Habari za Punde

Wadau wa Elimu Wawahimiza Wanafunzi Kujisomea Vitabu.

Na.Salmin Juma Pemba.

Serikali na wadau wengine wa elimu Zanzibar kwa nyakati tofauti wamekua wakisikika kuwahimiza wanafunzi kujisomea vitabu ili kukuza maarifa na kujitengenezea njia madhubuti za kufanya vizuri katika mitahani yao lakini azma hiyo inaonekana kua ni changamoto kufikiwa kwa wanafunzi wa kisiwani Pemba.

Idadi kubwa ya wanafunzi katika kisiwa cha Pemba wanaonekana kuvunjika moyo na usomaji wa vitabu kutokana na maktaba wanayoitegemea licha ya kuwa ni jengo jipya lakini ndani yake kuna upungufu mkubwa wa upatikanji wa vitabu vya kujisomea hali inayowafanya kutojua umuhimu wa uwepo wa maktaba hiyo kisiwani hapo.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi wanafunzi kisiwani humo na wadau wengine katika sekta ya elimu walisema, inakua ni vigumu sana kwa wanafunzi wa Pemba kufanya vizuri kupitia mchango wa vitabu kwakua hawana pakuvipata ingawa vinahitajika.

Abdalla Salim mwanafunzi wa kidato cha tano katika skuli ya sekondari shamiani amesema kuwa, katika masomo yao wanalazimika kusoma vitabu vingi ili wafanye vizuri na kimbilio lao ni maktaba lakini nako hakuna kinachopatikana.

Amefahamisha kua, wanapokwenda maktaba kutafuta vitabu, hulazimika kupoteza muda mrefu kusubiria kitabu kimoja, kitabu ambacho huazimwa na kila mwanafunzi ambapo hata kinapopatikana muda mwigi umeshapotea.

"unaweza kukuta kuna kitabu kimoja tu katika somo fulani na hicho kimoja ni kikongwe mno karatasi zake ,nyengine zimechanika na kutoka kabisa na hata ukikishika unahofia kisije kumalizika ' alisema Salim

Akijibu suala la mwandishi wa habari hizi aliyetaka kufahamu upatikanaji wa vitabu katika maktaba kuu chakechake Khamis Muhammed mwanafunzi anayesubiri matokeo ya kidato cha sita mwaka huu amesema, kwa harakaharaka huwezi kusema kuwa, mwanafunzi wa 'O" level mpaka "A" level kama anaweza kufanikiwa kupitia maktaba hiyo.

Alisema kuwa, katika maktaba hiyo kuna mapungufu ya vitabu kiasi ambacho unaweza kukuta kuna kitabu kimoja au viwili tu ikiwa ni cha simulizi au riyaya katika vitabu vinavyosomeshwa skuli, idadi ambayo haiendani na wanafunzi waliyopo kisiwani Pemba.

"mfano kuna kitabu cha CHUNGU TAMU vipo viwili tu na USALITI WA MJINI kipo kimoja" alisema Suleiman
Mwanafunzi wa sku ya sekondari Jadida Wete wa "O" level (jina limehifadhiwa) alisema, mpaka kufika sasa pemba bado haijawa na maktaba ya kuaminika na tegemezi kwa wanafunzi wa sekondari kutokana na kila kinachohitajika katika vitabu ni vigumu kupatikana.

Mwanafunzi huyo alieleza , hutoka masafa marefu kutoka Wete hadi chakechake ilipo maktaba hiyo (mwendo wa Maili 18) kutafuta vitabu kujisomea lakini huambulia patupu, amsema kutokana na gharama za usafiri wanazozipoteza wameamua kubakia nyumbani na kutumia ujanja mwengine wa kujisomea.

Mkutubi mkuu katika maktaba kuu Pemba bi Mwache Muhammeda alipotafutwa na mwandishi wa habari hii kuzungumzia kadhia hiyo alionekana kukubali kuwepo tatizo la upungufu na uhaba wa vitabu vya kusomea kwa wanafunzi wa sokondari katika maktaba yake.

Amesema wao kama maktaba hawana mtaala wa wanafunzi ili kujua kunahitajika kitabu gani "utaratibu wetu wa kupata vitabu ni kuletewa kutoka unguja sio sisi tunaonunua, lakini pia hatuwezi kuleta vitabu mpaka tupate orodha (list) ya vitabu vinavyotakikana, ndio tunaweza kuagiza kuwa kunahitajika vitabu fulani" alisema Muhammed.

Akielezea zaidi alifahamisha ,mapungufu hayo muda mwengine yanapelekewa na baadhi ya wanafunzi wasiokua waaminifu ambao huazima kitabu na kutorudisha tena jambo ambalo pia linawasumbua na kupelekea kuingia katika kadhia hiyo.

Kwa upande weke raisi wa Zanzibar Teachers Union chama cha walimu Zanzibar (ZATU) Maalim Seif Mohd Seif ambae ni mdau katika sekta ya elimu amesema maktaba ni sehemu moja muhimu sana ya kupata kila kinachohitajika katika vitabu na huduma nyengine na panapotokea kinyume chake huwa ni changamoto kubwa kwa wahitaji hususan wanafunzi.

Amesema kutopatikana vitabu kwa wanafunzi katika jengo hilo inapelekea yale malengo ya wizara ya elimu ya kutoa elimu bora kutofikiwa na ni hasara kubwa kwa taifa.

Amemalizia kwa wito wa kuitaka serikali kulitazama jambo hilo kwa maslahi ya taifa ili wanafunzi wapate vitabu vya kujisomea na elimu izidi kupanuka.

"maktaba sio jengo ,maktaba ni vitabu" alisema Maalim Seif

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.