Habari za Punde

Tanzania imefanikiwa kuimarisha mifumo ya ufamasia kwa msaada wa jumuiya za ACP na EU

 Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Zanzibar Dkt. Ghirmay Andemichael akizungumza na washiriki wa mkutano wa mwisho wa  Jumuia ya nchi za Afrika, Caribean na Pacific (ACP) wa kumiarisha mifumo ya kifamasia unaofanyika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
 Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Suzanne Hill akitoa hotuba katika ufunguzi wa mkutano wa mwisho wa kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa dawa kwa nchi za ACP katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mbweni.
 Wajumbe wa mkutano wa mwisho wa kuimarisha mifumo ya kifamasia wan chi za kanda ya Afrika Caribean na Pacific wakifuatilia ufunguzi wa mkutano huo unaofanyika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mbweni.
 Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya nchi za ACP Balozi Emile Ognimba akizungumza na washirki wa mkutano wa mwisho wa kuimarisha mifumo ya kifamasia unaofanyika Zanzibar Beach Resort Mbweni.


 Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Bi. Asha Abdalla Ali akifungua mkutano wa mwisho wa kuimarisha mifumo ya kifamasia unaoshirikisha mataifa ya Afrika Caribean na Pacific katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Picha na MAKAME MSHENGA.

Na Ramadhani Ali – Maelezo                                  

Tanzania imefaidika na imepiga hatua kubwa katika kufuata sheria na kuboresha uingizaji wa dawa na vifaa tiba sahihi kufuatia msaada mkubwa wa Jumuia ya nchi za Afrika, Caribean na Pacific (ACP) katika kudhibiti mifumo ya kifamasia kwa nchi za ukanda huo.

Akifungua mkutano wa mwisho wa Jumuiya ya nchi za ACP inayofadhiliwa na Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Bi. Asha Abdalla Ali alisema imefanikiwa kupanga mikakati kuhakikisha dawa zote zinazoingia nchini ni salama kwa matumizi ya binadamu.

Alisema Jumuiya imewajengea uwezo wafamasia kwa mafunzo mbali mbali ya kuboresha upatikanaji, usambazaji na  kusajili dawa zinazoingia ili kuhakikisha zilizokuwa chini ya kiwango haziingizwi nchini.

Katibu Mkuu aliongeza kusema kuwa Jumuiya ya nchi za Ukanda wa Afrika, Carbean na Pacific imefanya juhudi ya kuimarisha Bodi ya Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar na kuhakikisha inatekelezaji majukumu yake kwa ufanisi.

Aidha aligusia kuwa Jumuiya imeiwezesha Serikali kufanya mapitio ya sera yake ya dawa ili kuona inaendana na wakati wa sasa kwa mujibu wa mahitaji na  kuimarisha afya za wananchi.

Bi. Asha alilishukuru Shirika la Afya Duniani na Jumuiya ya nchi za ukanda wa Afrika, Caribean na Pacific kwa misaada yao mikuwa  katika kuimarisha mifumo ya ufamasia nchini.
Akiwakaribisha wajumbe wa mkutano huo kwa niaba ya mwakilishi wa Shirikala Afya Duniani nchini Tanzania, mwakilishi wa Shirika hilo Zanzibar Dkt. Ghirmay Andemichael alisema jukumu la kuwa na  dawa salama katika nchi linahitaji mashirikiano ya wadau mbali mbali ikiwemo taasisi za serikali, viwanda vya uzalishaji na waingizaji dawa.

Akizungumza katika mkutano huo, Mfamasia Mkuu wa Serikali ya Muungano wa Tanzania Hendry Kigunde alisema Jumuiya imetoa msukumo mkubwa katika kipindi cha miaka mitano tokea ilipoanzishwa kwa kuimarisha usambazaji wa dawa kwa njia za kisasa.

Alisema Serikali imefanikiwa kuboresha miongozo ya uingizwaji wa dawa na kuoredhesha dawa muhimu ambazo waingizaji wanashauriwa kuzipa kipaumbele kwa ajili ya matimizi ya wananchi.

Mkutano huo wa siku mbili utafanya mapitio katika kipindi cha  miaka mitano cha Jumuiya ili kujua mafanikio yaliyopatika katika kutandika mifumo sahihi ya dawa kwa nchi wanachama na kufahamu changamoto zilizojitokeza katika kipindi hicho.  

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.