STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 27.03.2017

RAIS wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza
kuwa idadi kubwa ya wagonjwa waliofanyia upusuaji wa maradhi ya kichwa na uti
wa mgongo hapa Zanzibar tokea kuanzishwa huduma hizo ni miongoni mwa mafanikio
makubwa katika sekta ya afya hapa nchini.
Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na
mazungumzo na ujumbe wa Wataalamu wa upasuaji wa kichwa na uti wa mgongo
waliofika Ikulu mjini Zanzibar.
Wataalamu hao ambao wapo Zanzibar kushiriki mkutano maalum wa
mafunzo kuazia kesho tarehe 28 hadi
tarehe 30 mwezi huu ambapo pia, ni miongoni mwa maadhimisho ya kutimiza
miaka miwili tokea kuaizishwa kwa jengo la huduma hizo katika hospitali Kuu ya
Mnazi Mmoja mjini Zanzibar, ambalo alilizindua Dk. Shein Januari 9, kwaka 2015.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa
mafanikio hayo yanatokana na juhudi kubwa zinazochukuliwa na wataalamu wa fani
hiyo kutoka sehemu mbali mbali duniani ambao wanaiunga mkono Zanzibar katika
kuimarisha sekta ya afya hasa katika kutoa huduma ya upasuaji huo.
Dk. Shein alisema kuwa hatua za utoaji wa huduma
hiyo zinazofanywa kwa Unguja na Pemba ambazo tayari zaidi ya wagonjwa 500
wameshafanyiwa upasuaji huo wakiwemo watoto, wanawake na watu wazima zimeweza
kusaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta ya afya hapa nchini.
Alieleza kuwa kuwepo kwa wagonjwa mbali mbali
wanaotoka nje ya Zanzibar na kuja kupata huduma hiyo hapa Zanzibar ni historia
ambayo inajirejea ambayo ilikuwepo hapa Zanzibar tokea wakati wa ukoloni ambapo
wagonjwa mbali mbali kutoka nje ya Zanzibar walikuja kupata huduma za afya hapa
nchini.
Alisema kuwa licha ya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kuokoa kiasi kikubwa cha fedha zilizokuwa zikitumika kwa ajili ya
kuwatibu wagonjwa wa maradhi hayo nje ya nchi faraja iliopo ni kuona huduma
hiyo muhimu inatolewa hapa nchini na kuweza kuwasaidia wananchi mbali mbali wa
ndani na nje ya Zanzibar.
Aidha, Dk. Shein aliueleza ujumbe huo juhudi zilizochukuliwa
na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha inanunua vifaa muhimu
na vya kisasa ikiwemo mashine ya “MRI”,
mashine ya “X-ray” pamoja na mashine za huduma za kusafisha damu kwa wagonjwa
wenye matatizo ya figo, ambazo zote hizo zimeshanunuliwa na serikali na kuanza
kutoa huduma kwa wananchi.
Mbali ya juhudi hizo, Dk. Shein aliueleza ujumbe
huoa azma ya Serikali ya kujenga hospitali mpya ya mafunzo ambayo mbali na mambo mengine pia, itatoa mafunzo juu
ya upasuaji wa kichwa na uti wa mgongo, azma ambayo iliungwa mkono na mkuu wa
Kanda wa Hospitali za Aga Khan, Shawn Balouki ambaye ni miongoni mwa wajumbe
waliofika Ikulu.
Nao Wataalamu hao wakiongozwa na Rais wa Taasisi
ya Maendeleo ya Elimu inayohusiana na upasuajai wa Mishipa ya Fahamu, Uti wa
mgongo na Vichwa maji (NED), Dk. Hosea Piquer pamoja na Dk. Mahmood Quiresh
walieleza mafanikio makubwa waliyoyapata katika huduma za upasuajai
walizozifanya tokea kuanzishwa huduma hizo hapa nchini.
Katika maelezo yao wataalamu hao walimuhakikishia
Dk. Shein kuwa wataendelea kuziunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya hasa katika huduma hiyo ya upasuaji wa kichwa na uti wa
mgongo.
Sambamba na hayo, Wataalamu hao walitumia fursa
hiyo kumueleza Dk. Shein azma ya kuendelea na utoaji huduma hizo Unguja na
Pemba pamoja na mkutano maalum wa mafunzo wa siku tatu kuzia kesho (tarehe 28-30,
2017) katika Taasisi ya maradhi hayo iliyopo katika Hospitali ya Mnazi Mmoja
mjini Zanzibar.
Wataalamu hao walieleza kuwa mbali ya kuwafanyia
upasuaji wagonjwa wa Zanzibar tayari wameshawafanyia upasuaji wagonjwa kutoka
Lamu, Dubai na sehemu nyengine nje ya Zanzibar jambo ambalo ni mafanikio huku
wakieleza kupokea wataalamu kutoka nchi mbali mbali za bara la Afrika wanaokuja
kujifunza namna ya kuanzisha na kuendeleza taasisi kama hiyo.
Taasisi kama hiyo ni ya pekee katika bara la
Afrika ambayo inatoa huduma hizo bure pamoja na kutumia vifaa vya kisasa na
utaalamu na wataalamu wakubwa kutoka sehemu mbali mbali duniani wakiwemo kutoka
nchini Spain, Ujerumani, Pakistan, Aga Khan na sehemu nyenginezo.
Pamoja na hayo, wataalamu hato walieleza namna
wanavyochukua juhudi za kutoa mafunzo wa wataalamu wazalendo huku wakieleza
mashirikiano mazuri wanayoyapata kutoka kwa wataalamu wazalendo.
Katika mazungumzo hayo ambapo Madaktari hao bingwa
walikuwa wameongozana na uongozi wa Wizara ya Afya chini ya Waziri wa Wizara
hiyo Mahmoud Thabit Kombo, ambao
walipongeza mashirikiano makubwa wanayoyapata katika kutekeleza shughuli zao
hapa nchini.
Pamoja na hayo, madaktari hao walieleza kuwa
miongoni mwa mafanikio makubwa yaliopatikana kutoka kwa Taasisi hiyo ni pamoja
na kufanya upasuaji huo kwa wagonjwa zaidi ya 500 wakiwemo watoto, wanawake na
watu wazima na kueleza jinsi Serikali ilivyokuw ikitumia fedha nyingi
kuwapelekea wagionjwa wa maradhi hayo nje ya nchi kabla ya kuanzishwa kwa
huduma hizo hapa nchini.
Madaktari hao walimueleza Dk. Shein kuwa gharama
hizo ni kwa ajili ya taaluma na upasuaji mbali na gharama nyengine ambazo
Serikali ingeweza kutumia katika usafirishaji, gharama za malazi na chakula kwa
wagonjwa na wauguzi wao pale wanapowasafirisha kwenda nje ya nchi.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address:
2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment