Habari za Punde

Mbunge wa Jimbo la Kiwengwa Akipiga Akabidhi Vyerehani Kwa Wanafunzi Wa Kituo cha Ushoni Kinduni.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhg. Riziki Pemba Juma akizindua Kituo cha Jamii Kinduni { Kinduni Community Center } kwa niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Kinduni Wilaya ya Kaskazini “B”.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Riziki Pembe akikabidhi vyarahani Vitano kwa Uongozi wa Askari Wastaafu wa Wilaya ya Kaskazini B Unguja vilivyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Kiwengwa Mh.Khamis Mtumwa  Ali kwa ajili ya Kituo cha Jamii Kinduni. hafla hiyo imefanyika katika majengo ya Kituo hicho kinduni Wilaya ya Kaskazini B Unguja.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Riziki Pembe akionyesha faraja yake baada ya kutembelea Vyarahani vitakavyotumika katika utoaji wa mafunzo kwenye Kituo cha Jamii Kinduni. 

Wanafunzi wa Darasa la Ushoni katika Kituo cha Jamii Kinduni wakifuatilia ufunguzi rasmi wa Kituo chao uliofanywa na Waziri wa Elimu Zanzibar Mh. Riziki kwa Niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.(Picha na OMPR)

Na. Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema njia pekee ya kukubalika kwa vyuo vinavyoanzishwa Nchini ni umahiri wa ufundishaji unaotokana na Walimu wenye ujuzi na sifa za kufundisha zitakazowashawishi watu kujiunga ili kupata maarifa ya kina.

Alisema umahiri huo utaimarika vizuri zaidi iwapo Uongozi wa Taasisi husika utaamua Chuo chao kukisajili kwenye Mamlaka husika kutegemea fani ya usomeshaji jambo ambalo litakifanya Chuo kilichoanzishwa kutoa vyeti bora vitakavyokubalika katika soko la ajira.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo katika hafla aliyowakilishwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Riziri Pembe Juma wakati akikizindua Rasmi Kituo cha Jamii Kinduni { Kinduni Community Center – KCC } kilichoanzishwa na Askari Wastaafu wa Wilaya ya Kaskazini “B”  kililenga kutoa mafunzo ya ushoni, Komyuta, ufugaji, kilimo pamoja na Ulinzi.

Alisema vyuo vingi vya  miradi ya kujitegemea katika kazi za amali huanzishwa kwa makeke lakini baada ya muda mfupi husambaratika kutokana na ubadhirifu wa mali pamoja na udhaifu wa Uongozi unaowekwa mambo yanayowapa wakati mgumu Walimu kuendelea kufundisha kwa utulivu.

Alitoa wito kwa Uongozi na Wanachama wa Kituo cha Jamii Kindi kutafuta watu wenye Taaluma ya kutosha kukiongoza Kituo hicho ili kuwa mfano bora wa vituo vya ujasiri amali vitakavyokuwa imara hapa  nchini.

Akiwapongeza Wanachama wa Kituo cha Jamii Kinduni kwa uamuzi wao wa kujenga jengo kwa nguvu zao ili kufanya shughuli zao za Maendeleo zitakazowasaidia kuimarisha harakazi zao za kimaisha katika kipindi  hichi cha Kustaafu.

Alisema uamuzi wao huo unaunga mkono sera ya Serikali inayowataka Wananchi kuunda vikundi vya kujiendeleza kimaisha badala ya kusubiri ajira Serikalini ambazo kwa sasa zina upungufu mkubwa sana.

Alieleza kwamba wapo wastaafu wengi ambao hutaka kurudi tena Serikalini kuajiriwa upya lakini Wastaafu hao tayari wameshaona mitaani yapo mambo mengi ya kufanya yanayochangia kupunguza ukali wa Maisha katika wakati wa kustaafu.

“ Kwangu mimi nyinyi ni chuo  cha wastaafu  wengine Nchini. Mmeweka mfano wa kuigwa na sisi tulioko Serikalini tutahakikisha ndoto yenu hii ya kujitegemea  inakamilika na inazaa matunda mliyoyategemea ”. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwashukuru askari wote wastaafu Nchini kwa kulitumikia Taifa katika ngazi ya Ulinzi hadi kufikia kipindi chao cha kustaafu.

Balozi Seif alisema mchango wa askari Wastaafu kwa Taifa hili hautosahauliwa daima kwa kipindi chote tokea Uhuru na Ukombozi ambapo Nchi imeendelea kuwa salama  na wao ndio wachangiaji wakubwa wa kulifikisha hapa lilipo Taifa.

Alisema Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Majeshi yake imejijengea sifa kubwa Duniani kutokana na askari wake kuonyeha ukomavu katika ulinzi wa Kimataifa kwenye Mataifa mbali mbali Duniani.

Makamau wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba Viongozi wa Serikali na Kisiasa wa Mkoa wa Kaskazini Unguja na Nje ya Mkoa huo kuendelea kuusaidia Umoja huo wa Askari Wastaafu ili uweze kufikia malengo uliojipangia wa Maendeleo.

Akisoma Risala Mkurugenzi wa Umoja wa Wastaafu wa Wailaya ya Kaskazini “B”  Ndugu Shabaan Mohamed Iddi alisema Umoja wao umepata mafanikio makubwa tokea kuanzishwa kwake Mwaka 1992 kwa kubuni mipango mbali mbali ya miradi ya Maendeleo.

Nd.Shabaan  alisema hatua hiyo imekuja kufuatia dhamira yao ya kuunga Mkono kuitikia wito wa Serikali ya  Mapinduzi ya Zanzibar  wa kuanzisha Vikundi vya Ujasiri Amali vinavyosaidia kuibua  nafasi za ajira hasa kwa Vijana ili kuabiliana na ukali wa Maisha.

Mkurugenzi  huyo wa Umoja wa Askari Wastaafu wa Wilaya ya Kaskazini “B” alisema licha ya mafanikio hayo zipo changamoto zinazokwaza maendeleo ya haraka ya Umoja huo akizitaja baadhi kuwa ni pamoja na upungufu wa Vyarahani kwa darasa la Ushoni, ukosefu wa sanamni ndani ya Jengo lao jipya wanaloendelea nalo pamoja na huduma za Umeme.

Nd. Shabaan aliiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Taasisi zake za Benki ya Watu wa Zanzibar {PBZ} na Wizara inayosimamia masuala ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kuwapatia Mikopo itakayowawezesh kuendesha Miradi yao waliojipangia kwa ufanisi mkubwa zaidi.

Akimkaribisha Mgeni rasmi kuzindua Kituo cha Jamii Kinduni iliyokwenda sambamba na Uzinduzi wa Jengo lao jipya Mwenyekiti wa Askari Wastaafu wa Wilaya ya Kaskazini “B” Ndugu Omar Bakar Yussuf  amewashukuru Viongozi na Washirika wa Maendeleo walioamua kusaidia Umoja huo.

Nd. Omar Bakari alisema misaada ya Viongozi na washirika hao imewawezesha Askari hao pamoja na Wanafunzi wao wa madarasa ya Ushoni, Kilimo, Kompyuta na Ulinzi kuendesha shughuli zao kwa ufanisi mzuri.

Katika hafla hiyo Mh. Riziri Pembe Juma kwa Niaba ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikabidhi Vyarahani Vitano kwa Uongozi wa Askari hao Wastaafu wa  Wilaya ya Kaskazini “B” kwa ajili ya Darasa la Ushoni la Kituo cha Jamii vilivyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Kiwengwa Mheshimiwa  Khamis Mtumwa Ali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.