Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein Asema SMZ Kuliimarisha Zao Karafuu na Kuwaneemesha Wakulima wa Zao Hilo.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
  Pemba                                                                                                                   23.08.2017
---
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesema kuwa lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar la kuliimarisha zao la karafuu ni kuwaneemesha wakulima wa zao hilo na kuwafanya wawe na maisha bora zaidi kuliko ilivyo sasa.

Amesema mipango ya kuliongezea thamani zao hilo pamoja na kuyatambua mashamba ya Serikali inalenga kuwaongezea kipato wananchi pamoja na kuwaweka utaratibu mzuri ambao baadae utawafanya wanaoyatumia vyema na kwa uadilifu mashamba hayo kuweza kumilikishwa.

Dk. Shein aliyasema hayo leo mara baada ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumaji na uchambuaji wa karafuu huko katika kambi ya Karafuu ya Mshashani ya mkulima Mohammed Kai Bakari iliyopo Kifundi,Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Amesema utaratibu wa sasa ambapo wakulima wa karafuu wanauza karafuu zao Shirika la Taifa la Biashara (ZSTC) kama zilivyo baada ya kukaushwa na ZSTC kuuza kwenye soko la dunia, haziipi faida kubwa serikali wala mkulima kuliko ambavyo zao hilo lingeongezwa thamani.

Kutokana na hali hiyo, Dk. Shein amesisitiza kuwa tafiti zitaendelea kufanywa kwa lengo la kuliongezea thamani zao hilo la karafuu na kuna haja ya wanasayansi waongeze kasi katika kuliongezeza thamani zao hilo.

Aidha, amesema mchakato wa sasa ambao serikali unaendelea nao wa kuyatambua mashamba yake hatimaye utaweka utaratibu mzuri wa kuwamilikisha wakulima wanaoyatumia vizuri.

Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanya uwamuzi wa makusudi wa kuliongezea bei zao hilo kwa lengo la kulipa heshima zao la karafuu.



Aliongeza kuwa Serikali haina nia wala lengo la kuwanyanganya wakulima mashamba ya karafuu kama inavyoelezwa na baadhi ya watu wachache bali ina mpaongo wa kuyatambua mashamba yake yote ya karafuu pamoja na eka za serikali.

Dk. Shein alieleza kuwa kila mwenye haki ya kupewa shamba ama heka atapewa kwa taratibu zitakazopewa na wale wenye kuyashughulikia mashamba hayo hivi sasa watapewa kipaumbele.

Nae Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Hamad Rashid Mohamed alitoa shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa kushiriki vyema katika shughuli ya uchumaji na uchambuzi wa karafuu.

Aliongeza kuwa ukulima wa zao la karafuu ni mgumu hivyo hatua za serikali za kuwaongezea wakulima beo za zao hilo na kutoa agizo kuwa asilimia 80 ya bei ya dunia walipwe wakulima ni mfano mzuri wa kuonesha kuwa Rais Dk. Shein na Serikali anayoiongoza inawajali wakulima.

Mapema Dk. Shein alipata maelezo juu ya ukodishwaji wa zao hilo la karafuu ulioanza tarehe 5 mwezi huu na tayari mashamba 100 yameshakodishwa yenye thamani ya TZS 158.9.

Shamba la mzee Mohammed Bakari Kai lima mikarafuu 125 bado halijakodoshwa lakini wakati ukifika wa ukodishwaji kipaumbele kitawekwa kwa msimamizi wa shamba hilo ambaye ni mkulima maarufu na mwenye sifa za kilimo ambaye aliwahi kupewa zawadi ya mkulima bora hapo mwaka juzi.

Balozi Ali Karume ambaye ni Kaimu Waziri wa Bishara, Viwanda na Masoko alieleza haja ya kulithamini zao hilo kwani ni zao la uchumi hapa nchini.

Nae mkulima huyo Mohammed Kai alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa hatua yake ya kufika katika shamba na hatimae katika kambi yake na kujionea shughuli za kambini hapo na kuungana na wakulima kwa kuchambua karafuu.

Mkulima huyo alieleza anavyofarajika na juhudi za Dk. Shein chini ya Serikali anayoiongoza katika kuliimarisha zao hilo la karafuu huku akieleza uzoefu wake katika kilimo cha karafuu pamoja na zawadi alizowahi kupewa kutokana na ukulima wake.

Mapema Dk. Shein aliweka jiwe la Msingi katika Skuli ya Chiba na kueleza azma ya Serikali ya kuiendeleza skuli hiyo ili watoto wapate fursa ya kusoma na kuondoa tatizo la kwenda skuli za mbali na makaazi yao.

Dk. Shein aliwapongeza wazee pamoja na Mfuko wa Halmashauri kwa juhudi kubwa walizozichukua katika ujenzi wa madarasa manne ya skuli hiyo pamoja na ofisi za mwalimu mkuu ambapohadi kufikia hatua hiyo ujenzi umegharimu TZS milioni 37.3.

Aidha, aliwataka watoto wa Chimba wasome kwa juhudi kubwa na kuwasisitiza kuwa Chimba itajengwa na wanachimba wenyewe.

Aidha, aliwata walimu kuwasomesha watoto vyema na wasichanganye elimu na siasa wala wasisomeshe kwa kuwababaisha kwani lengo ni kuwapa elimu bora watoto wote.

Pamona ja hayo, Dk. Shein aliwahakikishia wananchi wa Chimba kuwa barabara yao yenye urefu wa kilomita 8.9 itajengwa kwa kiwango cha lami.

Akiwa katika ziara hiyo Dk. Shein aliweka jiwe la msingi katika Tawi la CCM Njuguni na baadae kupigisha harambee kwa lengo la kumaliza ujenzi wa Tawi hilo ambapo zilipatikana fedha zote milioni saba ambapo yeye alichangia milioni mbili.

Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa ujenzi wa matawi ya chama ni njia moja wapo ya kukiimarisha chama hicho na hatimae kuweza kuongeza wanachama na kuweza kufanya vyema shughuli za chama kwa ufanisi zaidi.

Kabla ya hapo Dk. Shein alipokea taarifa ya Mkoa wa Kaskazini Pemba hapo katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa SUZA, Mchangamdogo.


 Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.