Habari za Punde

Uongozi wa Shirika la PSI Lautaka Uongozi wa Kamati ya Maendeleo Makangale Kuvunja Uongozi wa Kamati Hiyo na Kuchagua Mpya.

Na. Salmin Juma Pemba. 

Wajumbe wa Jumuiya ya Pemba Suport Island (PSI) wameelezea kutoridhishwa na utendaji wa kazi za Jumuiya ya Maendeleo ya Makangale (MADA) na kuagizwa kuvunjwa kamati ya Uongozi wa Jumuiya hiyo  haraka iwezekanavyo .

Uwamuzi wa kutaka kuvunjwa kamati ya Uongozi ya MADA umekuja  baada ya kujiridhisha kuwa umeshindwa kuwajibika katika kutekeleza wajibu na majukumu yao ya kazi .

Akizungumza kwenye mkutano wa dharura uliofanyika katika Skuli ya Makangale Makamo Mwenyekiti wa PSI Makao Makuu Nchini Island  Nelius Adolf amesema moja ya sababu zilizopelekea kuagiza kuvunjwa kamati hiyo ni kushindwa kuwasilisha ripoti kwa kipindi kirefu.

Amefahamisha kuwa kutowasilishwa ripoti ya kamati hiyo kwa kipindi cha mwaka mzima kumeonysha jinsi viongozi hao wasivyo wajibika  licha ya kamati hiyo kuendesha miradi mingi ya maendeleo katika shehia hiyo.

Ameeleza kuwa PSI imesaidia miradi mikubwa miwili  katika shehia hiyo iliyogharimu mamilioni ya fedha lakini inaonekana haijainufaisha wananchi tofauti na ilivyokusudiwa wakati ikianzishwa miaka mitatu iliyopita.

“Kuna miradi miwili mikubwa ambayo imegharimu mamilioni ya fedha ikiwemo wa ngombe pamoja na wa maji , lakini uongozi umeshindwa kutoa ripoti juu ya maendeleo ya miradhi kwa kipindi kirefu , hivyo ni bora iundwe kamati nyingine hata leo hii ”alieleza Nelius .

Naye Mwenyekiti wa PSI Pemba Hamza Suleiman amesema sababu nyingine iliyopelekea kuvunjwa kwa kamati hiyo ni viongozi kukaa madarakani muda mrefu na hivyo kufanya kazi kwa mazoea na kupungua kasi ya uwajibikaji .

Amefahamisha , kitendo cha kukaa madarakani kwa muda wa zaidi ya miaka sita umeshusha ari ya ufuatiliaji sambamba na kutofanyika kwa mikutano  kujadili matatizo  na mafanikio ya kazi zao za kila siku .

“Viongozi wamekaa madarakani kwa kipindi kirefu , hali hii imepelekea kufanya kazi kwa mazoea na hivyo kushindwa hata kuitisha vikao kujadili matatizo yanayokwamisha ufanisi wa miradi hiyo na kwamba  uchaguzi unapaswa kufanyika machi 5 mwaka huu ”alisema .

Mapema akitoa maelezo ya utekelezaji wa miradi hiyo , Katibu wa Jumuiya ya MADA John Simba amesema kwamba hakuweza kuandaa ripoti kutokana na kutokuwa na mawasiliano ya uhakika kwamba watatembelewa na ugeni kutoka PSI Makao makuu .

PSI imefadhiri mradi wa ngombe uliogharimu shilingi milioni 35 , mradi wa kisima cha maji uliogharimu shilingi milioni 20 pamoja na kusaidia masomo kwa baadhi ya wanafunzi wa skuli za msingi  , ufundi na chuo kikuu .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.