STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Pemba 03.04.2017
RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein amewataka
wananchi watambue kwamba huu si wakati tena wa kukaa maskani wakapeana ahadi
zisizokuwepo na badala yake wafanye kazi na Serikali yao itaendelea kuwaunga
mkono kwa kuwapelekea maendeleo popote pale walipo.
Dk. Shein aliyasema hayo katika hafla ya uzinduzi wa barabara ya Mgagadu-Kiwani,
Mkoa wa Kusini Pemba, iliyojengwa kwa fedha za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
ambapo kazi za ujenzi imefanywa ka kusimamiwa na Wizara ya Ujenzi Mawasiliano
na Usafirishaji kupitia Idara ya Ujenzi na Utunzaji UUB.
Katika
hotuba yake kwa wananchi, Dk. Shein aliwaeleza wananchi kuwa wakati wa kupiga
siasa umekwisha na kilichokuwepo hivi sasa ni kufanya kazi kwa kila mmoja
alieajiriwa na asieajiriwa na wale wanaojishughulisha na kilimo waendelee na
shughuli zao hizo kwa lengo la kujiletea maendeleo.
Alisema
kuwa uchaguzi haupo tena hadi mwaka 2020 na kuongeza kuwa vyama vya siasa vipo
lakini hakuna chama kitakacholeta Serikali nyengine kwani tayari Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar ipo madarakani ambayo imekuwa ikiwaheshimu na kuwapelekea
maendeleo wananchi popote pale walipo.
Dk.
Shein alisema kuwa yeye ndie Rais wa Zanzibar na kila analosema ana uhakika
nalo kwani hana kawaida ya kusema uwongo, hivyo aliendelea kuwaasa wananchi kisiwani
humo kuendelea na shughuli zao na kutosikiliza tumbaku za mitaani.
“Wananchi
wafanye kazi na zingatieni maelezo ninayosema mbali ya kuwa mimi ndie Rais wenu
pia, ni mwenenu na ndugu yenu…mjue kuwa hapa hakuna Serikali nyengine
itakayokuja kwani serikali halali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo na itaendelea
kuwepo”alisema Dk. Shein.
Aidha,
Dk. Shein aliwaeleza wananchi katika hafla hiyo kuwa barabara hiyo ni ya watu
wote na waitumie kwa maslahi yao kwani fedha zilizojengewa zinatokana na kodi
za wananchi wa Unguja na Pemba huku akiwataka waitunze na kuienzi.
Alisema
kuwa Serikali inaendelea kutimiza ahadi yake ya kuwapelekea wananchi maendeleo
huku akiwaeleza wananchi kuwa bado ujenzi wa barabara nyengine muhimu
unaendelea tena kwa kiwango cha lami kisiwani humo.
Pamoja
na hayo, Dk. Shein aliwaeleza wananchi wa Kiwani na vitongoji vyote ilikopita
barabara hiyo, kuanzia Mgagadu, Kivumoni, Minazini, Kirimdomo, Kendwa,
Jundamiti hadi kufikia Kiwani Pwani kuwa kufunguliwa kwa barabara hiyo ni
furaha kubwa kwao.
Miongoni
mwa barabara ambazo Dk. Shein alizitaja kuwa zimo katika ujenzi ni barabara ya
Ole-Vitongoji, Pujini hadi Kengeja yenye kilomita 35 imeanza kwa kifusi na
baadae itatiwa lami huku akieleza azma ya ujenzi wa barabara ya Chake Chake-Ziwani hadi Wete nayo
itajengwa kwa kiwango cha lami ambapo ujenzi wake utaanza si muda mrefu.
Dk.
Shein alisema kuwa Zanzibar inaendelea kwa kasi kubwa katika kuimarisha sekta
zake za maendeleo na kuwahakikishia wananchi kuwa ahadi zote zilizoahidiwa
zitatekelezwa.
Sambamba
na hayo, Dk. Shein aliwaahidi wananchi wa Kiwani kuwa kisima chao kitatiwa
umeme chini ya miezi miwili na nyumba ya daktari itajengwa, ahadi hizo
zinatokana na ombi la wananchi hao lililotolewa na Mzee Omar Khamis ambaye nae
alitumia fursa hiyo kumshukuru Dk. Shein kwa niaba ya wananchi wa Kiwani.
Nae
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Balozi Ali Karume alisifu
mashirikiano makubwa yaliopo katika Wizara yake hali ambayo ndio chachu ya
mafanikio katika Wizara hiyo.
Balozi
Karume alisifu juhudi za Dk. Shein za kutekeleza ahadi anazoziahidi na kueleza
kuwa ni kiongozi wa pekee anaefuatilia kwa karibu miradi ya maendeleo katika
Serikali anayoiongoza huku akisisitiza umuhimu wa uzalendo.
Mapema
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Mustafa Aboud
Jumbe akitoa taarifa fupi juu ya ujenzi
wa barabara hiyo alisema kuwa ujenzi huo ni mojawapo ya jitihada ambazo Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikichukua tokea Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka
1964 ya kujenga ustawi wa wananchi katika kuimarisha miundombinu ya barabara za
mijini na vijijiji kwa Unguja na Pemba.
Alisema
kuwa ujenzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya maendeleo, Mkuza III, Sera
ya Taifa ya Usafiri pamoja na Mpango Mkuu wa Usafiri Zanzibar na Ilani ya
Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi.
Aliongeza
kuwa Mradi wa ujenzi wa barabara ya Mgagadu-Kiwani ulianza rasmi mwaka 2009 na
umechukua muda mrefu kukamilika kutokana na changamoto mbali mbali
zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wake.
Katibu
huyo alieleza kuwa Februari 2017 barabara hiyo imekamilika rasmi kwa kiwango cha
lami mpaka pwani ambapo ujenzi wake ulikuwa wa awamu tatu.
Mradi
huo umefadhiliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia fedha za
maendeleo kutoka Mfuko Mkuu wa Hazina kwa hatua ya awali pamoja na Mfuko wa
Barabara Zanzibar kwa hatua za ukumilishaji wa ujenzi kwa gharama za Tsh
Bilioni 1.4 .
Alieleza
kuwa Barabara hiyo ina kilomita 8.85 ambapo hapo awali ilipangwa kujengwa
kilomita 7.6 na ongezeko la kilomita 1.25 limekuja kutokana na agizo la Rais
mara baada ya wananchi wa Kiwani Likoni kumuomba barabara hiyo iwekwe lami hadi
pwani na yeye alikuba kutokanan na umhimu wake.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment