Habari za Punde

Mwinyi wa Yanga awataka wachezaji Zanzibar kujituma ili kufanikisha malengo yao

Mchezaji wa kutumainiwa timu ya Yanga , Mwinyi Haji Ngwali


Na: Abubakar Khatib Kisandu, Zanzibar.

Wachezaji wa soka Visiwani Zanzibar wametakiwa kuwa wavumilivu, kuwa na nidhamu, pamoja na kufanya mazoezi kwa nguvu na bidii bila kukata tamaa kama wanataka kufanikiwa malengo yao waliyojiwekea.

Wito huo umetolewa na mlinzi wa kushoto wa Yanga Mwinyi Haji Ngwali “Bagawai” ambaye amewataka wanasoka hao hasa chipukizi kupenda kujifunza na kuzingatia mafunzo ya walimu wao ili wafanikishe dhamira yao.

Mwinyi amesema Zanzibar kuna vipaji vingi sana na yeye anawakubali Wazanzibar wenzake hivyo amewataka kuwa wavumilivu, nidhamu na kujituma zaidi ili wafike wanapopataka.

Amesema ukicheza timu kubwa za Tanzania bara kama Yanga ndipo utajua faida kubwa ya soka huku akiwasisitiza wachezaji wa Zanzibar wapigane wafike Bara na kuona faida ya soka.

“Zanzibar kuna vipaji vingi sana tena mpaka utashangaa, ukipita viwanjani utawaona watoto wanapiga soka hatari, mimi nawaomba wawe wavumilivu, wawe na nidhamu, na wafanye mazoezi kwa nguvu na bidii bila kukata tamaa, michezo inafaida nyingi sana."

 "mfano mimi nimecheza Yanga miaka miwili tu basi nimeona umuhimu wa soka, hakuna kisichowezekana, kwanini mimi nifike Yanga wenzangu wa Zanzibar wasifike, mimi naamini kuna wachezaji wana uwezo zaidi ya sisi tuliofika hapa, lakini kubwa ndo hivyo hakuna kukata tamaa madhali bado upo duniani”. Alisema Mwinyi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.