Habari za Punde

Risala ya WanaTaasisi ya Zanzibalicious Women Group Wakati wa Kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.

Ndugu Mgeni Rasmi,
Mke wa Rais wa Zanzibar,Mama Mwanamwema Shein, 
Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi
Mhe. Ayoub Mohammed Mahmoud Waziriwakazi, Uwezeshaji Wazee, vijana,Wanawake na Watoto
Mhe: Mama Maudline Castico Meza kuu, Viongozi wote wa serikali na vyama vyote.Walezi wa Taasisi.

Ndugu waalikwa wote na wanavikundi wenzangu
Habari za Muda huu.
Ifuatayo ni risala kutoka kwa Zanzibalicious Women Group
Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetujaalia uzima na afya kwa kipindi kirefu hadi tukaweza kukutana tena leo hii.

Mhe:Mgeni Rasmi ,Zanzibalicious ni Taasisi ya wanawake iliyoanzishwa mwaka 2011 na kusajiliwa mwaka 2013, kwa nia ya kumuendeleza na kumuwezesha mwanamke Kiuchumi, Kijamii na Kimwenendo.
Kutokana na mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi yanayoendelea katika sehemu mbali mbali ulimwenguni kote, hasa katika bara la Afrika. Utafiti umeonyesha kuwa wahanga wakuu waatharika zaidi ni wanawake na watoto.

Hivyo basi Zanzibalicious iliona ipo sababu ya kuwakomboa wanawake kutoka katika utumwa wa kiuchumiili kuwawezesha kuwapa ujuzi na maarifa yatakayowawezesha kuja kujikwamua kutoka katika dimbwi la umasikini.

MPANGO WETU                                                                      
Mhe:MgeniRasmi,Taasisi hii imeundwa kwa mtazamo wa kuwaunganisha, kuwahamasi kuwaendeleza wanawake kwa kuwapa ujuzi na maarifa ili waweze kujitambua na kuithamini nafasi yao katika kuleta maendeleo.
  
MALENGO YETU
Mhe:MgeniRasmi,
1:Malengo yetu ni kutoa elimu ya ujasiriamali kwa vikundi mbali mbali vya wanawake na kuwawezesha kubuni biashara ndogo ndogo na jinsi ya kuweza kutafuta mitaji kutoka taasisi mbali mbali za kitaifa.

2:Kutoa ushauri nasaha kwa masuala ya familia, waathirika wa VVU na Mihadarati (Dawa za Kulevya), Afya ya uzazi, Kansa ya matiti na shingo ya uzazi.

3:Kutoa ushauri wa kisheria katika suala zima la uzalilishwaji wa kijinsia hasa kwa wanawake na watoto.

4:Kuwakutanisha na kuwaunganisha wanawake kutoka sehemu mbali mbali kupitia maonesho ya kibiashara, matamasha na sherehe mbali mbali za kitaifa.

 CHANGAMOTO                                                                              
Mhe:MgeniRasmi,
Kila penye riziki pana mitihani, vikwazo vipo vingi katika juhudi zetu za kufikia malengo tuliyojiwekea.

Mwaka 2016 ulikuwa mwaka wa ukimya mwingi kutokana na mabadiliko mengi ya kiuchumi na kitaifa. Hivyo majukumu yetu mengi yalifanyika taratibu sana na ukimya mwingi lakini tunamshukuru Mwenyezi Mungu ametusimamia hatua kwa hatua mpaka hapa tulipo.

Hatuwezi kuelezea vikwazo vyote lakini vichache kati ya hivyoni:-
-    Kipato kidogo kimepelekea mipango mingi kuchelewa na kutokamilika kwa sababu haijitoshelezi mahitaji yote.
-      Wakati ni kikwazo kingine kwani muda haumsubiri mtu kila unapozidi kuchelewa na wakati nao unazidi kupotea nasi kuzidi kurudi nyuma.
-      Wanawake wengi kutokuwa na elimu ni kikwazo kikubwa sana. Inachukua muda mwingi sana kuwaelimisha hasa kwa wale wasiojua kusoma wala kuandika. 
 Pia inabidi mara kwa mara kuwakumbusha yale waliyojifunza kwani hawatunzi kumbukumbu kwa kutojua kusoma wala kuandika, na wengine wana umri mkubwa.
-      Mabadiriko ya mazingira yamekuwa changamoto kubwa sana kwetu, kwani mazao na mifugo mingi imeteketea kwa sababu ya joto kali.Hivyo vitendea kazi vinahitajika ili kukabiliana na mabadiriko ya mazingira.

MAFANIKIO                                                                            
Mhe:MgeniRasmi,                                                                   
Kwa upande wa mafanikio yetu mpaka sasa 2017 ni madogo kutokana na malengo tuliyojiwekea toka mwaka 2013 kwa kuwa hayajakamilika kwa asilimia tulizokusudia, lakini wahenga walisema HAKUNA KUPATA KUDOGO, nasi tunashukuru na kufurahia hatua tulizopiga mpaka hapa tulipo sasa.

Kila tunapomfikia mwanamke na mtoto na kumpa elimu, na ushauri au msaada wowote; kwetu ni mafanikio makubwa sana kwani hawa ndiyo mabalozi wetu kwa kina mama wengine.

Tumeweza kufungua ofisi na biashara, tumeweza kuanzisha na tunaendeleza vikundi vyetu viwili vya kina mama wa Chaani na Mwanakwerekwe sokoni. Pia tumeanzisha mpango wa utararibu wa ushauri wa kinadharia na vitendo kuhusiana na mfumo wa maisha bora.

Mpaka sasa tumeshamaliza maandalizi tunasubiri tarehe rasmini ya ufunguzi wa darasa letu la ushauri wa kiafya.

Katika kuhakiki lengo hili linawezekana na litaleta manufaa katika jamii.

Tumeaza sisi wenyewe kwa kufuata taratibu za kuishi kwa afya kwa kuanza taratibu (Program) za mazoezi na kula vyakula bora. 
Pia tumefanya vipimo mbali mbali kuangalia afya zetu.Na sasa tunahamasihana katika jamii iliyotuzunguka ili kutimiza malengo tuliyojiwekea.

Pia tuko katika muendelezo wa kutengeneza makala ya kazi zote tunazofanya katika jamii, na leo hii tutaonyesha baadhi ya kazi hizo.

Uboreshaji utakapokamilika, ofisi yetu itakuwa ya mwanzo kupokea makala hii pamoja na taasisi nyingine na wadau wetu wote.

Mhe:Mgeni Rasmi,
Mwaka uliopita wa 2016 tuliungana na EQUITY BANK ikiwa mdhamini wetu katika kuendeleza elimu za ujasiriamali, utunzaji wa fedha na taarifa za biashara katika vikundi mbali mbali vidogo vidogo vya wanawake na vijana wa kike na wakiume wa umri wa miaka kuanzia 18 mpaka 25.

Vikundi ni vingi sana lakini kwa uchache tumeweza kuwafikia wanawake wa Chaani, Mwanakwerekwe sokoni,Ubago, Vikundi vya kina mama wa Mjini Magharibi, Vikundi vya vijana wa mjini Magharibi vya Kijangwani, Youth Group ambavyo makao makuu yao yapo karibu na Madema na imeunganisha makundi mengi ya vijana. 

Vijana wa Jang’ombe wanaojishughulisha na upikaji chips na biashara ndogo ndogo.Vijana wakiume wa Kilimani waosha magari, ufundi gereji na wacheza mpira. Vijana wa kike wa kilimani wanaojishughulisha na ushoni, kuchora hina na kuimba kasida katika sherehe mbali mbali.

Kina mama wa Matemwe na kina mama wa Bweleo ambao wako katika makundi mengi mbali mbali.

 MWISHO
 Mhe:MgeniRasmi,
 Kazi zetu zote ni endelevu, tumezitenga katika makundi mbali mbali kwa wakati tuliojipangia. Kuanzia mwezi wa April 2017 tunaanza na uhamasishaji kina mama katika elimu na upimaji wa kansa ya matiti, na shingo ya uzazi.

Tutashukuru sana mheshimiwa mgeni rasmi katika hili pia ukishirikiana nasi kwa hali na mali.Pia tunaomba na kukukaribisha katika Taasisi za kiserikali, binafsi na wadau wote kushirikiana nasi katika kila hali kuhakikisha tumewafikia kina mama wote na kuwa na Zanzibar yenye kina mama wenye afya bora.

Tunatoa shukrani zetu za dhati kwako Mheshimiwa mgeni rasmi pamoja na waalikwa wote mlioshirikiana nasi tangu mwanzo hadi hapa tulipofikia. 

Tunaamini uwepo wenu na mashirikiano yenu yanatupa faraja sisi pamoja na wanawake wapenda maendeleo.

Tunaomba Mwenyezi Mungu azidi kutubariki sote.

Ahsanteni sana.
Katibu Zanzibalicious Women Group  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.