Habari za Punde

Zanzibar Mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa wa Magonjwa ya Ubongo na Uti wa Mgongo.

Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Mahmoud Thabit Kombo akizungumza na waandishi wa habari juu ya kufanyika Kongamano la Kimataifa la maradhi ya vichwa maji, uti wa mgongo na kensa ya ubongo litakaloanza kesho katika kituo cha Neurosurgical Mnazimmoja.
Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Jamala Adam Taib (kushoto) na Dkt. Mahmoud Quresh wakimsikiliza Waziri wa Afya (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kituo cha NED Mnazimmoja.
Mwandishi wa habari mwandamizi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar Ramadhani Ali akiuliza swali katika mkutano wa waandishi uliofanyika kituo cha NED Mnazimmoja.
Dkt. Mahmoud Quresh anaesimamia upasuaji wa maradhi ya vichwa maji, uti wa mgongo na kensa ya ubongo katika wodi ya maradhi hayo Hospitali ya Mnazimmoja akitoa ufafanuzi wa masuala ya waandishi wa habari kuhusu kufanyika Kongamano hilo Zanzibar.

Na Ramadhani Ali  Maelezo Zanzibar.                            
Zanzibar itakuwa mwenyeji wa Kongamano la Kimataifa la maradhi ya vichwa maji na uti wa mgongo na kensa ya ubongo litakalofanyika kwa siku tatu kuanzia kesho katika kituo cha maradhi hayo Hospitali Kuu ya Mnazimmoja.

Akizungumza na waandishi wa habari katika kituo cha upasuaji wa maradhi hayo NED, Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo alisema nchi tisa kutoka Afrika, Ulaya na Marekani zitashiriki Kongamano hilo.

Amesema Zanzibar imepewa nafasi hiyo kutokana na juhudi za Rais Shein katika masuala ya elimu na utafiti pamoja na ubora wa kituo hicho na utulivu wa wananchi.

Waziri Mahmoud ameongeza kuwa tokea kuanzishwa kituo hicho miaka miwili iliyopita zaidi ya wananchi 600 kutoka ndani na nje ya Zanzibar wamefanyiwa upasuaji ambapo asimilimia 92 zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Amesema kuwepo kwa kituo hicho Zanzibar kimeipunguzia Serikali mzigo wa kutumia fedha nyingi  kuwapeleka nje wagonjwa wanaokabiliwa na matatizo hayo ambapo gharma zake ni zaidi ya shilingi milioni 12 kwa mgonjwa mmoja.

Ameeleza kuwa kongamano hilo litakalosimamiwa na Daktari bingwa wa maradhi ya vichwa maji, uti wa mgongo na kensa ya ubongo kutoka Marekani Professa Paul Young litakuwa ni fursa pekee kwa madaktari wa Hospitali za Serikali na za watu binafsi kujifunza njia bora za kutibu maradhi ya hayo.

Akieleza malengo ya baadae ya Serikali ya kituo hicho Waziri Mahmoud Thabit Kombo alisema ni kufungua tawi Pemba na kukifanya kuwa kituo kikuu kwa nchi za Afrika Mashariki.

Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Jamala Adam Taib alisema juhudi zinaendelea kusomesha madaktari wazalendo wa kada mbali mbali ikiwemo maradhi ya vichwa maji, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu ili kupata madaktari wa kutosha watakaoendesha kituo hicho baada ya kuondoka wataalamu wa kigeni waliopo hivi sasa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.