Habari za Punde

WHO Yaipongeza Serikali ya SMZ Kwa Hatua ya Kukabiliana na Maradhi ya Kuambukiza Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akisalimiana na Mwakilishi wa Shirika la Afya Ulimwenguni  { WHO } Nchini Tanzania Dr. Mathew Kamwa  aliyepo kati kati alipofika Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar kwa mazungumzo.Wa kwanza Kushoro ni Mwakilisi wa Shirika la Afya Duniani { World Heathy Organization Kanda ya Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kulia akizungmza na Mwakilisi wa Shirika la Afya Duniani { World Heathy Organization } Tanzania Dr. Mathew Kamwa aliyekaa  kati kati .
Balozi Seif kati kati akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa Shirika la Afya Ulimwenguni pamoja na Uongozi wa ngazi ya juu wa Wizara ya Afya Zanzibar.
Mwenyekiti wa Kampuni ya Complant ya Nchini Jamuhuri ya Watu wa China Bibi Liu Yan wa Pili kutoka Kulia akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.
Bibi Liu Yan kati kati akimpatia zawadi ya Majani ya Chai Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya kumaliza mazungumzo yao.
Balozi Seif Kat kati akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Kampuni ya Kimataifa ya Complant ya Nchini China ukiongozwa na Mwenyekjiti wake Bibi Liu Yan.(Picha na – OMPR – ZNZ.)

Na. Othman Khamis OMPR.
Shirika la Afya Ulimwenguni {WHO} limeridhika na hatua kubwa na madhubuti inayoendelea kuchukuliwa na Zanzibar katika  mapambano yake dhili ya kukabiliana na  maradhi ya kuambukiza ya Kipindupindu.

Jitihada hizo zimelifanya shirika hilo kuhamasika na kujaribu kutafuta mbinu mbadala za kuendelea  kuiunga mkono  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kujikwamua na janga hilo linalooneka kuwa na kawaida hasa unapoingiza msimu wa mvua za masika.

Kauli hiyo imetolewa na Mwakilishi wa Shirika la Afya Ulimwenguni Nchini Tanzania Dr. Mathew Kamwa  alipokuwa akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar baada ya kupata fursa ya kutembelea maeneo mbali mbali na kuzungumza na watendaji wa Taasisi za Umma.

Ziara hiyo ya Dr. Mathew pia  ilihusisha kukagua huduma za afya  wanazopatiwa wagonjwa wa Maradhi ya Kipinduindu katika kituo cha Afya kilichotengwa maalum cha Chumbuni Mjini Zanzibar.

Mwakilishi huyo wa Shirika la Afya Ulimwenguni alisema Taasisi hiyo ya Kimataifa iliyoundwa kwa lengo la kusimamia ustawi wa Afya za Walimwengu itajenga ukaribu zaidi na Wizara ya Afya Zanzibar katika kuona yale mahitaji muhimu na ya lazima yanayolazimika kupatiwa Wananchi hasa Dawa na Vifaa yanapatikana kwa wakati.

Dr. Mathew Kamwa aliisisitiza Jamii ya Watanzania kupenda kutunza mazingira katika hatua za awali za kuwepuka kusambaa kwa maradhi ya kuambukiza ambayo ni hatari kwa binaadamu kutokana na athari yake kuibuka ghafla kabla ya kuchukuliwa hatua za tiba.

Akitoa shukrani zake kwa msaada mkubwa unaotolewa na Shirika la Afya Ulimwenguni wa vifaa pamoja na Dawa kwa Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali Kuu hivi sasa inaandaa mikakati ya kuzuia moja kwa moja mripuko wa maradhi ya Kipindupindu Visiwani Zanzibar.

Balozi Seif alisema Maradhi ya Kipindupindu yameanza kuibuka Zanzibar mnamo mwaka 1978 na kujichomoza  tena Miaka 20 baadaye hali ambayo kwa sasa imezoeleka kuonekana kuwa ya kawaida.

Alisema mazingira hayo ndio yaliyoifanya Serikai Kuu kupitia Halmashauri za Wilaya kuweka mikakati ya udhibiti wa uuzwaji wa bishara holela hasa zile za maji maji katika kipindi kinachoibuka  maradhi ya kuambukiza ya Kipindipindu.

Balozi Seif  alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haina nia ya kuwanyanyasa Wananchi hasa Wafanyabiashara wadogo wadogo kwa kuwazuia na kuwafungia biashara zao katika kipindi cha mzipuko wa maradhi, lakini kinachozingatiwa zaidi ni kuona Afya za Wananchi wote Nchini zinakuwa salama.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  alieleza kwamba wakati huu Wataalamu wa Afya wakiendelea na juhudi za kuwapatia Wananchi taaluma za kujiepusha na Maradhi mbali mbali yakiwemo ya Kipindupindu jitihada zinachukuliwa na Mamlaka ya Maji Zanzibar  katika kutibu Maji yanayosambazwa kwa ajili ya matumizi ya Wananchi.

Balozi Seif  alimueleza Mwakilishi huyo wa Shirika la Afya Ulimwenguni kuwa mahitaji makubwa yaliyopo kwa wakati huu ni upatikanaji wa Dawa za kutibu Maji kwa vile Wananchi walio wengi Nchini wameshaelewa umuhimu wa Dawa hizo kwa lango la kukinga Afya zao.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana kwa mazungumzao na Mwenyekiti wa Kampuni ya Complant kutoka Jamuhuri ya Watu wa China Bibi Liu Yan Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo Balozi Seif alisema Kampuni ya Complant imekuwa kiungo muhimu kilichosaidia kuimarisha uhusiano wa muda mrefu kati ya Jamuhuri ya Watu wa China na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema kiungo hicho kinatokana na Kampuni hiyo kuhusika na ujenzi wa Njia ya Reli kati ya Tanzania na Zambia katika Miaka ya 70 kupitia mradi wa pamoja wa nchi hizo wa TAZARA.

Akizungumzia miradi ya maendeleo na ustawi wa jamii inayotekelezwa na Zanzibar Balozi Seif alimueleza Mwenyekiti huyo wa Kampuni ya Complant kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bado inahitaji kuwa na kianzio mbadala cha umeme wa hakiba ikijitayarisha kukabiliana na athari yoyote inayoweza kujitokeza kwa vile hivi sasa inatumia kianzio kimoja kutoka Tanzania Bara.

Alisema kwa sasa kinachosubiriwa ni Ripoti ya utafiti uliofanywa wa umeme gani wa hakiba unaoweza kuanzishwa kati ya ule unaotokana na upepo, jua, mawimbi ya Bahari na ule unaotumia Mafuta.

Balozi Seif alifahamisha kwamba utafiti huo unafanywa na Wataalamu mbali mbali  wa ndani na nje ya Nchi chini ya gharama pamoja na usimamizi wa Mataifa ya Muungano wa Ulaya {EU}.

Mapema Mwenyekiti wa Kampuni ya Kimataifa ya Uhandisi ya Complant kutoka Jamuhuri ya Watu wa China Bibi Liu Yan alisema ziara yao Visiwani Zanzibar wameshuhudia maendeleo makubwa yaliyofikiwa katika miradi ya Kiuchumi na kustawisha Wananchi wake.

Bibi Yan alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Kampuni yake iko tayari kuendeleza miradi ya ujenzi wa Hoteli za Kitalii ili kuunga mkono jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha Sekta hiyo muhimu kwa mapato ya Taifa.

Alisema hatua hiyo imelenga kuharakisha uhusiano wa kirafiki wa muda mrefu uliopo kati ya Jamuhuri ya Watu wa China na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Vikiwemo Visiwa vya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.