STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 31.07.2017
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza haja ya kuzifahamu vyena na kuzifanyia
kazi sheria zilizounda Bodi za Wakurugenzi za Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na
Usafirishaji ili Bodi hizo ziweze kufanya kazi kwa ufanisi sambamba na
kuimarisha mashirikiano kati ya Bodi na Wizara.
Dk. Shein aliyasema hayo
Ikulu mjini Zanzibar kwa nyakati tofauti wakati alipokutana na uongozi wa
Wizara hiyo pamoja na Bodi ya
Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini na Uongozi wa Mamlaka ya Usafiri
Baharini, Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Bandari na Uongozi wa Shirika la
Bandari pamoja na Bodi ya Wakurugenzi ya
Shirika la Meli na Uongozi wa Shirika hilo.
Katika maelezo yake, Dk.
Shein alieleza kuwa mafanikio makubwa yatapatikana katika kufikia malengo
yaliokusudiwa iwapo sheria zilizopo zinazoziongoza Bodi hizo zitafanyiwa kazi
vizuri kwa lengo la kutekeleza mambo muhimu yaliokusudiwa.
Aidha, Dk. Shein
alisisitiza haja kwa uongozi wa Bodi hizo kuzipa kipaumbele Sheria tatu muhimu
ikiwemo Sheria namba 1 ya mwaka 1997, Sheria namba 2 ya mwaka 2001 na Sheria
namba 4 ya mwaka 2002, ili ziwe Dira katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila
siku.
Dk. Shein alisisitiza
haja ya kushirikiana na kupendana kwa wafanyakazi wa Bodi hizo, Mamlaka na
Mashirika, pamoja na viongozi wa Wizara hiyo ili kutimiza azma ya kuleta
maendeleo na kukuza uchumi wa nchi.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alieleza umuhimu kwa Bodi hizo za Wakurugenzi wa kutoa taarifa kwa
Serikali kupitia Wizara hiyo ili mipango inayopangwa iweze kuleta tija huku
akitumia fursa hiyo kupongeza mafanikio makubwa yaliopatikana katika Mamlaka ya
Usafiri Baharini, Shirika la Bandari pamoja na Shrika la Meli.
Aliongeza kuwa kazi za
Bodi sio kulumbuna ama kupambana na Wizara bali ni kushirikiana na Wizara
katika kuhakikisha mipango ya maendeleo iliyopangwa inakwenda vyema kwa lengo
la kuleta manufaa kwa taifa na jamii kwa ujumla.
Aidha, alieleza kuwa ni
lazima ifahamike kuwa Bodi hizo za Wakurugenzi, Mamlaka na Mashirika yaliomo
katika Wizara hiyo yote hayo ni ya Serikali, hivyo ni vyema yakafuata taratibu,
kanuni na sheria ziliopo ambazo zimewekwa na Serikali na kuepuka kujipangia
mambo wenyewe.
Dk. Shein Shein alitumia
fursa hiyo kutoa pongezi kwa uongozi wa Bodi hizo, Mashirika na Mamlaka
ya Usafirishaji na uongozi wake pamoja na uongozi wa Wizara hiyo kwa
mafanikio makubwa yaliopatikana sambamba na mabadiliko makubwa yaliyofanywa
katika kuhakikisha yanasaidia katika kuimarisha uchumi wa nchi.
Nae Makamo wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, alipongeza juhudi zinazochukuliwa na Bodi
hizo, Mamlaka pamoja na Mashirika hayo yaliyomo katika Wizara hiyo na
kusisitiza haja ya kuweka mikakati maalum ya kutambua mizigo inayopitishwa
katika Bandari ya Zanzibar ili kuepuka bandari hiyo kufanywa njia ya kupitishwa
bidhaa zisizofaa.
Waziri wa Wizara hiyo
Balozi Ali Karume alitumia fursa hiyo kueleza mashirikiano mazuri yaliopo kati
ya uongozi wa Wizara, Bodi na wafanyakazi wake huku akieleza,
Katibu Mkuu Kiongozi na
Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alieleza kuwa lengo la
kuundwa kwa Mamlaka na Mashirika ya Serikali ni kuchangia mapato katika Mfuko
Mkuu wa Serikali hivyo ni vyema juhudi zikachukuliwa katika kuhakikisha hilo
linafanikiwa.
Mwanasheria Mkuu wa
Zanzibar, Said Hassan alisisitiza haja ya Uongozi wa Bodi hizo za Wakurugenzi
kuendelea kushirikiana vyema na Ofisi yake huku akieleza umuhimu wa ukaguzi kwa
meli za ndani.
Aliongeza kuwa mbali ya
kujua sheria za zilizopelekea kuundwa kwa Bodi hizo ni vyema wajumbe na
viongozi husika wakazitambua sheria nyengine ili ziweze kuwarahisishia kazi zao
ikiwemo Sheria namba 2 ya mwaka 2002.
Katibu Mkuu wa Wizara
hiyo Mustafa Aboud Jumbe alitumia fursa hiyo kutoa historia ya Uanzishwaji wa
Mamlaka pamoja na Mashirika na hatimae Bodi hizo
Nao Wakurugenzi Wakuu wa
Wizara hiyo walieleza mafanikio yaliopatikana sambamba na mashirikiano mazuri
yaliopo kati yao na Bodi za Wizara hiyo hatua ambayo imepelekea kuweza kupiga
hatua kubwa ya maendeleo ya kiuchumi katika sekta ya huduma ya usafiri na
usafirishaji.
Wenyeviti wa Bodi hizo
kwa nyakati tofauti walieleza mafanikio makubwa yaliopatikana sambamba na
changamoto zilizopo ambazo walieleza kuwa zimo katika hatua za kupatiwa
ufumbuzi huku wakiahidi kuendeleza mashirikiano yaliopo kati yao na uongozi wa
Wizara.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment