Habari za Punde

Serikali yazungumzia juu ya kuondolewa CAF, yawaomba wazanzibari kuwa watulivu

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utalii Utamaduni na Michezo Zanzibar Omar Hassan Omar “King” alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)


Na: Abubakar Khatib “Kisandu”, Zanzibar.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Utalii Utamaduni na Michezo Zanzibar Omar Hassan Omar “King” amewataka Wazanzibar kuwa wastahamilivu na kuwa na subira katika kipindi hichi kigumu baada ya Zanzibar kuondolewa uanachama wao wa 55 wa kudumu wa Shirikisho la Soka Barani Afrika “CAF”.

King amesema wanachosubiri sasa ni ujio wa viongozi wa ZFA ambao waliokuwepo mjini Rabat, Morocco kwenye kikao cha Kamati utendaji ya CAF, viongozi ambao walikuwemo kwenye kikao hicho ambacho kuliamua mambo kadhaa likiwemo hilo la Zanzibar kufutiwa uanachama wake, na baada ya ripoti hiyo ya ZFA wao Serikali watatoa taarifa rasmi.

Viongozi wa ZFA walikuwepo katika Mkutano huo ni Rais wa ZFA Ravia Idarous Faina, Katibu Mkuu wa ZFA Mohd Ali Hilali “Tedy” pamoja na kocha mkuu wa timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) Hemed Suleiman “Morocco” ambao wanatarajiwa kuwasili Visiwani Zanzibar kesho Jumatatu ya July 24, 2017 kwenye uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume kuanzia majira ya saa 2 za usiku.

“Kama mulivyosikia tumeondolewa uanachama na CAF, lakini tunachokisubiri kwasasa ni kuweza kupata taarifa rasmi kutoka kwa ZFA na kupata barua ambayo itawasilishwa ZFA baadae barua ile kuwasilishwa Serikalini na pale ndipo tutaweza kujua ni ipi sababu gani ilipopelekea kutolewa, cha msingi jambo hili limetusikitisha sana Wazanzibar lakini mimi naomba tuwe watulivu kisha tuwe na subira katika kipindi hichi, baada ya hapo tutatoa taarifa rasmi kutoka Serikalini”.Alisema King.

Juzi Rais wa CAF, Ahmad Ahman amesema Zanzibar ilipewa nafasi hiyo kimakosa na si sahihi kwa nchi moja kuwa na wanachama wawili wa shirikisho hilo.

Zanzibar ilipewa uanachama wakati wa utawala wa Issa Hayatou ambaye alikuwa akiungwa mkono na TFF chini ya Jamal Malinzi, hata hivyo Hayatou aliangushwa na Ahmad Ahmad ambaye aliibuka mshindi katika uchaguzi wa CAF ambapo uanachama huo kwa Zanzibar ulidumu kwa siku 128 kuanzia Alhamis ya Machi 16, 2017 hadi juzi Ijumaa ya July 21, 2017.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.