STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 01.04.2017
RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amevitaka vyombo vya
habari vya Serikali kufuatilia kwa karibu matukio na maendeleo ya Serikali kwa kujua
vipaumbele vyake na kuwa vya mwanzo kutoa taarifa muhimu na zilizo sahihi ili jamii
iendelee kujenga imani na Serikali yao.
Dk.
Shein ameyasema hayo leo huko katika ukumbi wa Baraza la Zamani la Wawakilishi
wakati akifungua Semina ya siku moja ya Viongozi, Watendaji Wakuu wa SMZ,
Waandishi wa Habari, Wapiga Picha na Wahariri wa Vyombo vya Habari vya Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Katika hotuba yake ya
ufunguzi huo, Dk. Shein alisema kuwa ni muhimu kwa waandishi wa habari wa
vyombo vya umma kuvifahamu vyema vipaumbele vya serikali na masuala ambayo kwa
wakati huu Serikali imeyatekeleza vizuri na kuwataka viongozi wa taasisi husika
kushirikiana na waandishi wa habari wa vyombo vya umma kutangaza mafanikio
hayo.
Dk. Shein alitumia fursa
hiyo kutoa historia ya vyombo vya habari vya Zanzibar na kusema kuwa Zanzibar
ina historia ndefu ya vyombo vya habari ambapo Sauti ya Tanzania ya Zanzibar
ilikuwa ya mwanzo kuanzishwa Afrika kwenye miaka ya 50 na ya mwanzo kuanzisha
Televisheni ya rangi katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Pia, Shein alieleza
kuridhika kwake na mabadiliko makubwa yanayoendelea kufanywa hivi sasa katika
Shirika la Habari la Utangazaji Zanzibar (ZBC) Radio na TV, pamoja na Gazeti la
Zanzibar Leo ili kuhakikisha vyombo hivyo vinakwenda sambamba na sayansi na
teknolojia.
Aidha, Dk. Shein
aliwataka viongozi wa Serikali na Waandishi wa habari kujenga utamaduni wa
kuweka kumbukumbu za matukio na ahadi za Serikali ili kuweza kufuatilia na
kufahamu hatua za utekelezaji wa ahadi hizo na kwa wakati muwafaka kuiarifu
jamii hali halisi.
Alieleza kuwa hatua hiyo
itaondosha uwezekano wa watu wasioyayajua mambo hayo kueneza habari zisizokuwa
za kweli “Siku hizi tumbaku zimekuwa nyingi na ili tumbaku zisitokezee ni
jukumu la viongozi wa Serikali kutoa taarifa sahihi na wakati sahihi katika
vyombo vya habari”,alisema Dk. Shein.
Dk. Shein alisema kuwa
vyombo vya habari vina umuhimu wa pekee katika kusukuma mbele maendeleo ya nchi
na kukuza demokrasia, hivyo ni lazima ifahamike kwamba inapodhamiriwa kuleta
maendeleo endelevu na kujenga demokrasia ya kweli ni lazima iwepo jamii yenye
uwelewa wa mambo ya ndani na nje ya nchi.
Alisisitiza kuwa ni
jukumu la Serikali kuwapa wananchi taarifa kila inapobidi kupitia vyombo vya
habari na ndipo kutokana na umuhimu huo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimetambua umuhimu huo kwenye
Katiba zake ambapo kwa upande wa Katiba
ya Zanzibar ya mwaka 1984, Sura ya tatu, kifungu cha 18(2).
Aliongeza kuwa vyombo
vya habari vya Serikali vinapaswa kujenga taswira kwa umma kutokana na taarifa
zake inazozitoa na vyombo binafsi na si mbadala wa vyombo vya Serikali bali
vina kazi ya kuongeza nguvu kwa vyombo hivyo.
Aidha, Dk. Shein alisema
kuwa vyombo vya Habari vya binafsi vina kazi ya kushirikiana pamoja na vyombo
vya habari vya Serikali na si kuipinga Serikali kwani lengo ni kuwatumikia
wananchi.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein aliwataka viongozi wote wa Serikali kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu
utekelezaji wa mipango na mikakati ya Serikali kwenye vyombo vya habari na
kutowaogopa waandishi wa habari au kuogopa maswali yao.
Dk. Shein alieleza matumaini yake kuwa baada ya
semina hiyo ukurasa mpya wa maendeleo utafunguliwa katika utoaji wa taarifa kwa
wananchi kupitia vyombo vya habari vya Serikali na hata vile vya binafsi.
Katika maelezo yake Dk. Shein alitumia fursa hiyo
kutoa pongezi kwa waandishi wa Habari wa vyombo vya Habari vya Serikali na vile
vya binafsi kwa kazi nzuri wanazofanya za kutoa habari.
Nae Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo
Rashid Ali Juma alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa kuwa na wazo zuri la
kufanyika kwa Semina hiyo ambayo ni muhimu kwa viongozi na waandishi wa Habari
kwa maendeleo ya nchi.
Aliongeza kuwa Semina hiyo italeta mashirikiano
makubwa hatua ambayo itawasaidia wananchi kuendelea kupata habari kutoka vyombo
vya habari vya Serikali na vile vya binafsi.
Mapema, Katibu Katibu wa Baraza la Mapinduzi na
Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alisema kuwa Semina hiyo ya siku
moja ina madhumuni ya kujenga maelewano na mahusiano mazuri kati ya waandishi
wa habari na viongozi ambao ni watunga Sera pamoja na kuelewa wajibu na
majukumu ya viongozi na waandishi wa habari hasa wa vyombo vya umma.
Katika semina hiyo Mada ya Umuhimu wa Vyombo vya
Habari na Maendeleo ya Taifa ilitolewa na Hassan Abdallah Mitawi ambaye ni
Naibu Katibu Mkuu Habari, katika Wizara ya Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo
na baadae michango mbali mbali ilitolewa.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment