Na Hanifa Salim , Pemba
WALIMU wametakiwa kuzidisha juhudi ya kufundisha na
kusimamia maendeleo ya wanafunzi ili kuhakikisha wanafaulu katika mitihani yao.
Kauli
hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mwanajuma Majid Abdalla, alipokua
akizungumza na walimu na wanafunzi wa Skuli ya Sekondari ya Vitongoji, wakati
wa makabidhiano ya uwezekaji wa mabanda matano ya Skuli hiyo.
Alisema
waalimu ni vyema kushirikiana kwa pamoja
katika ufundishaji wa wanafunzi na kuzitumia fursa walizonazo katika uwajibikaji kama inavyotakiwa.
“Lazima
tuhakikishe tumetoa vigezo vizuri katika Skuli yetu, tuhakikishe tunapasisha
wanafunzi katika kiwango kizuri, hizi fursa tuzitumie vizuri waalimu tuwajibike
inavyotakiwa” alisema Mkuu huyo.
Aliwataka
wanafunzi kusoma kwa bidii na kuachana na vitendo vya udhalilishaji ambavyo
vimekuwa vikijitokeza katika Skuli mbali mbali sambamba na kujiepusha vishawishi watakavyo kumbana
navyo ili kujijengea maisha mazuri ya baadae.
“Wanafunzi
jitahidini musome mambo mengine kwani mtayakuta baadae hakuna haja ya kukimbilia
maisha lengo lenu ni kusoma tu wakati ukifika yatakuja wenyewe baada ya
kujijengea maisha yenu”, alisema.
Hata
hivyo aliwataka walimu kushirikiana kwa pamoja na kamati ya Skuli ili kujipanga
zaidi kudhibiti matendo machafu yanayojitokeza yakiwemo ya udhalilishaji ili
kuweza kufikia lengo linalokusudiwa.
Kwa
upande wake ,Mkurugenzi wa Baraza la mji Chake chake Pemba,Nassor Suleiman
Zaharan,akithibitisha uchangiaji wa Baraza la Mji kwa Skuli hiyo, alisema ni
jukumu lao baraza kufanya hayo kwa wananchi ili kuwaletea wananchi maendeleo.
Alisema
Baraza lake liliamuwa kuchangia ujenzi wa Skuli hiyo baada ya kuona Wazazi na
Walimu wa Skuli hiyo kuamuwa kujenga Skuli hiyo na hivyo baraza likatowa
mchango wa kuezeka.
Nae,
Mwalimu wa Skuli ya Sekondari Vitongoji, Hamad Abdalla Hamad, wakati akisoma
risala ya makabidhiano hayo alisema analiamini baraza kwa kuwaunga mkono na
kuwaomba wendelea kuwasaidia katika changamoto mbali mbali zinazowakabili
Skulini hapo.
Alisema
hadi kufikia kuweka linta Skuli hiyo ,tayari ilishatumia
jumla ya Shilingi 29,790,000/= harama
ambayo haikujumuisha gharama ya uezekaji ambapo ilifanywa na Baraza la Mji Chake chake.
“Fedha
iliyotumika katika ujenzi hadi kufikia hatua ya uwekaji linta umejuisha mchango
wa wahisani ambayo ni Shilingi 7,000,000/= na 19,334,000/= zikiwa ni michango
ya wazee na Skuli” alisema.
Alisema
changamoto zinazowakabili katika banda hilo la Skuli ni ukamilishaji hatua ya
upigaji plasta, uwekali wa sakafu na apron ambapo kwa makisio ni Shilingi
29,510,000/= ambazo bado ni mzigo mzito kwa Skuli na jamii iliyowazunguka.
Nae ,Mwalimu
Mkuu wa Skuli hiyo, Yussuf Ali Abrahman, alishukuru kupatiwa msaada huo wa
uwezekaji wa Skuli yao kupitia Baraza la Mji Chake chake na alilitaka baraza
kuendelea kuwaunga mkono kwa kuwasaidia ili kuondokana na changamoto zinazowakabili.
“
Hatuna budi kulishukuru baraza la Mji wa Chake Chake , kwa msaada wao mkubwa
waliotupatia , hata hivyo tunawaomba isiwe mwisho kutusaidia kwani tuhaitaji
misaada mbali mbali kwa ajili ya maendeleo ya Skuli yetu.” Alisema.
Jumla
ya bati 340 zimeezekwa katika Vyumba vitano
vya Skuli ya Sekondari ya Vitongoji zenye thamani ya Shilingi milioni
15,000,000/= ambazo zimegharamiwa
kupitia baraza la Mji Chake chake.
No comments:
Post a Comment