Habari za Punde

Washauri waajiri kuwafanyia uchunguzi wa afya waajiriwa kila baada ya muda

NA HAJI NASSOR, PEMBA

WANANCHI wa wilaya za Micheweni na Wete kisiwani Pemba, wamependekeza kuwa lazima, kuwe na kifungu kwenye sheria ya fidia inayofanyiwa marekebisho, cha kuwalazimisha waajiri kuwafanyia uchunguzi wafanyakazi wao, kila baada ya muda kabla ya kustaafu kazini rasmi.

Wamesema waajiiri hutambua umuhimu wa kumchunguza mtu afya yake, kwenye mchakato wa kutaka kumuajiri ili atambue ugonjwa wake, ingawa baada ya kumuajiria jambo hilo hupotea.

Wakichangia maoni yao kwa nyakati tofauti, wakati Tume ya Kurekebisha sheria ilipokutana nao, ili kutoa mchango wao wa kuzifanyia marekebisho sheria za fidia na sualama kazini, walisema lazima kiwemo kifungu hicho.

Walieleza kuwa, afya ya mfanyakazi hudhoofika sana kutokana na kazi anayoifanya, hivyo kama muajiri atalazimika kisheria kumfanyia uchunguuzi muajiriwa wake, anaweza kutibiwa kwa gharama za ofisi.

Mmoja kati wananachi hao, Ali Omar Mbarawa anaefanyakazi hospitali ya Wete, alisema lazima kuwe na timu ya wataalamu ya kuwachunguza wafanyakazi, magonjwa kdhaa kama anavyofanyiwa kabla ya kuajiriwa.

“Suala la matibabu kwa sasa linagharama kubwa sana, sasa lazima kama tunataka kuwatendea haki wafanyakazi wetu, lazima muajiri kisheria apewe jukumu la kufanya uchunguuzi wa kiafya”,alipendekeza.

Nae Afisa Utumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Micheweni Hamad Mbwana Shaame, alisema kama kikiwemo kifungu cha sheria kwenye sheria ya usalama kazini, hata waajiri watachunga vyema, haki za wafanyakazi wao.

Kwa upande wake mwalimu wa skuli ya sekondari Micheweni Hassan Haji Faki, alisema waalimu wamekuwa wakiishi kwenye vumbi la chaki, hivyo lazima fidia iwepo ili kutibu afya zao.

Hata hivyo afisa kutoka Idara ya Mazingira Pemba, Ali Abdi Mohamed alisema lazima wanaoanguka mikarafuu, wapatiwe fidia kwa wakati, ili wapate fedha za matibabu.

Akizungumza kwenye mikutano hiyo, mwanasheria Mohamed Ali Ahmed, aliwataka wafanyakazi na wananchi wengine, waondoe utamaduni wa kutodai haki zao kwa mujibu wa sheria zilizopo.

“Lazima tujengeni utamaduni wa kufuatilia na kudai haki zetu hasa tunapopatwa na ajali tunapokuwa kazini, maana kwa mujibu wa sheria, mwajiri anapaswa afidie matibabu yako”,alifafanua.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mshibe Ali Bakar amesema, lazima wafanyakazi wafahamishwe namna ya kupata haki zao, hasa za fidia na za matibabu wanapokumbwa na hasara wanapokuwa kazini.

Tume ya kurekebisha sheria Zanzibara ilikuwa kisiwani Pemba kwa ziara ya siku tano, kukutana na wadau mbali mbali wakiwemo wafanyakazi serikali, ili kukusanya maoni juu ya kuzifanyia marekebisho, sheria za fidia na ile ya usalama kazini, ambapo pia walitembelea kiwanda cha makonyo kilichopo Wawi Chakechake Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.