STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 23.03.2017

SERIKALI ya Jamhuri ya Watu wa China imeahidi
kukamilisha miradi yote inayoisaidia Zanzibar ikiwa ni pamoja na kukamilisha
jengo jipya la abiria katika uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume haraka
iwezekanavyo huku ikiahidi kuunga mkono ujenzi wa bandari mpya ya Mpigaduri.
Mjumbe wa Kamati Kuu na
Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), Guo Jinglong aliyasema
hayo katika mazungumzo kati yake na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) Zanzibar, huko Ikulu mjini Zanzibar.
Kiongozi huyo ambaye
yuko ambaye yuko nchini, amempongeza Dk. Shein kwa juhudi zake za kuoingoza
Zanzibar na kuweza kupiga hatua kubwa za maendeleo sambamba na kuimarisha amani
na utulivu hapa nchini na kusisitiza kuwa hatua hiyo ya kuziunga mkono sekta
hizo za maendeleo ikiwemo ujenzi huo wa jengo hilo jipya la abiria katyika
uwanja wa ndege wa Zanzibar kutaimarisha sekta ya utalii.
Alisema kuwa tokea Dk.
Shein kuweko madarakani Zanzibar imeendelea kupiga hatua kubwa za maendeleo na
kuongeza kuwa kuchaguliwa kwake tena na wananchi kwa kipindi cha pili
madarakani kuendelea na wadhifa wake huo kumezidi kuiletea maendeleo Zanzibar.
Kiongozi huyo alimueleza
Dk. Shein kuwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China pamoja na chama chake cha
CPC kimekuwa na uhusiano wa muda mrefu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kiongozi huyo wa CPC
alimueleza Dk. Shein kuwa hakuna sababu ya kuvunjika kwa uhusiano huo uliopo na
kueleza dhamira ya Serikali yake kuendelea kutoa ushirikiano kwa Zanzibar
pamoja na kuendelea kukiunga mkono Chama Cha Mapinduzi.
Kuhusu sekta ya afya
Kiongozi huyo alieleza kuwa China itaendelea na utaratibu wake wa kuleta
madaktari hapa Zanzibar kwa kila baada ya muda uliopangwa ili kuimarisha
utamaduni huo ambayo ulianzishwa tokea mwaka 1965.
Katibu Jinlong alisifu
jitihada zinazoendelezwa na CCM ambazo zina itikadi zinazofanana na CPC hatua
inayoonesha wazi ukomavu wa CCM kisiasa ambayo inawafanya wananchi walio wengi
waendelee kukiamini chama hicho kutokana na Sera zake imara za maendeleo kwa
ajili ya kuimarisha ustawi wa wananchi wa Tanzania bila ubaguzi.
Aidha, alieleza umuhimu
wa viongozi wa vyama vya CCM na CPC kutembeleana ili kubadilishana mawazo na
kuimarisha uhusiano na umoja wao wa kihistoria uliopo kati ya vyama hivyo.
Sambamba na hayo, Mjumbe
huyo wa Kamati Kuu ya CPC alitoa pongezi kwa wananchi wa Zanzibar, Serikali na
Chama Cha Mapinduzi kwa mapokezi mazuri waliyoyapata wakiwa hapa nchini yeye na
ujumbe wake.
Nae Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alitumia fursa hiyo
kutoa pongezi kwa ujio wa kiongozi huyo hapa nchini na kusisitiza kuwa hatua
hiyo ni uhusiano mwema na ushirikiano uliopo kati ya CCM na CPC pamoja na
Serikali za China na Tanzania.
Dk. Shein alisema kuwa
azma ya China kuendelea kushirikiana na Zanzibar katika kuimarisha miradi ya
maendeleo ukiwemo mradi wa ujenzi wa bandari ya Mpigaduri na uwanja wa ndege wa
Abeid Amani Karume kutaimarisha ukuaji wa uchumi sambamba na kuimarisha sekta
ya utalii.
Alieleza kuwa asilimai
80 ya fedha za kigeni zinatokana na mchango mkubwa wa sekta ya utalii ambayo
pia, huchagia asilimai 27 ya pato la Taifa.
Aidha, Dk. Shein
alisisitiza kuwa Zanzibar imekuwa na uhusiano na China tokea wa kihistoria kati
yake na China hatua ambayo imewapelekea wananchi wa China kuweza kuishi
Zanzibar na kuwa Watanzania hivi sasa.
Aliongeza kuwa Serikali
ya China imeweza kuiunga mkono Zanzibar katika sektra mbali mbali za maendeleo
ikiwemo sekta ya kilimo ambapo mara tu baada ya Mapinduzi matukufu ya Janurai
12, 1964 ambayo China ni miongoni mwa nchi za mwanzo kuyatambua ambapo pia,
Serikali hiyo ilianzisha kilimo cha umwagiliaji maji hapa nchini.
Aidha, China ilijenga
viwanda mbali mbali kikiwemo kiwanda cha sigara, kiwanda cha viatu pamoja na
viwanda vidogo vidogo sambamba na kuleta wataalamu wa fani mbali mbali hapa
Zanzibar.
Kwa upande wa sekta ya
afya, Dk. Shein alisema kuwa serikali ya China imeweza kuunga mkono sekta ya
afya kwa kuleta wataalamu wa sekta hiyo tokea mwaka 1965, na ujenzi mpya wa
hospitali ya Abdalla Mzee pamoja na vifaa kwa hospitali hiyo na hospitali ya
MnaziMmoja.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alisisitiza kuwa hakuna jambo linaloweza kuondosha uhusiano wa kihistoria
kati ya CCM na CPC pamoja na uhusiano wa Serikali zake ambapo alituma salamu za
pongezi na kumtakia afya njema Rais wa China Xi Jinping na kupongeza hatua
kubwa za maendeleo zilizofikiwa na nchi hiyo sambamba na kuimarika kwa uchumi
wake.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment