Habari za Punde

Wananchi shehia ya Ng'a'mbwa wakabidhiwa ng'ombe kupitia mradi wa kopa Ng’ombe lipa Ng’ombe.

NA HAJI NASSOR, PEMBA

WANANCHI saba wakiwemo wanawake wawili na wanaume watano, waliounda kikundi cha ufugaji waliopo shehia wa Ng’ambwa wilaya ya Chakechake, wamekadbiwa Ng’ombe (ndama) saba, kupitia mradi wa kopa Ng’ombe lipa Ng’ombe.

Hafla ya makabidhiano hayo, yalifanyika kwenye mabanda ya kufugia Ng’ombe hao yanayomilikiwa na kikundi cha Umoja ni nguvu cha shehia hiyo.

Mradi huo wa kopa Ng’ombe lipa Ng’ombe, uliochini ya Mradi wa kuimarisha huduma za kilimo na mifugo ASSP na ASDP-L unaodhaminiwa na Mfuko wa kimataifa wa maendeleo ya kilimo ‘IFAD’ kupitia serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kikundi cha umoja ni nguvu kilikabidhiwa Ng’ombe 20 mwaka 2015 wakiwa na mimba, lengo baada ya kuzaa majike ni kuwapatia wananchi wenzao ndama hao, ili wafuge na kisha wengine kuwapa wenzao.

Akizungumza kabla ya ugawaji wa Ng’ombe hao saba kutoka kwa wanakikundi cha Umoja ni nguvu kwenda kwa wanakikundi wengine, Mratibu wa mradi huo wa ASSP-ASDP-L Pemba Asha Omar Faki, alisema lengo ni kuona Ng’ombe hao wanasambaa kwa wananchi wote.

Mratibu huyo alisema, miongoni mwa masharti ya mradi huo ni kuwa wananchi wafugaji kujikusanya pamoja, ili kuendesha ufugaji na kisha wanapozaliwa wengine kuwagawa kwa wengine.

“Huu mradi lengo lake ni kuona unasambaa kwa jamii yote, baada ya wanaokabidhiwa Ng’ombe awali wakishazaa, hutakiwa kuwapa wengine ili nao wafuge na baada kuwapatia wengine kama tunavyofanya leo’’,alifafanua.

Kwa upande wake mjumbe wa kikundi cha umoja ni nguvu kilichotoa Ng’ombe (ndama) saba, Said Juma Salim alisema waliyalea makoo hayo 20, waliokabidhiwa ingawa wanne walikufa baadae.

“Haya makoo 16 yaliobakia yameshazaa, na leo (jana) tunakabidhi ndama majike saba,  kwa wenzetu wafugaji ili nao wakafuge na kisha kuwapa wenzao’’,alifafanua.

Akizungumza kwa niaba ya wafugaji wenzake wapya waliokabidhiwa ndama hao, Salama Abdalla Mohamed alisema, watahakikisha wanawatunza na baada ya kuzaa kuwagawa kwa wenzao wengine.

“Sisi tulikuwa na hamu ya kukabidhiwa ndama hawa, maana ufugaji unaweza kututoa kwenye umaskini nzito tulionao sasa’’,alifafanua.

Mkuu wa Idara ya Mifugo Pemba Aisha Zaharan Mohamed alisema, wanavyovituo tisa kisiwani Pemba ambavyo vimeanzishwa na serikali, kwa ajili ya wananchi ili kujiunga kwenye mpango huo wa kopa Ng’ombe lipa Ng’ombe.


Miongoni mwa vituo hivyo ni Makundeni, Vikunguni, Mizingani, Piki, Kisiwani, Wingwi na Makangale ambapo wanavikundi hao, walikabidhiwa Ng’ombe hao tokea mwaka 2015.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.