STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 13.10.2017
RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza Serikali ya
Oman chini ya uongozi wa Sultan Qaboos bin Said kwa kuendeleza uhusiano na ushirikiano
na Zanzibar na kueleza kuwa ujio wa meli ya Fulk Al Salamah kutoka Oman ni ishara
upendo wa kihistoria kati ya pande mbili hizo.
Dk.
Shein aliyasema hayo leo katika mazungumzo kati yake na Waziri wa Mafuta na
Gesi wa Oman Dk. Mohammed bin Hemed Al Ruhmi , Ikulu mjini Zanzibar ambaye yupo
Zanzibar kwa ziara maalum ya kuendeleza uhusiano, umoja na upendo akiongoza
ujumbe kutoka Serikali ya Oman ambao umefika nchini kwa kutumia usafiri wa meli
maalum ya Sultan Qaboos iitwayo Fulk Al Salamah.
Katika
mazungumzo hayo, Dk. Shein alimueleza Waziri Mohammed bin Hemed Al Ruhmi kuwa
ujio wa kiongozi huyo pamoja na ujumbe wakiwemo mawaziri kutoka Serikali ya
Oman kuja Zanzibar unaonesha jinsi nchi hiyo ilivyokuwa na dhamira ya dhati ya
kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria kati yake na Zanzibar.
Dk.
Shein alisema kuwa Serikali ya Oman imekuwa na uhusiano na ushirikiano mwema na
Zanzibar na bado inaendelea kuiunga mkono katika kuimarisha sekta mbali mbali
za maendeleo ikiwemo sekta ya afya, elimu na nyenginezo.
Aidha,
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi za pekee kwa Sultan Qaboos kwa
misaada yake mbali mbali ikiwa ni pamoja na msaada wa kujenga msikiti wa Jaamiu Zinjibar, uliopo Mazizini mjini
Zanzibar aliouzindua hivi karibuni ambao mbali na kutumika kwa ajili ya ibada
pia, ni kituo cha kutoa mafunzo ya dini ya Kiislamu.
Dk.
Shein alisema kuwa ujio wa ujumbe huo unaoongozwa na Waziri Dk. Mohammed bin
Hamed Al Ruhmi kuja Zanzibar kwa kutumia usafiri wa meli ni kuonesha historia
ya pekee ya watu wa Oman na Zanzibar jinsi walivyokuwa wakisafiri kwa kutumia
majahazi kwa kufuata pepo za Kusi na Kaskazi wakati huo.
Nae
Waziri Waziri wa Mafuta na Gesi wa Serikali ya Oman Dk. Mohammed bin Hamed Al
Ruhmi ameeleza kuwa ujio wao una lengo la kufikisha salamu za mashirikiano,
uhusiano na upendo kwa ndugu zao wa Zanzibar kutoka kwa Sultan Qaboos wa Oman.
Waziri
Mohammed ambaye amefuatana na Kiongozi wa Taasisi ya Uwekezaji Dk. Salem bin
Nasser Al Ismaily pamoja na Bi Maitha Al Mahrooqiya, Mshauri wa Waziri wa
Utalii na Balozi Mdogo wa Oman anayefanya kazi zake hapa Zanzibar Dk. Ahmed
Hamoud Al Habsy alieleza kuwa uwamuzi huo wa kuja Zanzibar ni uwamuzi wa
kihistoria na kidugu kati ya pande mbili hizo.
Aliongeza
kuwa watu wa Zanzibar wameonesha furaha kubwa kwa ndugu zao hao wa Oman
waliofika kwa ajili ya kuwatembelea na kusifu pamoja na kupongeza mapokezi
makubwa waliyoyapata wakati walipowasili hapa Zanzibar ikiwa ni nchi ya mwanzo
kutembelewa na meli hiyo yenye kuchukuwa watu zaidi ya 300.
Pamoja
na hayo, Waziri huyo alimueleza Dk. Shein haja ya kuendeleza na kuimarisha
uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na Oman huku
akiahidi kuwa Oman itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta
mbali mbali za maendeleo.
Aidha,
kiongozi huyo alimueleza Dk. Shein azma ya Serikali ya Oman chini ya uongozi wa
Sultan Qaboos ya kujenga hospitali hapa Zanzibar sambamba na kulifanyia
ukarabati jengo la Bait Al Ajab liliopo Forodhani mjini Unguja ambalo lina
historia kubwa ya Zanzibar
Wakati huo huo, Dk. Shein alifanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtandaji wa Shirika la Umoja
wa Mataifa la Mapango wa UKIMWI (UNAIDS)
na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Michel Sidibe, Ikulu mjini
Zanzibar ambapo Mkurugenzi huyo alipongeza juhudi za Zanzibar katika kupambana
na UKIMWI.
Katika
maelezo yake Mkurugenzi huyo wa (UNAIDS), aliiopongeza Zanzibar katika juhudi
zake za kupambana na UKIMWI na kueleza kuwa ni za kupigiwa mfano katika Bara la
Afrika na duniani kwa jumla.
Aidha,
alisisitiza kuwa mafanikio na juhudi hizo zimeweza kupatikana zaidi kutokana na
uongozi, sifa, uzoefu na utaalamu alionao Dk. Shein katika suala zima la
kupambana na UKIMWI, kwani juhudi hizo amezianza muda mrefu na kumfanya
atambulike Kimataifa.
Pia,
kiongozi huyo alieleza haja kwa nchi zinazoendelea zikiwemo nchi za Bara la
Afrika kuweka mpango maalum wa kuhakikisha inaziimarisha sekta za Afya kwa
kujiandaa na matukio yanayotokea hivi sasa ya kimisaada duniani.
Nae
Dk. Shein kwa upande wake alieleza
juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kupambana na
UKIMWI na kulipongeza Shirika hilo pamoja na mashirika mengine ya Umoja wa
Mataifa kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika mapambano dhidi ya UKIMWI.
Dk.
Shein alieleza kuwa mbali ya mafanikio yaliopatikana katika kupambana na UKIWMI
pia, juhudi za makusudi zimechukuliwa na Serikali anayoiongoza na kuweza
kufanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kupunguza vifo vya akina mama na watoto.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment