Habari za Punde

Waziri wa Afya Zanzibar Mhe Mahmoud Thabit Kombo Afungua Kambi ya Matibabu ya Macho (ZU) Tunguu na Kuwataka Wananchi Kutumia Fursa ya Kufanyiwa Uchunguzi na Kupatiwa Matibabu.

Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo akiwasili Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) Tunguu kufungua kambi ya matibabu ya macho ya siku tano inayosimamiwa na madaktari kutoka Chuo Kikuu cha Lahore Pakistan na madaktari wazalendo, (kulia) Mkuu wa Chuo cha ZU Dkt. Mustafa Rashashi.
Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo akizungumza na madaktari na wananchi waliofika katika kambi ya matibabu ya macho wakati wa ufunguzi wa kambi hiyo ZU Tunguuu.
Mratibu wa huduma za macho Zanzibar Dkt. Fatma Juma akitoa maelezo wakati wa ufunguzi wa kambi ya macho iliyopo chuo kikuu cha Zanzibar Tunguu.
Baadhi ya madaktari wa macho kutoka Pakistan na wananchi waliokwenda kutafuta matibabu kambi ya macho Tunguu wakimsikiliza Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo (hayupo pichani).
Kiongozi wa madaktari kutoka Pakistan Prof. Durraiz akimfanyia uchunguzi wa macho Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo ikiwa ni uzinduzi rasmi wa kambi ya matibabu ya macho Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu. Picha na Makame Mshenga.

Na Ramadhani Ali – Maelezo.
Chuo Kikuu cha Lahore nchini Pakistan kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) na  Wizara ya Afya Zanzibar wameandaa kambi ya matibabu ya macho ya siku tano chuo  Kikuu Tunguu chini ya ufadhili kutoka Saudi Arabia.

Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo aliifungua kambi hiyo na kuwataka wananchi wenye matatizo ya macho kutumia fursa hiyo kwenda Tunguu kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu bila malipo.

Alisema madaktari bingwa kutoka Pakistan na Saudi Arabia wakiwa na vifaa vya kisasa vya uchungu wa macho na dawa za kutosha wapo Zanzibar  kusaidia ndugu zao kwa lengo la kuwapunguzia gharama za kufuata matibabu nje ya Zanzibar.

Aliongeza kuwa wananchi watakaohitaji  operesheni  wa macho watafanyiwa katika Hospitali ya Jeshi la Wananchi iliyopo Bububu chini ya wataalamu kutoka Pakistan wakishirikiana na madaktari wazalendo wa Zanzibar.

Aidha Waziri Mahmoud amewaomba wananchi kuwapa ushirikiano madaktari hao kutoka Pakistan na Saudia Arabia muda wote watakapo kuwepo Zanzibar ili watekeleze kazi yao kwa ufanisi.

Mratibu wa huduma za macho kutoka Wizara ya Afya Dkt. Fatma Juma alisema madaktari hao kutoka Pakistan wamejiandaa kufanya operesheni 500 kwa muda wa siku tano watakazo kuwepo Zanzibar hivyo amewashauri wananchi wanaosumbuliwa na matatizo ya macho kuitumia nafasi hiyo ambayo ni adimu kupatikana.

Alisema kuwa madaktari hao wamekuja Zanzibar wakiwa na dawa zote muhimu za matatizo ya macho na wamejiadaa kuwafanyia upasuaji wananchi wote watakaohitaji huduma ya upasuaji.  

Alidokeza kuwa  utafiti uliofanywa miaka ya karibuni unaonyesha watu 6,500 wa Zanzibar wapo katika hatari ya kupata upofu na 3,500 kati yao wanaweza kunusurika iwapo watapatiwa matibabu mapema, hivyo aliwashauri wananchi kujitokeza kwa wingi kufanyiwa uchunguzi.

Kiongozi  wa madaktari kutoka Pakistan ambae ni daktari bingwa wa macho Professa Durraiz alisema wamejiandaa kuwahudumia wananchi wote watakaofika katika kambi hiyo ya Tunguu na watahakikisha wanatoa dawa sahihi kwa kila mgonjwa.

Mkuu wa chuo Kikuu cha Zanzibar Dkt. Mustafa Rashashi amesema lengo la chuo hicho kushiriki kuandaa kambi ya matibabu ya macho ni kutekeleza moja ya malengo ya vyuo vikuu ya kutoa huduma kwa jamii.

Kambi hiyo iliyoanza leo itaendelea mpaka tarehe 10 mwezi huu na Prof. Durraiz amewashauri wananchi wa Zanzibar wenye matatizo ya macho wasiogope gharama ya kufuata matibabu hayo Tunguu kwani huduma zao ni bure.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.