Habari za Punde

Mahakama Yakubali Shkuba na Wenzake Wakashtakiwe Marekani


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeyakubali maombi ya Serikali ya Marekani ya kuwataka raia watatu wa Tanzania akiwemo Mfanyabiashara Bilionea, Ally Khatib Hajj ‘Shkuba’ ili waende kujibu tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya nchini humo. 

Mbali ya Shkuba, watuhumiwa wengine waliotakiwa na serikali hiyo ya Marekani ni mfanyabiashara Idd Mafuru na Lwitiko Adam.
Shkuba alikamatwa na Serikali ya Tanzania mwaka 2014 kwa kusafirisha kiasi cha kilo 210 za Heroin, ambazo zilikamatwa Januari, 2012 mkoani Lindi.

Maombi ya Marekani, yaliwasilishwa na aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Harrison Mwakyembe kupitia Wakili wa Serikali Mkuu, Edwin Kakolaki yalianza kusikilizwa toka juzi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Cyprian Mkeha.

Akitoa uamuzi wa maombi hayo leo, Hakimu Mkeha alisema kuwa mahakama imekubaliana na maombi hayo.

Alisema kuwa kabla ya kutoa uamuzi huo, mahakama hiyo imepitia hoja za pande zote mbili ikiwemo serikali na utetezi wakati wa usikikizwaji wa maombi hayo.

Alisema kuwa licha ya mahakama hiyo kukubaliana na hoja za Serikali ya Marekani kupitia Waziri wa Tanzania wajibu maombi (Shkuba) wana haki ya kukata rufaa ndani ya siku 15.

“Mahakama imekubaliana na maombi haya lakini wajibu maombi wakae mahabusu hadi hapo waziri atakapotoa kibali ili wasafirishwe kwenda Marekani. Lakini wanaweza kukata rufaa kabla ya waziri hajatoa kibali ndani ya siku hizo 15,” alisema.

Awali katika usikilizwaji huo ambao wajibu maombi wanatetewa na jopo la mawakili watatu akiwemo Majura Magafu, wakili Kakolaki alieleza kuwa waziri mwenye dhamana alipelekewa maombi ya kutakiwa kwa Shkuba na wenzake Aprili 4, mwaka huu.

Baada ya kuwasilishiwa maombi hayo aliyowasilisha mahakamani, ambapo ilitolewa amri ya kukamatwa kwa washtakiwa wote watatu, ambao walikamatwa Aprili 6, mwaka huu na walifikishwa mahakamani.

Kabla ya kuwasilishwa kwa maombi hayo, Machi 9, mwaka jana, serikali ya Marekani kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Wizara ya Fedha inayoshughulikia udhibiti wa mali za nje (Foreign Assets Control-OFAC), ilimtaja Shkuba kuwa ni kinara mkuu wa kimataifa wa usafirishaji wa tani za dawa za kulevya ikiwemo Heroin na Cocaine kwenda Afrika, Ulaya, Asia na Marekani ya Kaskazini.

Na Denis Mtima/GPL

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.