Na Fredy Mgunda, Nachingwea, Lindi.
Mikopo yenye riba kubwa, maarufu kama mikopo ya kausha damu, imekuwa kizingiti kikubwa kwa maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wengi nchini, hasa wafanyabiashara wadogo. Riba kubwa na masharti magumu ya urejeshaji yamewafanya wengi kupoteza mitaji na biashara zao.
Hata hivyo, nuru imeonekana kwa baadhi ya wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi, baada ya serikali kuanzisha mpango wa utoaji wa mikopo isiyo na riba kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri.
Wananchi waliopokea mikopo hiyo, wakiwemo Zawadi Kanga, Ashura Chingu, Husura Mponga na Ramadhani Nambunga – wameeleza jinsi fedha hizo zilivyowasaidia kuondokana na adha ya mikopo yenye masharti kandamizi kutoka kwa taasisi binafsi na mabenki.
“Mikopo hii ya asilimia 10 ni tofauti kabisa. Hatunyonywi tena kama zamani. Tunafanya biashara kwa amani na kurejesha kwa mpangilio mzuri,” alisema mmoja wa wanufaika.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi hundi kwa vikundi mbalimbali, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea, Mhandisi Chionda Kawawa, alisema kuwa mpango huo ni sehemu ya mkakati wa serikali ya awamu ya sita wa kuwawezesha wananchi kiuchumi.
“Mikopo ya kausha damu imekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya wananchi wetu. Halmashauri imedhamiria kuwa sehemu ya suluhisho kwa kutoa mikopo isiyo na riba ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi ya wananchi,” alisema Mhandisi Kawawa.
Kwa mujibu wa Kawawa, jumla ya shilingi 649,781,998 zimetolewa kwa vikundi 54 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ili kuwainua kiuchumi na kuchangia pato la taifa kupitia shughuli zao za uzalishaji.
Aidha, aliwataka wanufaika kutumia fedha hizo kwa uangalifu na kurudisha mikopo kwa wakati ili kuwezesha mzunguko wa fedha kwa vikundi vingine.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri hiyo, Bi Stella Kategile, aliwakumbusha wanavikundi umuhimu wa uaminifu na nidhamu ya fedha.
“Wakirejesha kwa wakati, watakuwa wamefungua milango kwa wengine kunufaika. Pia, wataweza kukopa zaidi ya walichopata awali,” alisisitiza Bi Kategile.
Mpango huu wa mikopo isiyo na riba unatajwa kuwa mfano wa kuigwa katika kupunguza utegemezi na kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za kiuchumi vijijini.
No comments:
Post a Comment