Habari za Punde

Balozi Seif awafariji waliojeruhiwa na shambulio la kisu

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  Ali Iddi akiwafariji na kuwapa pole Raia wa Ujerumani wa kwanza kulia yake ni Anna Catharina Raia Miaka 20 na Bibi Jennifer Wolf  Miaka 24.Wa Kwanza kutoka Kushoto  ni Balozi Mdogo wa Shirikisho la Ujerumani aliyepo Zanzibar Bwana  Dominic Warth
Balozi Mdogo wa Shirikisho la Ujerumani aliyepo Zanzibar Bwana Dominic Warth akibadilishana mawazo na Balozi Seif baada ya kuwafariji Raia wa Nchi yake hapo katika Kituo cha Ufundi cha Pamoja Zanzibar Bweni.

 Balozi Seif  akimfariji Bwana Mauget Gerarol  Raia wa Ufaransa mwenye Umri wa Miaka 66 aliyejeruhiwa Jicho na kulazwa Hospitali ya Global Mnazi Mmoja.

Kati kati yao ni Daktari wa Mgonjwa huyo wa Hospitali ya Global Daktari Marisel kutoka Nchini Jamuhuri ya Cuba.
 Mwakilishi wa Jimbo la Tunguu ambae ni mdau mkubwa wa Sekta ya Utalii Zanzibar  Mh. Simai  Mohammed Said akimfariji Bwana Mauget Gerarol  Raia wa Ufaransa mwenye Umri wa Miaka 66 aliyejeruhiwa Jicho na kulazwa Hospitali ya Global Mnazi Mmoja.
Daktari wa Hospitali ya Global Dr. Marisel akimueleza Balozi Seif juhudi zilizochukuliwa na Hospitali hiyo katika kumpatia matibabu  Bwana Mauget Gerarol.Wa kwanza kutoka Kulia ni Mwakilishi wa Jimbo la Tunguu ambae ni mdau mkubwa wa Sekta ya Utalii Zanzibar  Mh. Simai  Mohammed Said.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa anzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kamwe haitokuwa tayari  kuona baadhi ya Watu wanafanya vitendo  vya hatari  vinavyotishia maisha ya Wananchi pamoja na Wageni wanaoingia Nchini.

Alisema vyombo vya Dola vitaendelea kudhibiti hali hiyo ili kutoa fursa kwa Wananchi na Wageni hao hasa wale wanaoingia Nchini kwa shughuli za Kitalii kufanya  mambo yao katika misingi ya amani na utulivu.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti wakati alipowatembelea Bibi Jennifer Wolf  Raia wa Ujerumani mwenye Umri wa Miaka 24 hapo kwenye Makaazi yao Mbweni aliyejeruhiwa Kichwani kwa kuchomwa Kisu  na Bwana Mauget Gerarol  Raia wa Ufaransa mwenye Umri wa Miaka 66 aliyejeruhiwa Jicho na kulazwa Hospitali ya Global Mnazi Mmoja.

Hata hivyo Raia huyo wa Ufaransa Bwana Gerarol ameamuliwa kupelekwa Jiji Dar es salaam kwa matibabu zaidi wakati wenzao wengine Anna Catharina miaka 20 raia wa Ujerumani, Liying Liang Raia wa Canada, Hassan Abdulla Abdulla wa Kiponda na Sajad  Hussein wa Mkunazini walipata matibabu na kuruhusiwa kurudi Nyumbani kufuatia mkasa uliowakumba wakati wakipata huduma za Chakula Juzi usiku katika Mkahawa la Loukman Mkunazini.

Balozi Seif akiwafariji majeruhi hao alisema ni jambo la kusikitisha kuona  baadhi ya Watu wanaamua kuhatarisha maisha ya wenzao bila ya sababu za msingi jambo ambalo vyombo vya ulinzi vitapambana nayo kwa nguvu zote.

Aliwataka waathirika wa tukio hilo la kusikitisha kuwa na moyo wa subra wakielewa kwamba mitihani ni mambo wanayopambanao nayo wanaadamu katika shughuli na harakati zao za kimaisha za kila siku.

Alisema yapo matukio ya kuhatarisha maisha ya watu yanayotokea na kuripotiwa na vyombo mbali mbali vya Habari katika sehemu mbali mbali Duiniani yakihusisha utashi wa mtu bila ya kuzingatia athari inayoweza kuikumba Jamii inayozunguuka maeneo husika.

Akielezea mikakati iliyowekwa na Jeshi la Polisi katika kupambana na vitendo vya kihuni na kuhatarisha maisha ya Raia Kamanda wa Polisi Mkoa Mjini Magharibi Kamishna Msaidizi Muandamizi wa Polisi Hassan Nassir Ali alisema tukio hilo ni uhalifu wa kaiwaida uliowakumba  sio wageni pekee bali hata watu wengine waliokuwepo sehemu hiyo.

Kamanda Nassir alisema Jeshi la Polisi limeshabaini mtuhumiwa wa tukio hilo ni Kijana anayejihusisha na utumiaji wa Dawa za kulevya lakini bado anaendelea kufuatiliwa ili atiwe mikononi kwa ajili ya kujibu makosa yanayomkabili.

Mapema Balozi Mdogo wa Shirikisho la Ujerumani aliyepo Zanzibar Bwana Dominic Warth  pamoja  na Mke wa Mjeruhiwa wa Kifaransa Bibi Makhtin Mauget wameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia vyombo vyake vya ulinzi kwa hatua ilizochukua kukabiliana na tukio hilo.

Bwana Dominic na Bibi Makhtin walisema  wao pamoja na majeruhi  wao wamepata faraja kubwa iliyowapa matumaini  ya kuendelea kuwa mawazo ya kutaka kuityembelea Tanzania na Zanzibar kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.