STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 22.07.2017
WANANCHI
katika Mkoa wa Kusini Pemba wameelezea kufurahishwa kwao kutokana na
utekelezwaji wa ahadi mbali mbali zilizotolewa na Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein na kutoa wito kwa
viongozi wengine wa kisiasa kuiga mfano huo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mahojiano
maalum baada ya kukabidhiwa mashua mbili za kuvushia wananchi kutoka kwa Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein,
wananchi wa Kisiwa Panza na Chokocho katika Wilaya ya Mkoani, wameeleza kuwa
wamekuwa wakishuhudia mabadiliko makubwa ya kimaendeleo katika Wilaya yao kwenye
sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii ndani ya kipindi cha miaka sita
iliyopita.
Wamesema sehemu kubwa ya maendeleo hayo yanatokana
na utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015 – 2020, ahadi zilizotolewa na Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi wakati wa kampeni za uchaguzi
wa mwaka 2010-2015 na 2015-2020 na ahadi alizozitoa wakati wa ziara zake katika
nyakati tofauti Wilayani humo.
Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Hemed Suleiman Hemed
amesema tatizo la usafiri wa baharini kwa wananchi wa vijiji vya Kisiwa Panza
na Chokocho ni la muda mrefu lakini limezidi kuwa kubwa mara baada ya uchaguzi
mkuu wa mwaka 2015, ambapo wanaomiliki vyombo vya usafiri waliamua kutoa huduma
kwa ubaguzi kwa kuzingatia misingi ya kisiasa.
Faki Mohamed Khamis na Khamis Juma Othman wamesema
kuwa kwa miaka mingi viswa hivyo havijawahi kushuhudia hatua kubwa za maendeleo
ya muda katika kipindi kifupi kama ilivyo mara hii ambapo huduma za maji safi
na salama, umeme na elimu zimeimarika zaidi.
Kauli kama hiyo pia, imetolewa na Bi Mwamize Vuai
Haji na Chum Abdalla ambao wamesema wanajivunia huduma hizo, huduma ya usafiri
wa baharini ambayo imetolewa hivi karibuni na Dk. Shein na ujenzi wa ukuta
unaozuia maji ya chumvi yanayoingia kwenye makaazi ya watu kutokana na
mabadiliko ya tabia nchi.
Uamuzi wa kununua mashua hizo zilizogharimu
shilingi milioni 27, ulichukuliwa na Rais Dk. Shein kufuatia malalamiko ya
wananchi wa Kisiwa Panza na Chokocho, ambao walimuelezea kilio chao kutokana na
usumbufu mkubwa wanaoupata wa usafiri hasa baada ya huduma hiyo kuanza kutolewa
kwa njia za kibaguzi.
Akikabidhi mashua hizo kwa niaba ya Rais Dk. Shein,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum
Mheshimiwa Haji Omar Kheir amesema mashua hizo ambazo zitakuwa chini ya
usimamizi wa Kikosi maalum cha kuzuia magendo zitatoa huduma chini ya misingi
ya usawa bila ya kujali rangi, dini wala chama cha siasa kama ilivyotokezea
hapo siku za nyuma kwa kubaguliwa kwa wananchi wanaotoka chama fulani.
Akizungumza kwenye sherehe za kukabidhi mashua
hizo, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mwanajuma Majid amesema kilio cha wananchi
wanaoishi kisiwa Panza na Chokocho kitaondoka baada ya mashua hizo kuanza kazi
rasmi hivi karibuni.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment