Habari za Punde

Serikali kuwajengea uwezo wakulima wa mwani, kutafuta masoko mapya na kuwapatia fursa za mikopo

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akipokea maandamano ya Wazalishaji wa zao la Mwani katika sherehe za maadhimisho ya Siku ya Mwani Duniani zilizofanyika Uwanja wa Malindi Mjini Zanzibar.

 Akina Mama wazalishaji wa zao la Mwani wakionyesha bidhaa zao kwenye maandamano ya Siku ya Mwani Duniani zilizofanyika Malindi ambapo Mgeni Rasmi ni Balozi Seif Ali Iddi.

 Bibi Maryam Pandu Kweleza wa Kikundi cha ushirika cha Kazi Moto Bwejuu akimfahamisha Balozi Seif  jinsi ya ukulima wa zao la mwani unavyoendeshwa kwenye maonyesha ya bidhaa zinazozalishwa na zao hilo hapo Malindi.
 Balozi Seif na Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Mh. Hamad Rashid Mohamed wakiangalia Mwani uliopea tayari kwa ajili ya kutengenezwa mali ghafi ya bidhaa mbali mbali.
Nyuma ya Mh. Hamad Rashid ni Mwenyeketi na Muwezeshaji wa Kongano la Ubunifu wa Mwani Dr. Flower Msuya akishuhudia kitendo hicho huku Bibi Marya Kweleza akiendelea kutoa maelezo.

 Balozi Seif akiridhika na bidhaa  safi za vyakula na Juisi zilizotengenezwa na wazalishaji wa mwani kutoka vikundi mbali vya akina mama wakati akikagua maonyesho ya bidhaa hizo.
Balozi Seif akiangalia sabuni ya maji iliyotengenezwa na Kikundi cha  akina Mama wa Kijiji cha Makangale Micheweni Pemba ambayo imetumia Mali ghafi  ya Mwani.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Serikali inaendelea kuwaunga Mkono Wananchi kwa kuwajengea uwezo ikiwemo fursa za mikopo pamoja na kuongeza kasi katika kutafuta masoko  mapya ili kuona Wakulima  wa kilimo cha Mwani wanaongeza kiwango cha uzalishaji na uwezo wa ubunifu.

Hatua hiyo italeta tija zaidi kwa Wakulima  wa Kilimo hicho kilichoanza kulimwa Nchini takriban kwa karibu  Miaka 30 sasa na kushirikisha vijiji zaidi ya 50 ili kuweza kujikwamua kiuchumi na kuongeza fursa kwa Taifa katika kukuza mapato yake .

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati  wa kilele cha maadhimisho ya siku ya Mwani ya Kongano Bunifu la Mwani Zanzibar yaliyofanyika katika viwanja vya Michezo vya Malindi Mjini Zanzibar.

Balozi Seif  alisema mwenendo wa mapato kwa Wananchi unaonekana kuongezeka siku hadi siku na kuonyesha  haja kwa Serikali kuendelea kutilia mkazo uzalishaji wa zao Mwani kwa vile ni sekta ya tatu kwa kuleta tija kwa Taifa ikitanguliwa na Utalii na Karafuu na ni zao la pili kwa kusafirishwa nje ya Nchi likitanguliwa na Karafuu.

Alisema Sekta hiyo tayari imeshatoa ajira za kudumu kwa zaidi ya Wakulima 23,000 na kuna ajira nyingi ambazo hutokea kipindi cha msimu wa kupanda, kuvuna na kusarifu Mwani.

Alieleza kwamba faida imeanza kuonekana kupitia zao la Mwani Kiuchumi ambapo Wananchi kutoka Vijiji mbali mbali vya Zanzibar  na hata baadhi ya Wilaya za Tanzania Bara walijishughulisha na zao hilo ambapo asilimia kubwa ya Wakulima wake ni Akinamama.

Balozi Seif alifahamisha  kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inazungumza na wadau mbali mbali wa ndani na nje ya Nchi ili waanzishe Viwanda vodogo vidogo vya kuweza kulifanyia kazi zao hilo hapa nchini pamoja  na kuimarisha soko na bei yake.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali inafahamisha kuwa pamoja na faida inayopatikana katika uzalishaji wa zao la Mwani lakini bado Sekta hiyo imekumbwa na changamoto kubwa ikiwemo kutofahamika kwa bei yake pamoja na utaratibu wa leseni kwa Wafanyabiashara wa Mwani.

Alisema katika kutatua changamoto za Masoko, Kongano la Mwani kwa kushirikiana na Shirika la Milele Zanzibar Foundation waliamua kuweka Siku ya Mwani ili kutoa nafasi kwa Jamii kujua matumizi halisi ya zao hilo na kulifanya litumike zaidi Nchini na kupunguza utegemezi mkubwa wa soko la nje.

Balozi Seif alitoa rai ya kuchukuliwa hatua za makusudi katika kuvitumia vyombo vya Habari Nchini na Nje ya Nchi kuutangaza Mwani kwa upana zaidi ili Wananchi  wapate mwamko juu ya zao la Mwani na sio kusubiri Makongano kwa ajili ya kujitangaza.

Amempongeza Mwenyekiti na Mwezeshaji wa Kongano la Mwani Dr. Flower  Msuya kwa uwamuzi wake wa kushirikiana na Wizara ya Kilimo Zanzibar pamoja na Shirika la Milele Foundation Zanzibar kuwa bega kwa bega na Wakulima katika kuzitambua changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaahidi wadau wa zao la Mwani kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesikia kilio chao kinachotokana na kodi kubwa la Bidhaa hizo wanazotozwa.

Alisema juhudi zitachukuliwa katika kuona kodi hizo zinapunguzwa au kuondoshwa kabisa ili kuwapa fursa ya kuweza kuliendeleza kwa vile limeshonyesha muelekeo wa kuongeza mapato yao.

Mapema Mwenyekiti na Mwezeshaji wa Kongano la Ubunifu wa Mwani Dr. Flower Msuya alisema bidhaa za mwani hivi sasa zimefikia 50  ikilinganishwa na bidhaa moja tuu iliyokuwa ikizalishwa na Kikundi cha Tusife Moyo cha Kijiji cha Kidoti mnamo Mwaka 2006.

Dr. Flower alisema mipango ya baadae ya ya Taasisi hiyo ni kuendelea kutengeneza bidhaa zinazotokana  na zao la Mwani baada ya kufanyiwa utafiti uliothibitisha kwamba bidhaa hiyo ina matumizi mengi mchanganyiko ikiwemo chakula.

Akitoa salamu za Taasisi ya Milele Zanzibar Foundation iliyoratibu hafla hiyo ya siku ya Mwani Duniani, Mwakilishi wa Milele Zanzibar bibi  Khadija Sharifu alisema Taasisi yake inakusudia kuwaleta Wataalamu wa kigeni kwa ajili ya kuwapatia mafunzo wazalishaji wa mwani.

Bibi Khadija alisema Wataalamu wa Milele wamegundua kwamba Sekta ya Mwani  inaweza kuwakomboa wananchi walio wengi kwa kutoa ajira kubwa ambapo kwa sasa tayari imetoa ajira ya watu zaidi ya 23,000 tokea kuanza kwa sekta hii nchini Tanzania.

Akimkaribisha mgeni rasmi kwenye siku hiyo ya Mwani Duniani Waziri wa Kilimo, Mali asili, Mifugo na Uvuvi Zanzibar Mheshimwa Hamad Rasid Mohamed alisema jamii inapaswa kubadilika katika utaratibu wao wa nlishe na kupoenda kutumia mazao ya Mwani kwa lengo la kujenga afya zao.

Waziri Rashid alisema zao la Mwani kwa utafiti wa kitalaamu linaonyesha kukinga maradhi mbali mbali ikiwemo ukanda wa jeshi,  Mshtuko wa Moyo pamoja na maradhi yanayodhoofisha upungufu wa Damu kutokana na ulaji ovyo wa vyakula vya makopo.

Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alipokea maandamano ya wazalishaji wa zao la mwani kutoka wilaya mbali mbali za Unguja na Pemba na baadaye kukagua bidhaa zao wanazozalisha kutokana na  mali ghafi hiyo ya Mwani.

Wakulima hao walimueleza Balozi Changamoto wanazopambana nazo katika harakati zao za kulima zao hilo kukausha hadi kukamilika kwa ajili ya soko ambapo walisema  kodi ya bidhaa iwanayotozwa kuhusiana na bidhaa ya zao hilo imekuwa ikiwakatisha tamaa.

Walieleza pia upo upungufu wa ukosefu wa mashine ya kukaushia mwani ambayo kwa sasa inapatikana  Kidoti Mkoa wa Kaskazini Unguja pamoja na bei ndogo ya zao hiyo isiyolingana na gharama za uzalishaji wake.

Kongamano Bunifu la Mwani Zanzibar lilianzishwa Mwaka 2006 kwa kupitia Mpango wa Makongano Bunifu Afrika unaosimamiwa na Tume ya Sayansi Teknolojia Tanzania {COSTECH} ili kuunga mkono juhudi zinazochukiwa na Serikali.

Mpango huo wa Makongano Bunifu ulianza na Makongano Manane kwa Tanzania Bara na Kongano Moja tu la Mwani  kwa Zanzibar  Tokea kubuniwa kwake ambapo kwa sasa tayari yapo Makongano 70 kwa Bara na Manane kwa Zanzibar.

Zao Mwani limekuwa likitumika kwa kutengeneza Sabuni, Mafuta ya kujipaka, shampuu na vyakula vya kama Juisi keki, jam, kachumbari na kupikwa kama mboga sambamba na utengenezaji wa dawa za Binaaadamu, vipodozi na chakula cha mifugo.

Ujumbe wa Mwaka huu wa Siku ya Mwani Duniani unaeleza Mwani kwa afya, Mwani kwa kipato na Mwani kwa uwezeshaji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.