STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Djibouti 9.05.2017
MKE wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein
ameeleza kuwa Wanawake wana nafasi kubwa ya kusimamia na kuendeleza Sera na
Mipango ya Serikali ya kuendeleza na kusimamia wa wanawake na watoto.
Mama Shein aliyasema
hayo kwa nyakati tofauti katika hotuba yake aliyoitoa mara baada ya kutembelea
Kituo cha Watoto pamoja na Makao Makuu ya Kitaifa ya Wanawake wa Djiboti vyote
vilivyopo mjini Djibouti.
Katika hotuba yake, Mama
Shein alisema kuwa katika ziara yake hiyo amefurahishwa kwa kiasi kikubwa kuona
juhudi za makusudi zinazochukuliwa na Serikali ya Djibouti katika kuwawezesha
wananwake sambamba na kuwatunza watoto.
Aliongeza kuwa amepata
kujifunza mambo mengi ambayo yanawapasa akina mama na watoto katika maendeleo
yao utoaji wa elimu na mafunzo mbali mbali wanayopewa wanawake ambayo baada ya
kumaliza huweza kuyafanyia kazi na kuweza kujiajiri wenyewe huku watoto nao
wakipata mafunzo ambayo huwaendeleza katika maisha yao.
Aidha, Mama Shein
alisema kuwa umefika wakati kwa Wanawake wa Zanzibar kushirikiana na kufanya
kazi kwa pamoja na wanawake wa Djibouti kwa lengo la kuwaendeleza wanawake
kiuchumi, usawa wa kijinsia pamoja na haki za watoto.
Alisisitiza kuwa ni
vyema kwa kila mmoja kwa pande mbili hizo kulifanyia kazi suala hilo ili
kuhakikisha linafanikiwa.
Pamoja na hayo, Mama
Shein alieleza haja ya kuwepo kwa ziara mbalimmbali za kubadilishana uzoefu na
utaalamu kati ya viongozi wa kike wa Zanzibar na wa Djibouti.
Sambamba na hayo, Mama
Shein alitoa pongezi na shukurani za pekee kwa Rais wan chi hiyo Ismail Omar
Guelleh kwa mwaliko wake aliofanya kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kutembelea nchi hiyo hatua ambayo itazidisha
na kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya pande mbili hizo.
Pia, Mama Shein alitumia
fursa hiyo kutoa pongezi kwa wananchi na viongozi wote wa Djibouti wakiwemo
viongozi wanawake wan chi hiyo kwa moyo wao mzuri waliouonesha katika mapokezi
makubwa ya ujumbe wa Zanzibar ulioongozwa na Rais Dk. Shein nchini humo na
kueleza faraja yake kwa hatua hiyo.
Nao viongozi wa vituo
hivyo walimueleza Mama Shein hatua wanazozichukua katika kuhakikisha watoto wanatunzwa
na kuendelezwa kielemu na kijamii pamoja na kumueleza hatua zinazochukuliwa
katika kuwawezesha na kuwaendeleza wanawake nchini humo.
Katika ziara hiyo Mama
Shein amefuatana na Rais Dk. Shein pamoja na viongozi mbali mbali wa Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar, ziara ambayo inatokana na mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Rais
Ismail Guelleh kwa Dk. Shein.
Miongoni mwa viongozi
aliofuatana nao Dk. Shein ni Mama Shein, Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na
Usafiri, Baalozi Ali Karume, Waziri wa Afya Mahmoud Thabik Kombo, Naibu Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk. Susan Alphonce Kolimba.
Wengine ni Mkurugenzi
Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) Salum Khamis
Nassor, Mshauri wa Rais Masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa, Uchumi na
Uwekezaji, Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa pamoja na watendaji wengine wa
Serikali.
Rais Dk. Shein
anatarajiwa kurejea nchini Mei 10 2017.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment