Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Aishukura Kuwait Kwa Msaada Wao Huo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi zawadi ya Mlango (Zanzibar door) Naibu Mkurugenzi wa Mfuko wa Kuwait kwa Maendeleo ya Kiuchumi Bwana Hamad S. Al Omar baada ya kuwezesha kusainiwa kwa mkataba wa Mkopo kwa ajili ya ukarabati mkubwa wa hospitali ya Mnazi Mmoja.(Picha na OMPR)

Na. Sharifa B.Juma.OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi azungumza na Ujumbe wa Uongozi wa Mfuko wa Kuwait Kwa Maendeleo ya Kiuchumi ofisini kwake Vuga kwa lengo la kutoa neno la Shukrani baada ya kupatiwa mkopo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya Mradi wa Ukarabati Mkubwa wa Hospitali ya Mnazi Mmoja.
Balozi Seif alitoa shukrani hizo za dhati kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar baada ya Serikali kupatiwa fursa ya kusaini Mkataba wa Mkopo huo chini ya Uongozi wa Mfuko wa Kuwait unaongozwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo Bwana Hamad S. Al Omar.
Kiasi cha Fedha kilichosainiwa na  Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango Dr. Khalid S. Mohammed ni dola za kimarekani Milioni elfu kumi na tatu nukta sita ambazo ni sawa na  zaidi ya Bilioni thelasini za kitanzania kwa ajili ya kuchangia sehemu ya ukarabati mkubwa wa hospitali hiyo.
Sambamba na hayo Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais amemuomba Naibu Mkurugenzi wa Mfuko wa Kuwait kuzidi kuipa fursa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutoa mikopo kwa lengo la  kuendelea kuchangia sekta mbalimbali za kimaendeleo nchini zikiwemo uchumi, elimu na jamii kiujumla.
Balozi Seif ameuambia ujumbe huo kwamba Zanzibar ni nchi yenye amani, upendo na utulivu hivyo hufungua milango ya fursa kwa wawekezaji kuja kuikeza nchini hapa.
Pia wageni wengi huvutiwa na utulivu wa nchi hii jambo ambalo linapelekea kuwepo kwa wageni kutoka nchi mbali mbali duniani kwa lengo la kuekeza na kuiendeleza nchi yetu.
Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais aliusisitiza ujumbe huo  kuwa mlango wa Zanzibar uko wazi kwa mtu yeyote ambae yuko tayari kuja kushirikiana nasi kwa lengo la kusukuma gurudumu la maendeleo ya nchi yetu.
Nae Naibu Mkurugenzi wa mfuko wa Fedha wa Kuwait amesema nchi yake iko tayari kujitolea kwa maendeleo ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo kusaidia sekta ya elimu, afya na nyenginezo.  
Nchi hiyo pia iko tayari mda wowote kuanzia sasa kutoa msaada kwa kila jambo kwa lengo la kukuza mashirikiano yaliyopo baina ya nchi hizi mbili na uboreshaji wa maeneo ya ushirikiano huo baina ya Zanzibar na Mfuko wa Kuwait.

Sharifa Barki Juma
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais
21 Septemba 2017


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.