NA HAJI
NASSOR, PEMBA
WANANCHI
wawili kisiwani Pemba, wameripotiwa kufariki dunia, baada ya kuanguka kutoka
juu ya mkarafuu, kati ya wananchi 196 walioanguka, baina ya msimu wa mwaka 2015
hadi mwanzoni mwaka huu.
Akizungumza na wadau wa zao la
kafaruu, Mdhamini wa Shirika la Taifa la Biashara Zanzibar ‘ZSTC’ Pemba Abdalla
Ali Ussi, kwenye mafunzo ya haki za binadamu, yaliofanyika mjini Chakechake,
alisema waliopewa fidia katika kipindi hicho, walikuwa 147, ambapo baadhi
hawakupewa kutokana na sababu mbali mbali.
Alisema katika kipindi hicho shilingi
milioni 130 zilitumika kupitia Shirika la Bima Zanzibar, kwa ajili ya kuwalipa
fidia wananchi hao walioanguka mikarafuu na wengine kufariki.
Alisema kwa msimu wa mwaka 2015 hadi
2016, wananchi walioanguka mikarafuu walikuwa 113, ambapo kati ya hao 108 pekee
ndaio waliolipwa fidia, sawa na shilingi milioni 100 na waliobakia, hawakulipwa
kutokana na kuwa nje ya vigizo na utaratibu wa Shirika husika.
Aidha Mdhamini huyo wa ZSTC, alisema
msimu mwa mwaka 2016/2017 uliomalizika, kulikuwa na wachumaji wa zao la karafuu
63 walioanguka kutoka juu ya mkarafuu, na kuripoti kwenye vyombo husika na 39
tu ndio waliolipwa, sawa na shilingi milioni 30, huku wengine wakikosa malipo
hayo kwa vile wanaendelea na matibabu.
Alieleza kuwa, kazi ya kufanya
tathimini, kuangalia vipimo vya kiwango cha fedha kwa muangukaji wa mkarafuu,
hufanywa na Shirika la Bima Zanzibar, ambapo ZSTC hutoa fedha hizo kila msimu.
‘Sisi kila msimu ndio tunawapa fedha
wenzetu wa Shirika la Bima, lakini suala la kutoa fedha na viwango husika,
jukumu hilo bado wanalo wenyewe Bima”, alifafanua.
Katika hatua nyengine, Mdhamini huyo
wa ZSCT Pemba, aliwataka wananchi kuacha tabia ya kuhifadhi karafuu zao
majumbani, kwani zinatabia ya kupungua uzito kila baada ya muda.
“Mkizihifadhi zinapungua uzito, na
kama mnataka kuziweka basi njooni ZSTC mchukue kibali au museme muhifadhiwe,
lakini usikae nazo nyingi bila ya kufuata taratibu zinavyoelekeza”, alifafanua.
Akiwalisha ufafanuzi wa sheria ya no 2
ya mwaka 2014 ya maendeleo ya karafuu, Afisa Mipango wa ZLSC tawi la Pemba,
Mohamed Hassan Ali, alisema sheria hiyo imefanyiwa marekebisho na kueleza maana
ya magendo na aina zake.
Mapema akifungua mafunzo hayo,
Mratibu wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba, Fatma Khamis
Hemed, alisema kituo kimekuwa na mpango wa kuyawezesha makundi kadhaa
kitaaluma, ili yafahamu sheria.
Alisema wadau hao wa zao la karafuu,
ni moja kati ya hao wengi, ambapo iwapo watakuwa makini kwenye mafunzo hayo,
wataweza kuwaleimisha wenzao.
Wakichangia mada kadhaa washiriki
hao, walisema bado jamii haijaelimishwa vya kutosha juu ya kanuni na sheria za
karafuu, hali iliopelekea wananchi kuhisi wanaonewa juu ya maamuzi mbali mbali
ya serikali.
Katika mafunzo hayo ya siku mbili,
mada kadhaa zilijadiliwa ikiwa ni pamoja na taratibu za upatikanaji wa fidia
kwa wanaoanguka mikarafuu, kanuni na sheria ya maendeleo ya karafuu, haki za
binadamu na majukumu ya wadau wa wazao la karafuu.
No comments:
Post a Comment