Habari za Punde

Jamii yaagizwa kubadili tabia kwa kuweka mazingira safi kujiepusha na maradhi ya mripuko

 Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar, Dkt. Fadhil Mohammed Abdalla  akieleza mipango iliyoandaliwa ya  kukabiliana na maradhi ya kipindupindu iwapo yatatokezea katika kikao kilichofanyika Hospitali ya wagonjwa wa akili Kidongo chekundu Mjini Zanzibar.

 Mkuu wa Kitengo cha Afya ya Mazingira Rukaiya Mohamed Said akiwasilisha taarifa ya kikao kilichopita cha Kamati hiyo kilichofanyika mwezi uliopita.

 Afisa kutoka Jumuia ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi Zanzibar Jokha Masoud Salim akitoa mchango wakati wa kikao hicho.
 Baadhi ya washiriki wa mkutano wa Kamati ya kukabiliana na kipindupindu wakifuatilia kikao hicho kilichofanyika Hospitali ya wagonjwa wa akili Kidongochekundu.



Afisa operesheni na huduma za kibinadamu, Kamisheni ya kukabiliana na maafa, Makame Khatibu Makame akitoa mada juu ya mpango wa kukabiliana na maafa Zanzibar katika cha Kamati hiyo kilichofanyika Hospitali ya wagonjwa wa akili Kidongochekundu.

Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar


Na  Khadija  Khamis –Maelezo  

Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Dkt  Fadhil Moh’d Abdalla ameitaka jamii kubadili tabia kwa  kuweka mazingira yaliyowazunguka safi na kuhakikisha wanatumia maji safi na salama ili kujiepusha na maradhi ya mripuko .

Hayo ameyasema wakati  wa kikao cha kamati ya kitaifa ya kuandaa mpango mkakati wa kudhibiti maradhi ya kipindupindu  hasa kipindi  hichi ambacho mvua za masika zimeanza kunyesha.

 Alisema lengo kuu la kamati hiyo ni kufanya tadhmini ya muendelezo wa mpango kazi wa kudhibiti maambukizi ikiwemo kutoa elimu ya usafi wa mazingira kwa jamii na  kupambana na mazingira hatarishi katika maeneo mbali mbali ya Manispaa ya Zanzibar.

Ameishauri Mamlaka ya Maji Zanzibar  (ZAWA) kuhakikisha  maji  yanayotumiwa na wananchi yapo katika hali ya safi na salama kwa  kutia dawa vianzio vyote vya maji  na kuwataka wananchi kuacha tabia  ya kufanya uharibifu kwenye njia za maji kwa kutoboa  mabomba yanayosamba maji .

Alieleza changamoto zinazowakabili kwa sasa ni kuwepo kwa wafanyabiashara wasiofuata taratibu za usafi wa chakula na mazingira  katika utendaji mzima wa biashara zao.

Alisema uzoefu unaonyesha maradhi ya kipindupindu mara nyingi hutokea wakati wa kipindi cha mvua hivyo tahadhari zinahitajika katika kuweka mazingira katika hali ya usafi

 “Wananchi wahakikishe wanakunywa maji ya kuchemsha au kuyatia watergard ili kuweka tahadhari wakati huu wa kipindi cha mvua za masika kwani kunauwezekano mkubwa wa kuchafuka vyanzio vya maji kwa kuingia maji machafu,”  Alisema Mkurugenzi kinga .

Aliwashauri wananchi wanaoishi sehemu za mabondeni kuchukue juhudi za makusudi kuhama katika maeneo hayo ili kuepuka majanga  katika kipindi hichi cha mvua za masika 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.