STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 03.07.2017
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza matumaini yake makubwa kwa kuundwa
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) na kuanza kazi
zake vyema tena kwa muda mfupi na kueleza kuwa kazi za Mamlaka hiyo zitaenda
vizuri iwapo wataenda sambamba na sheria ya Mamlaka hiyo.
Dk. Shein aliyasema hayo leo
Ikulu mjini Zanzbar wakati alipokutana na uongozi wa Wizara ya Ardhi, Maji,
Nishati na Mazingira pamoja na Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa
Huduma ya Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) na Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya
Maji Zanzibar (ZAWA).
Katika maelezo yake, Dk.
Shein alisema kuwa Mamlaka ya ZURA imeweza kuleta matumaini makubwa katika
kutatua changamoto kadhaa zilizokuwepo hapo siku za nyuma katika suala zima la
uhaba na upandishaji wa bei ya mafuta kiholela uliokuwa ukitokea na kuleta
usumbufu kwa wananchi.
Hivyo, aliitaka ZURA
kuendelea na kasi na ari waliyonayo ya utendaji wa kazi na kusisitiza haja ya
kuiangakia kwa umakini sheria ya Mamlaka hiyo kwani ina mambo mengi ya msingi
yanayoigusa Bodi, Wizara na Jamii.
Dk. Shein alieleza kuwa
kwa upande wa wananchi wanapaswa kuijua na kuitambua ZURA na kazi zake ili
kuweza kupeleka malalamiko yao hasa katika suala zima la bei ya mafuta.
Nae Makamo wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, alitoa pongezi kwa ZURA na Bodi yake na
kueleza haja ya kuangalia ujenzi wa vituo vya kuuzia mafuta kwa kufuata sheria
na taratibu za ZURA.
Waziri wa Wizara hiyo
Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Salama Aboud Talib, alipongeza mashirikiano
yalipo kati ya Wizara na Bodi hiyo huku akieleza changamoto iliyopo katika
suala zima la ujenzi wa vituo vya kuuzia mafuta ambao ujenzi wake umekuwa
haufuati taratibu.
Katibu Mkuu Kiongozi na
Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alieleza haja ya
kutafutwa sehemu mbadala ya eneo la kuhifadhia mafuta liliopo Mtoni ambalo kwa
hivi sasa liko karibu sana na maakazi ya wananchi.
Aidha, alisema kuwa
tayari eneo la Mtoni miundombinu yake imechakaa ambapo pia, meli za mafuta hivi
sasa haziwezi tena kufika katika eneo hilo sambamba na kueleza umuhimu wa kuwepo
utaratibu wa kuuza maji kwa magari ambayo hupeleka mahotelini kwani hiyo ni rasilimali
ya Serikali.
Pia, Dk. Abdulhamid
aliitaka ZURA kushirikiana na vyombo vya ulinzi katika kupambana na wauza mafuta
ya magendo.
Nao uongozi wa ZURA
ulieleza kuwa juhudi zimekuwa zikichukuliwa katika kulitafutia ufumbuzi suala
zima la miundombinu ya vituo vya mafuta ambavyo vingi vimekuwa na vifaa
vichakavu.
Wajumbe wa Bodi ya ZURA
walimueleza Rais kuwa tokea kuanza kwa kazi kwa ZURA suala la kuwepo kwa uhaba
wa mafuta mara kwa mara limeondoka sambamba na lile la wafanyabiashara kupandisha
bei ya mafuta kiholela.
Walieleza kuwa kwa hivi
sasa wameweza kujipanga vizuri na kupelekea kuongeza mapato na kueleza mpango
wao wa kutekeleza miradi mikubwa ukiweo wa ujenzi wa ofisi zitakazojumuisha ofisi
za Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira pamoja na ujenzi wa bandari kwa
ajili ya shughuli za mafuta na gesi huko Mangapwani.
Aidha, Mamlaka ya ZURA
imeleeza mipango yake ya kutaka kubadilisha mfumo wa uletaji mafuta hapa nchini
ambapo mafuta yataletwa moja kwa moja hapa Zanzibar hali ambayo itasaidia
kushuka kwa bei ya mafuta na kuweza kuwasaidia wananchi.
Pia, uongozi huo wa Mamlaka
ya ZURA ulieleza kuwa tayari kumejitokeza Makampuni kadhaa yanayotaka
kushirikiana na Mamlaka hiyo katika ujenzi wa Bandari huko Mangwapwani katika
eneo maalum lililotengwa kwa ajili ya bandari pamoja na eneo kwa ajili ya
mafuta na gesi.
Sambamba na hayo, ZURA
ilieleza azma yake ya kulishughulikia suala zima la maji na umeme ambalo limo
katika majukumu yao kisheria ili wananchi wapate kuzitumia vyema huduma hizo
huku wakieleza mashirikiano yao yaliopo kati yao na Mamlaka ya Udhibiti wa
Nishati na Maji Tanzania (EWURA).
Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana na uongozi wa
Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), uongozi wa Wizara husika pamoja na Bodi ya
Mamlaka hiyo na kutaka kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizopo hasa katika
suala zima la upatikanaji wa maji.
Dk. Shen pia, alieleza
namna Serikali inavyoangalia haja ya kuyahifadhi maji kwani maji yamekuwa yakipotea
ovyo hasa mara baada ya kumalizika kunyesha kwa mvua huku akiitaka ZAWA, Bodi,
Uongozi wa Wizara kuijua Sheria na kuifanyia kazi.
Nae Makamo wa Pili wa
Rais Balozi Seif Ali Idd, alieleza umuhimu wa kutafuta ufumbuzi wa malalamiko
ya upatikanaji wa maji katika maeneo kadhaa ya wananchi hapa nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa ZAWA
Mustafa Ali Garu alieleza jitihada zinazochukuliwa na ZAWA ikiwa ni pamoja na
kuendeleza miradi mikubwa ukiwemo Mradi chini ya ufadhili wa Serikali ya China,
Mradi wa ADB, Serikali ya India ambao umo katika matayarisho, pamoja na Mradi kutoka
Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la misaada la JICA.
Alisema kuwa visima
katika mradi wa ufadhili wa China unaenda vizuri katika maeneo mbali mbali kama
vile Donge, Chaani, Pangeni na maeneo mengine ambayo tayari miudombinu ya maji
imeshaanza kuwekwa.
ZAWA ilieleza kuwa mapato
yameongezeka kwa kiasi kikubwa lakini hata hivyo bado wanahitaji kujiimarisha
katika kuongeza mapato hayo na kueleza kuwa hilo linawezekana iwapo jitihada
zaidi zitafanyika.
Alieleza kuwa hali ya
maji yaliopo Zanzibar ni ya kutosha na kueleza jinsi ilivyohuwika hasa katika kipindi
kilichopita cha mvua za masika ambapo maji yameweza kuongezeka kwa kiasi
kikubwa.
Dk. Garu alieleza
changamoto zilizopo ambazo ni pamoja na upotevu wa maji huku akieleza kuwa hali
ya miundombinu chakavu nayo hipo lakini jitihada zimekuwa zikifanyika katika
kuodoa tatizo hilo kupitia miradi husika.
Nao Wajumbe wa Bodi ya
ZAWA walieleza ponhezi zao kwa Rais kwa kuwepo kwa mradi wa Ras-el kheiman ambao
kukamilika kwake kutatatua changamoto kubwa ya maji kwa upande wa Unguja na
Pemba.
Walieleza changamoto
zilizokuwepo ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa miundombinu chakavu na kuongeza kuwa
Mita za kawaida hazijaweza kutosheleza ambapo bado kuna wateja wengi
wanaohitaji huduma hiyo kuipata.
Uongozi wa Wizara kwa
upande wake ulieleza juhudi, malengo na mikakati liyoiweka katika kuhakikisha
changamoto ya sekta ya maji inapatiwa ufumbuzi huku ikiitaka jamii kuitumia
vyema rasilimali hiyo iliyopo kwa kuihifadhi vyema pamoja na vianzio vyake.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment