia Mkurugenzi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
itaendelea kushirikiana na Benki hiyo katika kuimarisha sekta za maendeleo na
kukuza uchumi wa nchi na wananchi wake.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa
NMB, nchini Tanzania Bi Ineke Bussemaker alipongeza juhudi zinazochukuliwa na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha miradi ya maendeleo katika
jamii na kuahidi kuendelea kuunga mkono.
Bi Bussemaker alisema
kuwa Benki yake imekuwa ikisaidia katika kuimarisha miradi mbali mbalio katika
jamii ikiwemo miradi ya elimu, kilimo, afya na mengineyo na kuahidi kuiendeleza
kwa lengo la kuinua kipato cha mwananchi hapa Zanzibar.
Aidha, Bi Bussemaker
alisema kuwa Benki ya NMB imeweza kusaidia miradi kadhaa ikiwemo miradi ya
elimu kwa kusaidia madawati, na kueleza azma ya benki hiyo kusaidia kompyuta 50
kwa skuli za Zanzibar.
Pia, Mkurugenzi huyo
alieleza hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Benki yake katika mradi wa
kuwasaidia wakulima katika kuimarisha na kusafirisha bidhaa zao zikiwemo bidhaa
za viungo na kusisitiza umuhimu wa kukusanya mapato kwa kutumia mfumo wa kisasa
wa “e-tax” ambapo benki yake tayari imeshaanza mchakato huo kwa upande wa
Tanzania Bara.
Pamoja na hayo, Mkurugenzi huyo aliahidi kuwa NMB
itaendelea kusaidia miradi mbali mbali katika jamii kwa lengo la kuwaunga mkono wananchi katika kujiletea maendeleo yao ya kiuchumi na kijamii.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment