Habari za Punde

Dk: Shein awanyooshea vidole wakandarasi, washauri majenzi


Awataka wawe waangalifu na kazi zao

NA HAJI NASSOR, PEMBA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk: Ali Mohamed Shein, amewataka wakandarasi na washauri elekezi kwenye majengo ya serikali, kuwa makini na kazi zao, kwani fedha zinazotumiwa ni za wananchi, hivyo hazihitaji kuchezewa.

Alisema lazima waelewe kuwa, kila jengo la serikali linalojengwa, zinazotumika huwa ni fedha za walipa kodi, hivyo lazima wawe makini ikiwa ni pamoja na kufuata wakati wa ujenzi na umaliziaji, uliomo kwenye mikataba yao.

Dk: Shein alieleza hayo Daya Mtambwe Wilaya ya Wete Pemba, mara baada ya kupokea maelezo ya kukinza kutoka kwa mjenzi na mshauri elekezi, wanaojenga Chuo cha Amali kilichopo eneo hilo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tano kisiwani humo.

Alisema hata kama jengo hilo linajengwa kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika ADB, lakini itafika wakati mkopo huo unahitajika kulipwa kwa fedha za walipa kodi wa ambo ni waaanzibari.

Alieleza kuwa, ujenzi huo ambao alisema takriban umesimama kwa miezi saba, alikuwa na hamu ya kufika eneo hilo, ili kujionea kwa macho yake, na kujua sababu za kusimama kwa ujenzi huo.

Hivyo amewataka wajenzi ambao ni kampuni ya ZECCON LTD chini ya mshauri elekezi Mohamed Nuren kutoka kampuni ya Newtech Consulting Group ya Sudan, kufikia mwafaka wa haraka, ili jengo hilo lililofikia hatua ya msingi, lijengwe na limalizike kwa wakati.

Dk: Shein alieleza kuwa, jengo hilo linasubiriwa kwa hamu na wananchi, ili walitumie kwa maslahi ya kupata ujuzi na kisha kuwa na njia za kujikwamu na umaskini.

“Mimi nilikuwa na hamu ya kuja kuona mwenyewe, na nimeshayasikia melezo ya pande zote mbili, nimeridhika na fanyeni haraka kuendelea na ujenzi, walu mwakani likamilike’’,alifafanua.

Akizungumza na wanafunzi wa skuli ya Daya Mtambwe mara baada ya kupokea maelezo kwenye jengo hilo la chuo cha Amali, amewataka kuacha anasa na kusoma zaidi, ili wajenga msingi madhubuti wa maisha yao ya baadae.

Alisema lazima wanafunzi katika kipindi hichi, wajielewe kuwa kazi ilioko mblele yao, ni moja tu nayo ni kuwatii wazazi na walezi wao, huku wakisaka elimu kwa hali yoyote.

“Acheni kila jambo lisilo na maslahi na sasa kazi yenu nyinyi ni kusoma na serikali yenu inaendelea kujenga chuo cha amali ili wengine mnaweza kujiunga na kutafuya ujuzi’’,alifafanua.

Dk: Shein aliwakumbusha wanafunzi hao pamoja na wananchi wengine kuwa, ujenzi wa chuo hicho cha amali, alikidahidi mwaka 2010 wakati akiwa kwenye kampeni zake za kuomba kuchaguliwa kuwa rais.

“Kile nilichokiahidi kupitia Ilani ya chama cha mapinduzi ya mwaka 2015 hadi 2020, leo nakitekeleza kwa vitendo, sasa kazi yenu kikimalizika  tuni kusoma kwa bidii na kuchota ujuzi ’’,alifafanua.

Mapema Ali Mbarouk Juma kutoka kampuni ya ZECCON LTD ya Zanzibar, alimueleza rais huyo wa Zanzibar kuwa, kilichosababisha kusita kwa ujenzi wa jengo hilo, ni kutofanyiwa vipimo vya kitaalamu udongo wa eneo hilo.

“Mheshimiwa tatizo lililojitekeza hapa, huu udongo mwengine haukufanyiwa vipimo, ingawa kwa sasa tayari na wakati wowote ujenzi utaendelea’’,alisema.

Awali Rais huyo wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pamoja na ujumbe wake, ulifika eneo la Mzambarau takao na kupokea taarifa ya ukarabati wa barabara ya Madenjani hadi Mzambarau takao.

Dk: Shein alipongeza hatua iliofikwa ya ukarabati wa barabara hiyo, kazi inayofanywa na kampuni ya MECCO ya Tanzania bara, inayoendelea na kuwataka kukamilisha kwa wakati.

“Sawa mimi nimefurahi na nimeona kazi yenu ya ukarabati wa barabara hii, endeleeni na jitahidini mmalize kwa wakati, ili wananchi wapate kuitumia kwa upana’’,alishauri.


Dk Shein yupo kisiwani Pemba kwa ziara ya siku tano, ambapo pamoja na mambo mengine, anatarajiwa kutembelea ujenzi wa barabara ya Ole- Kengeja, kuzungumza na waalimu wa skuli za sekondari, barabara ya Kipapo- Mgelema, Kuyuni- Ngomeni pamoja na kuzungumza na kamati za chama kisiwani Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.