STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
04.08.2017
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, ameeleza kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar itachukua juhudi za makusudi kuzihakiki na kuzitambua eka tatu zilizotolewa kwa
wananchi na Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume baada
ya baadhi yao waliopewa kwenda kinyume na lengo lililokusudiwa.
Dk. Shein aliyasema hayo, alipokutana na uongozi
wa Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira, Wajumbe wa Bodi ya Kamisheni ya
Ardhi na Uongozi wa Kamisheni ya Ardhi katika vikao vinavyoendelea Ikulu mjini
Zanzibar.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa eka
zimebadilishwa mwelekeo na baadhi ya wananchi waliopewa eka hizo kwa lengo la
madhumuni mazuri wamebadilisha mwelekeo na wengine wamekuwa wakiziuza na
wengine wamediriki hata kuzikata viwanja.
Alisisitiza kuwa juhudi za makusudi zitachukuliwa
katika kuhakikisha ufumbuzi unapatikana juu ya suala hilo.
Aidha, Dk. Shein alisisitiza haja kwa Bodi ya
Kamisheni ya Ardhi kufanya kazi kwa uaminifu, uadilifu na ukweli kwani kwa muda
mfupi imeonesha kupata mafanikio makubwa hivyo ni vyema ikaongeza spidi ili
ipate mafanikio zaidi.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza azma ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuendelea kuyahakiki mashamba yote ya
karafuu ya Serikali Unguja na Pemba ili kuweza kuyatambua.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alisisitiza haja ya
kuimarishwa kwa mashirikiano kati ya uongozi wa Wizara, Bodi pamoja na
wafanyakazi wa taasisi za Wizara hiyo ili waweze kuendelea kufanya kazi kwa
ufanisi zaidi.
Dk. Shein pia, alisisitiza umuhimu wa usimamizi
katika kazi kwa viongozi kwani bado kumekuwepo kuoneana muhali, woga na kujenga
hofu kwa wafanyakazi ambao wamekuwa wakikeuka maadili, taratibu, sheria na
kanuni za kazi.
Aliongeza haja ya kufanya kazi kwa kufuata Sheria
na utaratibu bila ya kumpendelea mtu huku akitilia mkazo kufuatwa kwa Sheria ya
ardhi pamoja na sheria nyengine zote zinazoendana na taratibu za ardhi pamoja
na ile sheria ya Kamisheni ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2011.
Kwa upande wa mafanikio, Dk. Shein alitoa pongezi
kwa Bodi ya Kamisheni ya Ardhi kwa mafanikio iliyoyapata sambambana huku
akieleza kuwa Zanzibar ni miongoni mwa nchi za mwanzo za Afrika ya Mashariki
zilizoanza na Sheria za ardhi na si mwanagenzi wa masuala hayo hivyo, ni vyema
zikafuata ili mafanikio zaidi yaendelee kupatikana.
Nae Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Idd, alisisitiza azma ya wananchi wa Zanzibar kupewa eka tatu tatu ikiwa ni
pamoja na kulima ili waweze kuendesa maisha yao wao na familia zao na si
vyenginevyo.
Aliongeza kuwa kisheria kwa wale wote waliopewa
heka tatu tatu pale wanapofariki ni lazima warithi warudi serikalini kwa lengo
la kurithishwa kwa wale walioorodheshwa lakini ni bahati mbaya kwa baadhi ya
wananchi waliopewa heka hizo hawafanyi hivyo.
Balozi Seif alitumia fursa hiyo kuipongeza Bodi
hiyo pamoja na kueleza imani iliyopo kwa Bodi hiyo kutokana na uongozi wake.
Mapema Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira
Salama Aboud Talib alieleza juhudi
zinazoendelea kuchukuliwa na Wizara yake kwa kushirikiana na Bodi hiyo katika
kutatua changamoto mbali mbali zilizokuwepo na kueleza mashirikiano yaliokuwepo
kati ya Wizara hiyo na taasisi nyengine ikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Zanzibar.
Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee nae kwa upande wake alisisitiza haja ya Bodi
hiyo kutembelea katika maeneo ya ardhi badala ya kufanya kazi ofisini pekee kwa
lengo la kuonana na wananchi na kutatua changamoto ziliozpo.
Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Said Hassan nae kwa
upande wake alisisitiza haja ya kuzijua na kuzifuata sheria zote zinazojikita na
masuala ya ardhi hasa ikizingatiwa kuwa eneo la ardhi ndio linaloongoza kwa
kuwa na sheria nyingi.
Akitoa maelezo yake, Mwenyekiti wa Bodi ya
Kamisheni ya Ardhi Abdi Khamis Faki alieleza mafanio, dira, mwelekeo, madhumuni
na changamoto za Bodi hiyo ikiwa ni
pamoja na kuanza kwa matayarisho ya ramani mpya ya Zanzibar kwa kutumia picha
kwa utaalamu wa kisasa (drones).
Nae Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Ardhi Rashid
Abdulrahman Rashid alieleza mafanikio yaliopatikana katika Kamisheni hiyo ya
Ardhi kwa kipindi kifupi pamoja na kueleza jinsi mashirikiano mazuri
wanayoyapata kutoka kwa Washirika wa maendeleo ikiwemo nchi ya Finland katika
kutekeleza miradi mbali mbali ukiwemo mradi wa kujenga uwezo wa taasisi
zinazohusika na sekta ya ardhi.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment