Habari za Punde

Pendekezo: Watoto wafidiwe pindi wakipata ajali wakichuma Karafuu

NA HAJI NASSOR, PEMBA

WANANCHI wa wilaya ya Mkoani kisiwani Pemba, wameitaka Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar, kuingiza kipengele cha watoto wanaoanzia miaka 14 kulipwa fidia, wakati wanapopata ajali wakiliokoa zao la taifa la karafuu.

Walisema wachumaji wakubwa wa zao la karafuu ni watoto wenye umri kati ya miaka 14 hadi 17, hivyo ni vyema kwenye marekebisho ya sheria ya fidia, watoto wenye umri huo nao wakatambuliwa na sheria ili kulipwa fidia.

Wananchi hao walieleza hayo mbele ya Tume ya Kurekebisha Sheria, inayoongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Mshibe Ali Bakari, wakati ilipokutana na wananchi hao, ili kukusanya maoni yao, juu ya kuzifanyia mapitio sheria za usalama kazini na ile ya fidia zote za mwaka 2005.

Maoni ya wananchi hao, yalikuja kufutia sheria ya sasa ya fidia ya mwaka 2005 kwamba, haimtambui kifidia kwa mtu alienguka wakati akichuma karafuu, kama hajafikia umri wa miaka 18.

Mjumbe wa mkutano huo Juma Bakar Shoka, alisema wachumaji hasa wa zao la karafuu ni watoto wenye umri kuanzia miaka 14 na kuendelea, hivyo lazima sheria iwatambue kulipwa fidia.

“Mimi napendekeza kwenye sheria mpya ijayo ya fidia, na hawa watoto walipwe fidia, maana ndio hasa wenyewe wanaozichuma karafuu na hata skuli wakati mwengine hufungwa’’,alipendekeza.

Nae Salum Omar alisema watu wenye umri mkubwa, wengi wao sio wachumaji hasa wa zao taifa la karafuu, na badala yake watoto wenye umri wa kati, ndio wahusika wakuu.

“Hata mimi napendekeza sheria ya fidia ijayo, iwatambue watoto wenye umri kuanzia umri wa miaka 14 na kuendelea, maana tukifanya kinyume chake, tutawakosesha haki yao ya kujifunza kuchuma karafuu’’,alisema.

Kwa upande wake Rashid Abdalla, alisema hata sheria inayokuja ielekeze wapi fedha hizo zinapatikana na kusiwe na urasimu, na kumfanya mpatwa na ajali kujuta kuzifuatilia.

Akifungua mkutano huo Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar Jaji Mshibe Ali Bakar, alisema ingawa sheria za kimataifa zinakataza mtoto kufanyishwa kazi zenye kuhatarisha maisha yake, lakini hilo wataliangalia kwa ukaribu.

Katika hatua nyengine Mwenyekiti huyo, alisema lengo la kuzifanyia marekebisho sheria za fidia na ile ya usalama kazini za mwaka 2005, kuhakikisha wananchi wote wanaishi kwa usawa.

Sheria ambazo Tume ya Kurekebisha Sheria Zanzibar inazifanyia mapitio ni ile sheria ya fidia ya kazini no 15 ya mwaka 1986 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2005 na sheria ya usalama kazini no 8 ya mwaka 2005.
             


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.