Habari za Punde

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
Description: Description: Description: Description: Description: Coat of ArmsKURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
Simu: 255-22-2114512, 2116898
E-mail: press@ikulu.go.tz
Tovuti : www.ikulu.go.tz

Faksi: 255-22-2113425


OFISI YA RAIS,
      IKULU,
 1 BARABARA YA BARACK OBAMA,  
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 21 Agosti, 2017 amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA),Bwana Shinichi Kitaoka Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Katika Mazungumzo hayo Bw. Kitaoka amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa uongozi mzuri na wa mfano hususani katika kupambana na rushwa na msukumo mkubwa anaoutoa katika maendeleo hususani katika kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Jitihada  zinazosaidia kuimarisha uchumi na kuboresha huduma za kijamii na kuahidi kuwa JICA itaendelea kuwa mshirika mkubwa wa maendeleo kwa Tanzania.

Bw. Kitaoka ambaye ni mara yake ya kwanza kuitembelea Tanzania kama Rais wa JICA amemuahidi Rais Dkt Magufuli kuwa miradi yote ya maendeleo ya nyuma na ya sasa inayotekelezwa kwa pamoja kati ya  Tanzania na JICA itamalizika kwa wakati ikiwemomradi wa ujenzi wa barabara za juu (Flyover) wa TAZARA unaoendelea kujengwa hivi sasa,mradi wa ujenzi wa barabara ya Mwenge - Moroco yenye urefu wa kilomita 4 nukta 3 pamoja na mradi wa ujenzi wa daraja la Gerezani.

“Tumefikia makubaliano mazuri kuhusiana na miradi tunayoendelea kuitekeleza hapa nchini na wananchi watarajie kuona kazi zikifanyika kuanzia mwezi june,mwakani hususani katika ujenzi wa daraja la gerezani na mingineyo”

Kwa upande wake Mhe. Dkt Rais Magufuli amemshukuru Rais huyo wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la JapanBw. Shinichi Kitaoka kwa uamuzi wake wa kuja Tanzania na amemhakikishia kuwa Tanzania inatambua mchango mkubwa ambao Japan inautoa katika maendeleo ya Tanzania kupitia JICA, na kwamba itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na Japan katika masuala mbalimbali.

Mhe. Rais Magufuli ameishukuru JICA kwa kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi jijini Dar es Salaamikiwemo upanuzi wa barabara ya Mwenge – Morocco, utakaoiwezesha barabara hiyo kuwa na zaidi ya njia nane, ujenzi wa barabara ya TAZARA, ujenzi wa Daraja la Gerezani njia nne, na barabara ya Bendera tatu hadi Kamata.

“Tunathamini sana mchango unaotolewa na walipa kodi wa Japan kupitia JICA katika kutekeleza miradi ya maendeleo hapa nchini na ninakuomba kuangalia uwezekano wa kufadhili na kujenga miundo mbinu na miradi mbalimbali ya maendeleo katika Makao Makuu ya nchi Dodoma ambako serikali imedhamiria kuhamia huko ili kuweka alama ya urafiki na mahusiano mema yaliyopo kati ya Tanzania na Japan

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Balozi wa Japan hapa nchini Mhe. Masaharu Yoshida,Katibu Mkuu wizara ya Fedha na Mipango Doto James,Katibu Mkuu Ujenzi Mhandisi Joseph Nyamhanga na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini Mhandisi Patrick Mfugale.


Emmanuel Buhohela,
Mwandishi wa Habari,Msaidizi wa Rais,
Dar es Salaam.

21 Agosti, 2017

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.