Habari za Punde

Skuli ya Highlight Wawi yaomba kuungwa mkono na Serikali


Skuli ya Maandalizi na Msingi ya Highlight  , ilipo Wawi Chake Chake Pemba.


Picha na Bakar Mussa -Pemba.



Na Bakar Mussa-ZANZIBARLEO.

Mkurugenzi mkuu wa Skuli ya Maandalizi na Msingi ya Highlight, ilioko Wawi Chake Chake Pemba, Hamad Bakar Ali, ameiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar , kuunga mkono juhudi zilizochukuliwa na Uongozi wa Skuli hiyo katika kuinuwa kiwango cha Elimu nchini.

Alisema Skuli ya Highlight, ambayo ilianza na kutowa Elimu ya maandalizi katika masomo ya Sayansi na Lugha, ilianzishwa kwa lengo la kuisaidia Serikali katika kuinuwa kiwango cha Elimu nchini, ambapo kwa wakati huu imepata maendeleo makubwa pamoja na changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo.

Hamad , alieleza hayo huko Chake Chake Pemba, wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi , juu ya azma ya kuiboresha Skuli hiyo sambamba na kuanzisha Chuo ambacho kitatowa mafunzo mbali mbali ambayo mbali na Elimu ya darasani pia itamuwezesha Kijana kuweza kujiajiri.

“ Tunayo azma kubwa mungu akipenda tuanzishe Chuo ambacho kitatowa mafunzo mbali mbali katika sehemu hii ambayo Skuli hii ipo na baadae Skuli hii tuihamishie katika eneo letu lililoko Mabaoni Chake Chake , kwa lengo la kuwasaidia Vijana kupata mafunzo ya fani mbali mbali,” alieleza Mkurugenzi huyo.

Alifahamisha Skuli hiyo ilianza mwaka 2016 , ikiwa na Wanafunzi 30 wa Nasari pekee ,ambapo kwa sasa wanao Wanafunzi 120 ambao husoma masomo ya Sayansi na Lugha , na hao walianza hapo  maandalizi hadi  Darasa la Kwanza.  

Mkurugenzi huyo, alisema pamoja na mafanikio walioyapata kwa kufanya mahafali ya mwanzo na kuwawezesha Wanafunzi kuendelea na Darasa la Kwanza hapo, lakini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbali mbali kama vile huduma ya Maji Safi na Salama, Umeme , Vifaa vya kuchezea Wanafunzi wa Nasari na hata Computer.

Kwa upande wake , Mkuu wa taaluma , Ibrahim Abdulaziz , kwa niaba ya Mwalimu mkuu wa Skuli hiyo ,alisema lengo la Skuli hiyo ni kwenda mpaka Sekondari kwani uwezo wa kufanya hivyo kama wataruhusiwa na Wizara utakuwepo hapo baadae kutokana na Wanafunzi wao kuwa na upeo mzuri.

“ Sisi hatutaishia hapa , lengo letu ni kufikia hatuwa ya Sekondari iwapo tutaruhusiwa kufanya hivyo , kwani Wanafunzi wetu tumekuwa tukiwaandaa vizuri na maendeleo yao tunapowapima wanatupa hamasa ya kuwa nao katika Elimu hiyo,” alieleza.

Akizungumzia suala la mashirikiano baina ya Wazazi , Walimu na Kamati ya Skuli  alieleza yapo yakutosha kwani wanapoitwa hufika kwa wingi na kutowa michango yao ya hali na mali hadi sasa hivi .

Alisema hadi sasa wanashukuru wazazi wa Watoto wako 
bega kwa bega na Walimu hasa ikizingatiwa Watoto waliopo hapo wengi wao ni wadogo na pale wanapoambiwa kunahitajika michango wamekuwa wakitekeleza kwa haraka.

Hivyo wanaomba kuungwa mkono na Serikali yao ili waweze kufikia malengo yao kama walivyokusudia , kwa kukuza kiwango cha Elimu nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.