Habari za Punde

Uzinduzi wa Uwashaji Mwenge Katavi

Balozi Seif akimkabidhi mwenge wa Uhuru Kiongozi wa Mbio za Mwenge mwaka huu Nd. Amour Hamad Amour kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja hapo kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Mwenge Mjini Mpanda mkoani Katavi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwasha Mwenge wa Uhuru kuashiria kuzindua Rasmi Mbio za Mwenge huo mwaka huu kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein hapo katika uwanja wa Kumu kubmu ya Mwenge wa Uhuru Wilayani Manda Mkoa wa Katavi.
Balozi Seif akisalimiana na Mmoja wa Vijana walioteuliwa kutembeza mwenge wa Uhuru mwaka Huu Nd. Salome Obadia Mkoa Mkoa Mwenyeji wa Mwenge wa Uhuru wa Katavi.
Vijana Sita walioteuliwa kuutembeza Mwenge wa Uhuru katika Mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar waki makini kufuatilia matukio mbali mbali yaliyojiri kwenye uzinduzi wa mbio hizo Mkoani Katavi.
Vijana wa Halaiki wakionyesha umahiri wao kwenye sherehe za uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu zilizofanyika katika uwanja wa Kumbukumbu ya Mwenge wa Uhuru Wilaya ya Mpanda Mkoani
Katavi.
Akina Mama wa Kikundi cha Utamaduni cha Nsimba cha Wilaya ya Manda Mkoani Katavi wakitoa burdani kwenye uzinduzi wa mbio za mwenge wa Uhuru ambapo Mgeni rasmi alikuwa Makamuj wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa niaba ya Rais Wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein.
Baadhi ya Mawaziri na Viongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa wakionekana kuhamasika kutokana na midundo ya ngoma ya Kibati iliyopigwa na Kikundi cha Utamaduni cha JKU kutoka Zanzibar hao Mkoani Katavi.(Picha na Hassan Issa OMPR.)  

Na Othman Khamis OMPR.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduai Dr. Ali Mohamed Shein alisema Falsafa ya Mwenge wa Uhuru inastahiki kuendelezwa kwa vile bado jitihada za kuwakomboa Watanzania hazijafikia mwisho licha ya kupatikana kwa Uhuru na Tanganyika Mwaka 1961 na Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964.


Alisema Falsaha hiyo ni muhimu na kichocheo kikubwa katika kuhamasisha juhudi za Maendeleo, Umoja, Uzalendo, Mshikamano na kudumisha amani ndani na nje ya mipaka ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dr. Ali Mohamed Shein alitoa kauli hiyo katika sherehe za uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Mwenge wa Uhuru Wilayani Mpanda  Mkoani Katavi katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yakena Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Alisema Falsafa hiyo ina mchango mkubwa katika kuibua hamasa za kufanya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyowakomboa Wananchi wanyonge wa Zanzibar na hatimae kuasisiwa kwa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo Tarehe 26 Aprili 1964 ambapo mwezi huu unatimiza miaka 53 kwa mafanikio makubwa.

Rais wa Zanzibar alisisitiza kwamba kutokana na umuhimu wa dhamitra ya kuanzishwa kwa mbio za Mwenge wa Uhuru na mafanikio yanayoendelea kupatikana kupitia utekelezaji wa ujumbe wa mbio hizo na uhamasishaji na shughuli mbali mbali za maendeleo, Serikali zote mbili zitaendelea kuienzi na kuiendeleza falsafa hiyo kwa vitendo.

Dr. Shein alisema Ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru wa Mwaka huu usemao “ Shiriki Kukuza Uchumi wa Viwanda na Maendeleo ya Nchi Yetu ” kwa kiasi kikubwa unatilia maanani dhamira ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwa na Uchumi wa Kati ifikapo Mwaka 2025.

Alisema hatua hiyo itafikiwa kwa kuwa na Uchumi wa Viwanda iwapo Taifa litakuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa bora zitakazoweza kuhimili ushindani wa soko la Kimataifa badala ya kuendeleza kuzalisha mali ghafi na kuwa soko la bidhaa za Viwanda kutoka Mataifa mengine.

Rais wa Zanzibar alieleza ni dhahiri kwamba uwekezaji katika Viwanda una mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa, kuchochea ukuaji wa sekta nyengine za Maendeleo.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza furs za ajira hasa kwa Kundi kubwa la Vijana na kuwawezesha kukidhi mahitaji yao ya lazima pamoja na kuimarika kwa huduma za Kijamii katika maeneeo mbali mbali ya Nchi.

Dr. Shein alifahamisha kwamba uzoefu unaonyesha wazi kuwa  Mataifa yaliyopiga hatua kubwa ya Kiuchumi Duniani yaliamua kuwekeza katika maendeleo ya Viwanda. Hivyo Jamii nzima ina mchango katika kufikia dhamira hiyo ili kupiga hatua zaidi kwenye nyanja zote za Maendeleo ya Taifa.

Alisema katika kuchochea Maendeleo ya Viwanda Nchini, Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imeandaa Mkakati wa kujenga uchumi wa Viwanda unaohusisha sekta zote za uchumi katika kipindi cha miaka Mitano {2015 -2020}.

Dr. Shein alisema Mkakati huo una malengo ya kuendeleza sekta ya Viwanda ambayo itazalisha kwa ajili ya kutosheleza mahitaji ya Taifa na kukidhi matihaji ya bidhaa ambazo zinanunuliwa kwa wingikutoka nje ya nchi.

Alisema mkakati huo utaendea sambamba na kuazishwa kwa nyororo wa tahamani kwa viwanda ambavyo vitaunganisha na kuleta uwiano wa maendeleo ya kiuchumi Vijijini na mijini kwa kuunganisha tasnia za uzalishaji wa awali wa malighafi za Viwanda kama kilimo, uvuvi, misitu na madini.

Alieleza kuwa Serikali imeweka mazingira mazuri na mifumo thabiti ya kusaidia kuendeleza shughuli mbali mbali za Viwanda, ikiwa ni pamoja na kuanzisha maeneo  maalum ya uwekezaji ya SEZ na EPZ.

Alisema Wananchi wanayo nafasi kubwa katika kujenga na kuendeleza Viwanda hapa Nchini kwa vile ukuaji wa uchumi wa Viwanda unaanza na jitihada za Wananchi katika kuanzisha na kuendeleza sekta hyo katika maeneo yao.

Alifafanua kwamba ni vyema vikaanzishwa viwanda vya aina hiyo katika sekta  za Kilimo, Uvuvi, Madini, Ujenzi na Mawasiliano ili ifikie hatua ya Wananchi wote kwa pamoja wanaimba wimbo wa viwanda nchi nzima kwa vitendo.

“ Naamini kupitia mbio za mwenge wa Uhuru za mwaka huu tutaweka njia thabiti ya kuelekea kule tunakokusudia kwnenda”. Alisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dr. Shein alisema dhamira kama hiyo inatekelezwa kwa kuhamasisha kasi ya uwekezaji katika sekta mbali mbali za kiuchumi kupitia Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi {ZIPA}.

Alisema uhamasishaji pia umelengwa kwa miradi ya pamoja kati ya Sekta Binafsi na Sekta za Umma {PPP} pamoja na kuendeleza viwanda katika maeneo huru ya Uchumi ya Fumba kwa Kisiwa cha Unguja na Micheweni kwa Kisiwa cha Pemba.

Alisema katika kipindi hicho Serikali ya Mapinduizi ya Zanzibar imeshaidhinisha  jumla ya Miradi 51 ya Uwekezaji yenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 497.92 ambapo katika miradi hiyo asilimia 53 ni Miradi inayomilikiwa na Wazalendo.

Dr. Shein alifahamisha kwamba Miradi hiyo inatarajiwa kutoa ajira zipatazo Elfu 2,658 na itakwenda sambamba na dhamira ya kupunguza tatizo la ajira na kuondoa umaskini.

Akizungumzia janga la dawa za kulevya nchini Dr. Ali Mohamed Sheinn alisema Serikali zote mbili zinaendelea na mapambano dhidi ya dawa hizo kwa nguvu zake zote kufuatia operesheni ya ukamataji wa dawa hizo unaoendeshwa na vikosi vya ulinzi na kuleta mafanikio makubwa hapa nchini.

Alisema katika kipindi cha Mwei Januari hadi Disemba mwaka 2016 idadi ya watuhumiwa 16,026 walikamatwa na kiasi cha Kg 13.129 za Heroin, Kg 17.33 Cocaine, Kg 56.739  za Bangi na Kig 14.863 za Mirungi.

Kwa upande wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein alisema kati ya Tarehe 23 Febuari 2017 na Tarehe 21 Machi 2017 jumla ya watuhumiwa 168 walikamatwa na kuhojiwa na vyombo vya ulinzi.

Alisema katika kipindi hicho watumiaji 245 walikamatwa na kuhojiwa pamoja na kukamata aina mbali mbali za dawa za kulevya ikiwemo Heroin na Cocaine, Bangi na Mirungi ambapo kesi 87 zimeshafunguliwa na ziko katika hatua  mbali mbali za kushughulikiwa kisheria.

Akitoa salamu kutoka Serikalio ya Mapinduzi ya Zanzibar Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Vijana, Wazee, Wanawake na Watoto Mh.Moudline Cyrus Castico alisema Mbio za Mwenge wa Uhuru ni faraja kwa kuleta mshikamano miongoni mwa Watanzania katika masuala ya Kijamii, Kisiasa, Utamaduni na hata Biashara.

Mh. Castico alisema mshikano huo unastahiki kudumishwa na kuendelezwa kwa faida ya Wananchi wote vyenginevyo iko siku Vizazi vijavyo vinaweza kuwasuta Wazazi na Viongozi endapo Muungano wa Tanganyika utatetereka jambo ambo hata Dunia italishangaa Taifa la Tanzania lilikuwa kigezo cha Amani Duniani.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na  Wenye Ulemavu Mh. Jenista Joaqim Muhagama alisema mbio za Mwenge wa Uhuru zimekuwa zikitumika katika kichocheo cha Maendeleo Nchini.

Mh. Jenista alisema Wizara zinazosimamis Mwenge wa Uhuru Bara na Zanzibar zitaendelea kuhamasisha Wananchi kushiriki vyema katika mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya, Ukimwi na udhalilishaji wa Kijinsia kwa kuchapisha vipeperushi wanatavyopewa Wananchi.

Vijana Sita wamepata mafunzo maalum  watautembeza Mwenge wa Uhuru katika Mikoa yote 31 ya Tanzania bara na Tanzania Zanzibar ambao unatarajiwa  kuchukuwa siku 195.
Vijana hao ni Ndugu Bahati Lugodisha Kutoka Mkoa wa Geita Ndugu Fatma Yunus Hassan Mkoa wa Kusini Pemba, Nd. Fredrick Joseph wa Mkoa wa Singida, Salome Obadia kutoka Mkoa wa Katavi, Shukuru Islam  Msuri Mkoa Mjini Magharibi na Kiongozi wa Mbio hizo Nd. Amour Hamad Amour kutoka Mkoa Kaskazini Unguja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.