Habari za Punde

SHERIA ya uharibifu wa mazao kuwamulika na masheha: Jaji Mshibe

Na.Haji Nassor - Pemba.
MWENYEKITI wa Tume ya Kurekebisha sheria Zanzibar Jaji Mshibe Ali Bakari, amesema sheria ijayo ya kudhibiti uharibifu wa mazao, itawabana pia masheha wenye tabia kutoa vibali kwa wafanyabiashara, wanaosafirisha mazao machanga au yalioivishwa kwa moto ikiwemo ndizi.
Alisema kwa sasa sheria hiyo inaendelea kufanyiwa mapitio na tume yake kwa kuwashirikisha wadau mbali mbali, hivyo ndani ya sheria hiyo vimo vifungu vinavyowagusa viongozi hao wa shehia iwapo watatoa vibali kiholela.
Mweyekiti huyo alieleza hayo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na msheha wa mkoa wa kaskazini Pemba pamoja na wadau, wengine wakati akifungua mkutano wa uwasilishaji wa rasimu za awali za sherioa za uharibifu wa mazao, sheria ya usajili wa nyaraka na urithi wa ardhi endelevu mkoani humo.
Alisema kwa sasa wapo wafanyabiashara wamekuwa na mfumo wa kuyaharibu mazao ikiwa ni pamoja na kuyachuma machanga au kuyaivishia kwa moto bila ya kuulizwa, ingawa sheria inayokoja hilo litahesabika kama kosa.
Aidha Mwenyekiti huyo wa tume ya kurekebisha sheria, alisema hata masheha kama wakijaribu kuwapa vibali vya kusafirishia wafanyabiashara wenye tabia hiyo, nao sheria inawamulika hivyo lazima wajitenge na jambo hilo.
Katikati ni Jaji Mshibe Ali Bakar, ndie Mwenyekiti wa Tume hiyo
“Sheria hii ambayo ni kongwe na sasa inafanyiwa marekebisho, haitowagusa tu waharibifu wa mazao kama vile wafanyabiashara waoingiza au kutoa nje ya Zanzibar mazao, hata masheha wakitoa vibali kw amuharibifu nao watawajibika”,alifafanua.
Katika hatua nyengine Mwenyekiti huyo, aliitaja jamii kuendelea kujenga utamaduni wa kusajili nyaraka zao pamoja na ardhi ili ziwe na thamani kisheria.
Mapema Katibu wa Tume hiyo Asma Hamid Jidawi, alisema sheria ya usajili wa ardhi endelevu, unalengo pia la kuondoa migogoro kwenye ardhi za matumizi endelevu kama vile viwanja wa michezo, misikiti na makanisa.
Baadhi ya masheha wa mkoa wa kaskazini Pemba, walisema kama sheria hiyo itatekelezwa ipasavyo baada ya kupitishwa yaweza kuwa ni mwarubani wa mazao kununuliwa yakiwa na uasili wake sokoni.
Sheha wa shehia Micheweni Dawa Juma Mshindo alisema Zanzibar inazosheria nyingi na mzuri, ingawa changamoto huja kwenye utekelezaji wake.
Akiswalisha mswada wa sheria ya usajili wa nyaraka mwanasheria kutoka tume hiyo Mwita Khamis Haji, alisema sheria hiyo imeeleza aina mbili za nyaraka zikiwemo za lazima na nyengine ambazo ni hiari.
“Nyaraka ya nyumba unayoishi au wa kiwanja cha nyumba hizi ni lazima, ingawa zipo nyengine kama vile mikataba ya kijamii hizi hulazimiki, ingawa faidi yake ukizisajili zipo”,alisema.

Tume ya Kurekebisha sheria Zanzibar chini ya Mwenyekiti wake jaji Mshibe Ali Bakar imeshazifanyia marekebisho sheria 17 ikiwemo sheria ya ushahidi, sheria ya wanyama, vileo na sheria ya usafirishaji baharini, na kwa sasa wanaendelea na sheria za uharibifu wa mazao, nyaraka na ardhi endelevu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.