Habari za Punde

WanaCCM wasiwe na hofu ya kuwepo mabadiliko katika mfumo wa serikali

Na Muhammed Khamis

Wanachama wa chama cha mapinduzi CCM  visiwani Zanzibar wametolewa  hofu ya kutokuwepo aina yoyote ile ya mabadiliko katika mfumo wa Serikali.

Kauli hio imetolewa na makamo wa pili wa Rais Zanzibar ,Balozi Seif Ali Iddi wakati  akiwahutubia wajumbe wa baraza  la wawakilishi wakati wa ufungaji wa kikao cha tano cha baraza hilo.

Alisema wanaoendelea kusema taarifa zisizokuwa na ukweli kupitia mitandao  wataendelea kufanya hivyo huku Serikali ikiendelea na shughuli zake kama kawaida .

Balozi alisema kuwa kiongozi wa chama cha upinzani ( CUF) Maalim Seif hana uwezo wa kuwa Rais wa wananchi wa Zanzibar na ndio maana amekuwa akishindwa katika chaguzi zote tokea mwaka 1995.
‘’’Serikali hii itaendelea kuwepo mpaka mwaka 2020 msitishwe na mtu yeyote, yule Maalim Seif hana ubavu hata huo uchaguzi mwengine ukifika hataweza kushinda na kamwe Serikali hii haitatoka mikononi mwa chama cha mapinduzi’’alisema Balazi Seif.

Alieleza kuwa kinachoendelea kufanywa ni ''propaganda'' za kisiasa ili wananchi wao waendelee kuwaamini na kuwepo kwa mabadiliko jambo ambalo kiuhalisia halina ukweli wa aina yoyote hile.

Katika jitihada za kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar Balozi alisema Serikali kwa sasa wanaendelea na jitihada mbali mbali kuwaletea maendeleo wananchi wote bila ya ubaguzi.

Pamoja na hayo kiongozi huyo aligusia uwepo wa changamoto kubwa visiwani Zanzibar ya rasilimali ya mchanga kutokana na kuadimika kwa kiasi kikubwa bidhaa hio.

Alieleza kuwa lengo la serikali sio kuwatesa wanachi lakini ifike wakati kila mmoja wetu kukubali ukweli kuwa mchanga visiwani hapa unakaribia kumalizika.

Katika kukabiliana na hilo tayari Serikali imeunda tume ya watalamu kufanya utafiti na hatimae kushauri njia na maeneo gani yanafaa kuchimba mchanga.

Aidha alieleza kuwa baada ya utafiti huo kufanyika na kwa sasa tayari serikali itazindua rasmi mashimo yanayopaswa kuvunwa kwa mchanga pamoja na kutoa bei elekezi ili kuzuia ulanguzi kwa wananchi.

Akiendelea kufafanua zaidi  kiongozi huyo alisema kuwa wameamua kuchukua jitihada hizo ili kuzuia athari  ambazo zingeweza kujitokeza iwapo rasilimali hio ingendelea kuchimbwa bila ya udhibiti.

Sambamba na hayo alisema Serikali haitolipa fidia maeneo yoyote yale ambayo yatalazimika kuchimbwa kwa mchanga kwa ajili ya wananchi wote wa Zanzibar.

Kiongozi huyo pia  alitoa wito kwa wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika nyanja mbali mbali kwa wananchi wote bila ya ubaguzi.

Kikao cha tano cha cha  baraza kwa wajumbe wa baraza la wawakilishi visiwani hapa kimefungwa  jana na kinatarajiwa kufunguliwa tena mnamo tarehe 10 ya mwezi wa tano mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.