STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 19.4.2017
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ameipongeza Serikali ya Cuba kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar
katika kuimarisha sekta ya afya na kueleza haja ya kuendelea na hatua hiyo kwa sekta
nyengine ili kuzidisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya
Zanzibar na nchi hiyo.
Akizungumza na Balozi
mpya wa Cuba katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Lucas Domingo Hernandez
Polledo Ikulu mjini Zanzibar, Dk. Shein
alieleza kuwa uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Cuba na Zanzibar una historia kubwa kwani
nchi hiyo ni ya mwanzo kuyatambua Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964
na kuanzisha ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tokea kipindi
hicho hadi hii leo.
Katika Mazungumzo hayo,
Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Cuba ina historia kubwa katika juhudi za kuiunga
mkono Zanzibar kwenye sekta za maendeleo hasa sekta ya afya kwani tokea mwaka
1966 nchi hiyo imekuwa ikileta madaktari wake kwa awamu kuja kufanya kazi katika
sekta hiyo hapa Zanzibar.
Alieleza kuwa mbali ya
madaktari hao kuja kufanya kazi kwa kutoa huduma ya afya kwa jamii hapa nchini,
pia, Cuba imekuza uhusiano wake kupitia sekta ya afya kwa kushirikiana na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuanzisha chuo cha Udaktari ambacho tayari kimeshaanza
kuzaa matunda kwa kutoa Madaktari Wazalendo ambao hivi sasa wanatoa huduma za
afya hapa nchini.
Dk. Shein alisema kuwa
Madaktari hao kutoka nchini Cuba wamekuwa wakifanya kazi ya kutoa huduma ya
afya kwa wananchi wa Unguja na Pemba usiku na mchana kwa kushirikiana na
madaktari wazalendo.
Aidha, Dk. Shein
alieleza kuwa mbali ya ushirikiano katika sekta ya afya ipo haja ya kuanzishwa
ushirikiano katika sekta ya utalii kutokana na Cuba kupiga hatua kubwa na
kupiga hatua katika sekta hiyo.
Aliongeza kuwa Zanzibar
ina mengi ya kujifunza katika sekta ya utalii kutoka Cuba kutokana na nchi hiyo
kujiimarisha kwenye sekta ya hiyo na kuweza kupata mafanikio makubwa sambamba na kuendeleza vyanzo vyake vya utalii
likiwemo eneo maarufu la ukanda wa kitalii
la ‘Varadero’.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alisema kuwa ushirikiano huo, ni vyema ukahusishwa na Miji Mikongwe ya Zanzibar na Cuba ukiwemo Mji
Mkongwe wa Zanzibar na Mji Mkongwe wa Havana ambayo yote ina historia kubwa pamoja na vivutio kadhaa vya kitalii ndani yake.
Akieleza juhudi za
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta hiyo ya utalii, Dk.
Shein alimueleza Balozi huyo kuwa kumalizika kwa jengo la abiria katika uwanja
wa ndege Kimataifa wa Abeid Amani Karume nako kutachangia ujio wa watalii wengi
kutoka nchi mbali mbali duniani wanaokuja kuitembelea Zanzibar.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alitumia fursa hiyo kumuekleza Balozi huyo haja ya kuwepo kwa
mashirikiano katika sekta ya elimu hasa kwa kuvihusisha vyuo vikuu vya Zanzibar
kikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na vile vya nchini kubwa hasa
katika suala zima la ufanyaji wa tafiti mbali mbali ambazo zitasaidia masuala
mbali mbali kati ya pande mbili hizo.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alisisitiza haja kwa viongozi wa nchi mbili hizo kuimarisha uhusiano kwa
kutembeleana na kubadilishana uzoefu na ujuzi huku akitumia fursa hiyo
kuwakarisha wanachi wa Cuba kuja kuitembelea Zanzibar hatua ambayo itazidi
kuimarisha uhusiano na ndugu zao wa Zanzibar ambao nao watatumia fursa hiyo
kwenda kutembelea nchi hiyo.
Dk. Shein
alimuhakikishia Balozi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza
uhusiano na ushirikiano wake na Cuba kwa lengo la kuimarisha udugu na umoja wao
uliopo wenye kihistoria kwa pande mbili hizo.
Nae Balozi mpya wa
Cuba katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Lucas Domingo Hernandez Polledo
alimueleza Dk. Shein kuwa Cuba inathamini sana uhusiano na ushirikiano wa
kihistoria kati yake na Zanzibar na kuahidi kuwa nchi yake itaendelea kuudumisha.
Balozi Polledo
alimuhakikishia Dk. Shein kuwa Cuba iko tayari kuendeleza uhusiano huo kwa
kuimarisha sekta nyengine za maendeleo ikiwemo sekta ya utalii, elimu na
nyenginezo huku akieleza kuwa hatua ya nchi yake kuleta madaktari wake hapa Zanzibar itaendelea kwani ni ya kihistoria sambamba na
madaktari wa Cuba kutoa mafunzo ya udaktari hapa nchini.
Alisisitiza kuwa
madaktari wa Cuba wanaofanya kazi zao hapa Zanzibar wameridhishwa na kufarajika
na mashirikiano wanayoyapata kutoka kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
pamoja na madaktari wazalendo na
wananchi wake ambao wanazipenda huduma wanazozitoa.
Balozi huyo mpya wa
Cuba alimueleza Dk. Shein hatua za makusudi atakazozichukua katika kuhakikisha
nchi hiyo inaimarisha sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo afya, elimu,
utal;ii na nyenginezo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment