STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
21.09.2017
UHUSIANO na ushirikiano wa vyuo vya ndani na nje ya Zanzibar
unaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha sekta ya elimu kwa vyuo
vikuu vya Zanzibar kikiwemo Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).
Hayo yalielezwa na
Makamo Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Profesa Idris Ahmada Rai
wakati alipokuwa akizungumza na Makamo
wa Rais wa Taasisi ya ‘China National Research Institute of Food and Fermentation
Industries’ (CNRIFFI) Profesa Huang Yutong huko katika ofisi za chuo hicho
Tunguu Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.
Katika mazungumzo
hayo, Profesa Rai alimueleza Makamo wa Rais wa Taasisi hiyo ya (CNRIFFI) ya
nchini China kuwa uhusiano na
ushirikiano kati ya SUZA na Taasisi hiyo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha
mahusiano kati ya Zanzibar na China.
Alisema kuwa uhusiano
huo utaweza kuimarisha zaidi azma ya kukuza sekta ya elimu hapa nchini sambamba
na kuendeleza sekta nyengine muhimu za kimaendeleo ikiwemo sekta ya utalii.
Profesa Rai alitumia fursa
hiyo kutoa pongezi na shukurani kwa Serikali ya China na kueleza kuwa nchi hiyo
ina uhusiano na urafiki mwema na Zanzibar kwani tayari taasisi na vyuo vingi
vikuu vya nchi hiyo vimeshaonesha azma ya kushirikiana na Chuo hicho cha Taifa
cha Zanzibar hatua ambayo alisema inaleta matumaini makubwa katika kuimarisha
sekta ya elimu nchini.
Aliongeza kuwa Chuo
Kikuu cha SUZA kupitia Tawi lake la Chuo cha Utalii kilichopo Maruhubi
kitahakikisha kinatoa mafunzo katika kada mbali mbali za utalii ikiwa ni pamoja
na mafunzo juu ya mapishi, ukarimu na mengineyo kwa kutambua kuwa bado kuna
mahitaji ya mafunzo hayo kwa wafanyakazi walio wengi hapa nchini hasa wale
wanaoifanya kazi sekta ya utalii.
Pamoja na hayo,
Profesa Rai alimpongeza Makamo huyo wa Rais wa Taasisi ya (CNRIFFI) kwa kuja
Zanzibar yeye na wakufunzi wenye ujuzi mkubwa na kuitikia wito kwa vitendo wa
kuja kutoa mafunzo kwa watendaji wa Serikali wanaotoa huduma za upishi na
ukarimu kwa viongozi wakuu wa nchi pamoja na walimu kutoka Taasisi ya Utalii
iliyopo Maruhubi.
Nae Makamo wa Rais wa
Taasisi ya ‘China National Research Institute of Food and Fermentation Industries’
kutoka nchini China Huang Yutong alionesha kuvutiwa na mipango pamoja na
mikakati ya Chuo Kikuu cha SUZA katika kutoa elimu hasa katika sekta hiyo ya
utalii na kueleza kuwa taasisi yake iko tayari kushirikiana na SUZA katika azma
kuendeleza utalii hapa nchini ambao tayari umeonesha kuimarika.
Kiongozi huyo
aliongeza kuwa uhusiano na ushirikiano kati ya Taasisi hizo utaweza kusaidia
kwa kiasi kikubwa katika kufikia lengo la Serikali la kutoa mafunzo
yatakayoinua sekta ya utalii.
Alieleza kuwa mafunzo
ya mapishi, ukarimu na yale yote yanayohusiana na kada hiyo yanaweza kusaidia
kwa kiasi kikubwa katika kutoa elimu hiyo itakayosaidia kuimarisha sekta ya
utalii na hata utamaduni wa hapa nchini.
Pamoja na hayo, Huang
Yutong alieleza kuvutiwa kwake na aina ya vyakula mbali mbali vya Zanzibar na
kusema kuwa iwapo mikakati maalum itawekwa katika kuvitangaza na kuvipa
kipaumbele vyakula hivyo itakuwa ni kivutio chengine kikubwa cha utalii mbali
ya kuweko vivutio kadhaa vikiwemo viuongo.
Huang Yutong
alimuhakikishia Profesa Rai kuwa Taasisi ya (CNRIFFI) imekusudia kutoa mafunzo
kwa wapishi wakuu ili waweze kuhudumia na kuwa na sifa za kutoa huduma za
kitaifa na kimataifa.
Wakati huo huo, Huang Yutong alitembelea
Taasisi ya Kilimo Kizimbani ambapo alipata maelezo kutoka kwa Mwalimu wa
taasisi hiyo Foum Ali Garu nakumueleza kuhusu hatua zinazochukuliwa katika
kuyaimarisha mazao ya viungo na umuhimu wake katika matumizi ya mwanaadamu
sanjari na kuwa kivutio kimoja wapo kikubwa cha utalii.
Nae Profesa Yutong kwa
upande wake ametoa shukurani kwa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi kwa kumuandalia ziara hiyo ya kutembelea Taasisi ya Kilimo Kizimbani pamoja
na mashamba ya viungo na kuweza kuna
viungo hivyo kwa uhalisia.
Alisifu jitihada
zinazochukuliwa na uongozi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Kizimbani kwa kuendelea
kuvihifadhi viungo vilivyopo na kuweza kuwapa taaluma ya uhakika wageni
wanaotembelea eneo hilo.
Sambamba na hayo,Makamo
huyo wa Rais wa Taasisi ya (CNRIFFI)
inayohusiana na mambo ya mapishi na ukaribu ilichopo mjini Beijing
nchini China, ameahidi kuendelea kuziunga
mkono jitihada zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa
kulitangaza eneo hilo lenye viungo vyenye thamani kubwa duniani.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment