NA HAJI
NASSOR, PEMBA
WAKULIMA wa
zao la muhugo wilaya ya Mkoani Pemba, wamelalamikia tabia iliojitokeza kwa
kuibiwa mbegu zao za muhogo, ambapo
baadhi yao huiba na muhogo, jambo ambalo linawarejesha nyuma.
Walisema mara baada ya mvua kuanza kunyesha
kwa kasi, wapo baadhi ya wenzao, wamekuwa na mtindo wa kukata mbegu na wengine
kuiba na muhogo, na kuziuza kwa wakulima wengine.
Wakizungmza na mwandishi wa habari
hizi kwa nyakati tofauti kufuatia mkulima Mohamed Salim Juma wa Mtuhaliwa
kung’olewa visiki vyake vya muhogo 200 alivyovipanda siku moja, walisema hali
kwa sasa inatisha.
Walisema imekuwa ni jambo la kawaida
hasa baada ya mvua kuanza, kuibiwa mbegu zao au wakati mwengine hata kuibiwa
mbegu ambazo tayari zimeshapandwa kabla ya kuanza kuota.
Mmoja kati ya wakulima hao, Mohamed
Salim Juma wa Mtuhaliwa, alisema yeye juzi alipofika kwenye shamba lake,
aligundua kung’olewa kwa mbegu zake 200 alizokwishazipanda.
Alisema baada ya mvua kuanza,
alipigisha matatu kadhaa, na siku ya pili kununua mbegu za muhogo na kuzipanda,
ingawa hakuzikuta.
“Visiki vyangu 200 vya muhogo
vimeibiwa kimoja baada ya chengine, jamani huu ni kuzidishana umaskini, baada
ya kuniibia muhogo, sasa na mbegu mpaka nilizokwisha kuzipanda’’,alilalamika.
Nae Mwamini Haji Ussi wa Mkanyageni alisema,
yeye aliibiwa mbegu kwa katwa katwa na kisha watu hao wasiofahamika kung’oa na
muhogo robo eka.
“Hata mie ni kweli juzi niliibiwa
mbegu na muhogo kwenye shamba langu, maana kipindi hichi cha mvua, kila mmoja
anataka kulima, ni kutokana na uhaba wa mbegu’’,alifafanua.
Kwa upande wake Kassim Bendera Vuia
wa Mtambile, alisema alilazimika kutoa taarifa kituo cha Polisi Mtambile
kufuatia kuibiwa mbegu zake zaote.
“Mimi niliibiwa mbegu tu, lakini
muhogo wala haukung’olewa, na bahati nzuri, nilizikamata eneo la Jiondeni
Mkoani, ingawa mwizi sikumjua’’,alinifahamisha.
Alifafanua kuwa, alipotaka taarifa za
ndani juu ya wapi mbegu hizo mnunuaji huyo amezipata, alimueleza kuwa alinunua
eneo la Mizingiani njia ya Wambaa, ingawa baada ya kufuatilia aligundua kuwa ndie
aliefanya hivyo ni jirani yake.
Mwananchi Bakari Haji Bakari wa
Kengeja, alisema wamekuwa wakati mwengine wakilinda mashamba yao kwa kwenda
mapema na kuchelewa kurudi kwa kuhofia wizi wa mbegu.
Sheha wa shehia ya Mtambile Rajab
Risasi, alisema hayajapokea taarifa zozote za wizi wa mbegu, na kuitaka jamii
kuendelea kukinawirisha kikosi cha polisi jamii.
Katika wiki tatu sasa tokea kuanza
kwa msimu huu wa mvua, kumekuwa kikiibuka malalamika kila siku, kutokana na
wakulima wa zao la muhugo kuibiwa mbegu na muhogo.
No comments:
Post a Comment