Habari za Punde

SMZ yataja mambo manane yatakayoibeba Mahakama ya Kadhi


Haji Mtumwa, Mwananchi 

Zanzibar. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imetaja mapendekezo manane iliyoyawasilisha kwenye Baraza la Wawakilishi ambayo yatatumika kuimarisha Mahakama ya Kadhi, huku ikipendekeza kufutwa kwa sheria iliyounda mahakama hiyo.
Katika mapendekezo yake, SMZ imeyataja baadhi ya mambo inayotaka kuyatumia kuboresha mahakama hiyo kuwa ni pamoja na mamlaka ya Mahakama ya Kadhi, ushahidi, kanuni na taratibu za utendaji kazi, muda wa utumishi wa viongozi wakuu wa mahakama hiyo, uwezo wa mahakama, uwepo wa mrajisi wa mahakama na lugha itakayotumika.
Katika mapendekezo yake, Serikali inapendekeza kufutwa kwa Sheria namba 3 ya mwaka 1985 iliyounda mahakama hiyo ikitaka kuanzisha sheria mpya pamoja na kuweka masharti mengine. Mapendekezo hayo yaliwasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Ussi ‘Gavu’ katika mkutano wa saba wa Baraza la Wawakilishi unaoendelea Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Akiwasilisha mapendekezo hayo, Issa alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya kuonekana sheria inayotumika hivi sasa ina upungufu mwingi wa kisheria.
Alisema licha ya ukosefu wa kanuni nzuri za kuendesha mahakama hiyo, sheria haielekezi utaratibu wa usuluhishi ambao ungesaidia kupunguza idadi ya kesi zilizopo mahakamani na pia haiwapi uwezo makadhi kuwashughulikia watu wanaodharau au kutotoa ushahidi unaotakiwa.
“Wengi wanaopata matatizo makubwa katika suala la upatikanaji wa haki katika Mahakama ya Kadhi ni wanawake na watoto hasa baada ya ndoa zao kuvunjika, hivyo tunaamini kuja kwa muswada huu kutasaidia makundi hayo kupata haki zao stahiki na kwa wakati,” alisema Issa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.