Habari za Punde

NCIC Yatamani Kenya Iwe Kama Tanzania

Mkurugenzi wa Programu, Bi. Millicent Apondi Okatch akiongea katika kikao kifupi baina ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) na National Cohesion and Integration Commission (NCIC), kulia anayeandika ni Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Bahame Tom Mukirya Nyanduga.
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Bahame Tom Mukirya Nyanduga (kulia) akiongea katika kikao kifupi na ujumbe wa Kamisheni  inayohamasisha umoja kwa jamii ya watu wa Kenya na kuondosha aina zote za utengano wa makabila (National Cohesion and Integration Commission) uliomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam  kwa lengo la kujifunza namna tume inavyofanya kazi zake. Ujumbe huo uliongozwa na Kamishna, Mhe. Morris Dzoro (kushoto), wa pili kushoto ni Kamishna, Profesa Gitile Naituli, wa tatu kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Programu, Bi. Millicent Apondi Okatch.
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Bahame Tom  Nyanduga (kulia) akiongea na Makamishna wa NCIC mara baada ya kumaliza kikao. Kushoto ni Kamishna, Mhe. Morris Dzoro na katikati ni Kamishna, Profesa Gitile Naituli.

Na Mbaraka Kambona,
Ujumbe wa Tume inayohamasisha umoja na mshikamano  na kupambana na aina zote za utengano wa Makabila kwa jamii ya watu wa Kenya ( National Cohesion and Integration Commission) umesema kuwa wanatamani kuiona Kenya inakuwa kama Tanzania ambayo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliijenga katika misingi ya umoja na mshikamano.

Wakiongea katika kikao kifupi mara baada ya ujumbe huo kufanya ziara katika ofisi za Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora jijini Dar es Salaam Machi 29,2017, ujumbe huo haukusita kueleza hisia zao juu ya Tanzania na kueleza  kuwa  suala la Ukabila nchini Kenya bado lipo na ndio moja ya mambo ambayo wanashughulika nayo.

“Tungetamani sana Kenya ingekuwa kama Tanzania, kwani Mwalimu aliijenga Tanzania kuwa taifa moja” alisema  Kamishna Dzoro

“Tunasikia wivu kwenu, Tanzania imejengwa kama taifa sisi Kenya bado ni nchi”, aliongeza Profesa Gitile

Naye, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Bahame  Nyanduga wakati akiwaeleza kuhusu majukumu ya tume,  pia aliwaomba kwamba, kwa kuwa wanaelekea katika uchaguzi mkuu wahakikishe vyama vya nchini kwao vinajihepusha na kuunda vikundi vya vijana wa chama “youth league” ambavyo kwa uzoefu uliopatikana katika uchaguzi  uliopita nchini Tanzania  vikundi hivyo vilianza kujiingiza katika majukumu ambayo sio yao ya kutaka kulinda maeneo ya kupigia kura na kulinda kura jambo ambalo ni hatari kwa  amani na usalama wa nchi.

Ujumbe huo wa watu wanne ulioongozwa na Kamishna, Mhe. Morris Dzoro ulikuwa na lengo la kujifunza namna Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora wanavyofanya kazi zake.
Wajumbe wengine waliokuwa katika ziara hiyo ni  Kamishna, Profesa Gitile Naituli,  Mkurugenzi wa Programu, Bi. Millicent Apondi Okatch na Afisa wa elimu ya uraia na uhamasishaji, Ndugu Richard Nderitu.

NCIC ilianzishwa kwa lengo la kuhamasisha umoja na mshikamano katika jamii ya watu wa Kenya  kwa kuandaa michakato na sera mbalimbali zinazowezesha kuondoa aina zote za ubaguzi wa kikabila nchini humo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.