Habari za Punde

Wananchi Kisiwani Pemba Wapata Elimu ya Sheria ya Ardhi.


Na.Haji Nassor - Pemba.
Jamii imetakiwa kujisomea sheria mbali mbali zinazohusu ardhi, ili kujiepusha na migogoro, inayoweza kujitokeza wakati wanapotaka kuitumia kwa kazi tofauti, ikiwa ni pamoja na ujenzi.
Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC Tawi la Pemba, Bi.Fatma Khamis Hemed alipokuwa akiwasilisha mada ya sheria na matumizi ya ardhi no 12 ya mwaka 1992, kwa wasaidizi wapya wa sheria, kwenye mafunzo yaliofanyika mjini Chakechake.
Alisema, zipo sheria saba zinazohusu masuala ya ardhi ikiwemo ya sheria ya kumtambua na kumthibitisha mwenye kumiliki ardhi no 8 ya mwaka 1990, sheria ya mahakama ya ardhi no 7 ya mwaka 1994.
Alieleza kuwa sheria nyengine ambazo jamii inapaswa kuzielewa, ni ile ya kamisheni ya ardhi ya mwaka 2015 sambamba na sheria ya usajili wa ardhi no 10 ya mwaka 1990, ambayo inaelezea umuhimu na ulazima wa kusajili ardhi.
Hivyo Mratibu huyo wa ZLSC, amesema kwa vile hakuna kinga kwa mtu asiyejua sheria,  ni vyema kwa jamii ikafanya juhudi za kuzielewa.
“Jamii ikitumie kituo chetu kujifunza mambo mbali zikiwemo sheria za ardhi na nyengine, ili wajiepushe na migogoro isiyokuwa ya lazima”,alieleza.
Kwa upande wake, Hakimu wa Mahakama ya ardhi Pemba Mhe. Khamis Rashid akiwasilisha sheria ya Mahakama hiyo no 7 ya mwaka 1994, alisema lengo la kuwepo kwa mahakama hiyo, ni kupunguza mrundikano wa kesi, kwenye mahakama za kawaida.
“Kabla ya kuwepo kwa mahakama hii, ilikuwa kesi zote zinazohusiana na ardhi zilikuwa kwenye mahakama nyengine, lakini kuanzia mwaka 1994, zimeanza kusikilizwa na mahakimu maalum”,alifafanua.
Nae Naibu Mrajisi wa usajili Asha Suleiman Said, alisema lengo la kuanzishwa kwa kamisheni hiyo ni kuwa na chombo kimoja cha kusimamia ardhi, ambapo hapo kabla kulikuwa na taasisi tofauti zilizokuwa na kazi moja.   
Aidha alieleza kuwa, kazi nyengine ni kuweza kuifanyia tathmini ardhi na kuanziasha kodi, hivyo ni wajibu wa jamii na wasaidizi wa sheria kuisoma na kuielewa.
Wakichangia mada kwenye mafunzi hayo, wasaidizi hao wa sheria walisema, elimu kwa jamii inahitajika sana hasa kwa vile zipo sheria saba zinazozungumzia masuala ya ardhi.
Msaidizi wa sheria kutoka Jimbo la Chambani Idrisa Khamis alisema sheria zipo nzuri, ingawa jamii imekuwa ikikosa kuzielewa.

Mafunzo hayo ya siku mbili yaliowashirikisha wasaidizi wa sheri kutoka majimbo ya uchaguzi kisiwani Pemba, mada kadhaa zilijadiliwa ikiwa ni pamoja na usajili wa ardhi no ya mwaka 1990, sheria ya kamisheni ya ardhi  ya mwaka 2015 pamoja na sheria ya matumizi ya sheria ardhi no 12 ya mwaka 1992.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.