Habari za Punde

Jiji la Potsdam la Ujerumani latia saini hati ya makubaliano ya mahusiano memo na Shehia ya Kikwajuni

 Meya wa Jiji la Potsdam Nchini Ujerumani Jann Jakobs akiukagua Mti alioupanda Mwaka 2014 alipotembelea Zanzibar mwaka huo.
 Meya wa Jiji la Potsdam Nchini Ujerumani Jann Jakobs na Ujumbe wake wakipita katika Maeneo ya Kikwajuni kwa Mjerumaini kabla ya hafla ya kusaini hati ya Makubaliano ya Mradi wa Mahusiano mema baina ya Jiji la Potsdam na Kikwajuni Mjini Zanzibar.
 Baadhi ya wananchi wa Shehiya ya Kikwajuni Juu wakisalimiana na Meya wa Jiji la Potsdam Ujerumani mara baada ya kutembelea maeneo ya Kikwajuni kwa Mjerumani. 
 Sheha wa Shehiya ya Kikwajuni juu Mzee Juma Saadat Haji na  Kati Anton Mkurugenzi wa Nyumba za kulelea Watoto wa Drewtz wakisaini hati ya Makubaliano ya Mradi wa Mahusiano mema Baina ya Mji wa Drewits na Kikwajuni Mjini Zanzibar kulia yao ni Meya wa Jiji la Potsdam Ujerumani 
Picha ya Pamoja ya Wananchi wa Kikwajuni na Ujumbe kutoka Jiji la Potsdam mara baada ya kusaini hati ya Makubaliano ya Mradi wa Mahusiano mema Baina ya Mji wa Drewits na Kikwajuni Mjini Zanzibar 

Picha na Makame Mshenga.



Na Faki Mjaka-Maelezo 

Mji wa Drewits uliopo Jiji la Potsdam nchini Ujerumani kwa kushirikiana na Shehia ya Kikwajuni Juu wamesaini hati ya makubaliano ya Mradi wa mahusiano mema baina ya Jiji la Potsdam na Kikwajuni Mjini Zanzibar.

Miongoni mwa Vipengele vya makubaliano hayo ni kuijenga miundombinu ya Majumba ya Mjerumani Kikwajuni ili kuhakikisha muonekano wake inafanana na Mji wa Drewits wa Potsdam Ujerumani.

Akizungumza katika Hafla hiyo Meya wa Jiji la Potsdam Jann Jakobs amesema amefurahi kuona mambo mbalimbali yameanza kutekelezwa kabla ya utiaji saini jambo ambalo linaonesha matumaini mazuri.

Miongoni mwa mambo ambayo yameanza kutekelezwa ni pamoja na upandaji Miti inayozunguka Uwanja wa Mnazi mmoja na Mtaro wa kutirishia Maji machafu katika eneo hilo.
Meya huyo amesema atahakikisha mradi huo unafikia malengo yake kwa ajili ya maslahi mapana ya Watu wa Ujerumani na Zanzibar kwa ujumla.

Kwa upande wake Mwandishi wa mradi huo Idrissa Haji Ali amesema ili kuufanikisha mradi huo kutakuwa na ujenzi wa mambo mbali mbali ikiwemo Maduka, Viwanja vya kuchezea, Taa za Barabarani na barabara ili uendanane na Mji wa Drewits.

Amesema yeye kwa kushirkiana na Wenzake walienda Ujerumani kutembelea na kujifunza mambo mbali mbali hasa ya kimiundombinu na mazingira ili iwe rahisi ya kutekeleza mradi huo.

Kwa upande wake Sheha wa Shehia ya Kikwajuni Juu, Juma Saadat Haji amemshukuru Meya wa Mji huo pamoja na ugeni wake kwa namna walivyojitolea kuufanikisha mradi huo wenye maslahi makubwa katika shehia yake.

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutawawezesha wananchi wa Shehia yake kuishi maisha mazuri ambapo huduma za kijamii zitapatikana kwa kiwango cha hali ya juu.

Utiaji Saini ulifanywa na Sheha wa Kikwajuni Juu, Juma Saadati kwa niaba ya Watu wa Kiwajuni ambapo kwa upande wa Mji wa Drewits uliwakilishwa na Mkurugenzi wa Nyumba za Watoto wa Mji huo Kati Antoni.

Katika ziara hiyo Meya wa Mji wa Potsdam aliambatana na wataalamu tofauti wakiwemo wa Majenzi, Mazingira,Familia na Wanahabari ili kufanikisha ziara yake.

Meya huo ataendelea na ziara yake katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar na kutiliana saini na Mwenyeji wake Meya wa Mji wa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.