Na Khadija Kombo--ZBC.Pemba
Jeshi la Polisi Mkoa wa kusini Pemba, linamshikilia Ustaadhi wa Madrasa ya msikiti wa Ijumaa Miembeni Chake Chake Kisiwani Pemba, Khamis Rashid Ali (35), mkaazi wa mvumoni Chake Chake kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wake mwenye umri wa miaka kumi nanne (14) na kumsababishia ujauzito hali ambayo imempelekea kumuathiri mtoto huyo kimwili na kisaikolojia.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba (RPC) ,Mohammed Sheikhan Mohammed alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kwa tuhuma za kumbaka na kumpatiaujauzito mtoto mdogo (14) hivi sasa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi na utakapo kamilika watamfikisha mahakamani kwa kujibu tuhuma hizo.
Kamanda Sheikhan, alisema mara baada ya kupata tuhuma hizo walimchukua mtoto huyo na kumpeleka Hospitali kupimwa na vipimo vilionesha kuwa mtoto anaujauzito wa miezi saba na siku tano.
Bibi wa mtoto huyo ambae ni wa mwanzo kugundua tukio hilo ambae jina lake limehifadhiwa, alisema alipelekewa mtoto huyo na mama yake mzazi kwa lengo la kukaa nae kwa kipindi cha wiki mmoja kutokana na mama huyo kupata dharua na kusafiri.
"Kwa vile huyu alikuwa ni mtoto wa kike anahitaji kuwa chini ya uangalifu wa mtu wakati wote ndio akaona amlete huku kwangu lakini ahh, kumbe mtoto alishakuwa na mtihani" alisema bibi huyo.
Akielezea kwa masikitiko bibi huyo, alisema aligundua tukio hilo baada ya mtoto wake mwengine alieona hali ya mabadiliko ya dada yake huyo na kumuuliza juu ya hali hio.
"Mama vipi mbona huyu dada tumbo lake limekuwa kubwa na hakuwa na tumbo kama hili na mimi ndipo niliposhituka nikaanza kumchunguza kwa makini" alielezea bibi huyo.
Bibi huyo, aliendelea kufahamisha kwamba baada ya uchunguzi aligundua mambo mengi kwani mbali ya kukua kwa tumbo lakini pia hata nguo zake kifuani zilikuwa zikimbana sana tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
"Baada ya kuona hayo moja kwa moja nilianza kuyatia watuni na ndipo alipopelekwa hospitali na kugundulika kuwa ana ujauzito wa miezi saba",alieleza bibi huyo.
Alipoulizwa na mwandishi wetu kuhusu ninani aliyempa ujauzito bibi huyo alisema mtoto mwenyewe alipohojiwa alisema aliyempa ujauzito huo ni mwalimu wake wa madrasa na akamtaja kuwa ni mwalimu Khamis Rashid.
Akizungumza kwa huzuni huku machozi yakimtoka mtoto huyo alisema Ustadh huyo alimbaka ndani ya Ofisi ya madrasa ambayo imo ndani ya Msikiti wa Ijumaa Miembeni Chake Chake.
"Ilikuwa ni mwezi wa pili mwaka huu, ustadh alituita Ofisini tukaandike kombe kila mmoja alikuwa anaandika na anae maliza anatoka nje mimi nikawa wa mwisho kumaliza hivyo aliukomea mlango kisha akaniambia ananipenda nikamwambia mwalimu sitaki mimi ni mtoto mdogo hakuniachia ndipo aliponibaka" alieleza mtoto huyo.
Mama mzazi wa mtoto huyo, ambae alikuwa akizungumza huku akikata chozi alisema kwamba yeye hakujua kabisa kama mtoto wake anaujauzito tukio ambalo limemuathiri sana moyoni mwake.
"Mtoto wangu ni mdogo sana kiumri na kimaumbile hivyo kila nikifikiri na mtihani uliompata ni mzito kwake naendelea kuteketea" alisikitika mama huyo.
Hivyo alisema wakati wote alikuwa akiwaangalia sana watoto wake wa kike na wakiume kutokana na kuhofia hayo hayo ndipo alipopata safari akaamua kumpeleka kwa bibi yake lakini kumbe kule madrasa alikofikiria kuwa ni sehemu salama ndiko alikofikwa na janga mtoto wake .
No comments:
Post a Comment