Habari za Punde

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Magufuli ni Kama Mwalimu Nyerere.

Na.Emmanuel J. Shilatu
Naungana na Mamilioni ya Watanzania katika kumbukizi ya maadhimisho ya kifo cha Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kilichotokea Oktoba 14, 1999.

Mwalimu Nyerere aliyezaliwa April 13, 1922 kijijini Butiama aliamua kuiacha kazi yake ya Ualimu na kuingia kwenye mapambano makali ya kusaka Uhuru wa Tanganyika ambapo jitihada zake za dhati zilizaa matunda Disemba 9, 1961 kwa kupata Uhuru toka kwa Mwingereza.
Mwalimu Nyerere aliamini katika nguvu ya umoja na mshikamano baina ya nchi na nchi. Kutokana na ujasiri, ushupavu na nia ya dhati Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume walibadilishana Hati za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Aprili, 1964 na hivyo kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliohusisha Muungano wa nchi za Tanganyika na Zanzibar.

Mwalimu Nyerere alijenga nchi kwa misingi ya ujamaa na kujitegemea, alijenga mashirika ya umma, umoja na mshikamano wa kitaifa huku akipinga vikali masuala ya ukabila, udini, ubaguzi na rushwa. Hakika alijenga misingi imara ya amani na mshikamano.

Hakuishia kusaka Uhuru wa Tanganyika tu bali aliendeleza harakati za kusaka Uhuru na ukombozi wa nchi za kusini mwa jangwa la sahara na Afrika nzima.

Licha ya kazi Kubwa aliyoifanya na Watu wengi kuendelea kuhitaji utumishi wa Mwalimu Nyerere lakini aliamua kung'atuka rasmi Urais mwaka 1985.

Hakika Watanzania, Afrika na Dunia nzima ilipigwa ganzi Kubwa ilipopata habari ya kifo cha Mwalimu Nyerere na daima dumu ataendelea kukumbukwa. Hakika Dunia haitokaa imsahau kamwe Mwalimu Nyerere.

Leo hii tunaadhimisha kumbukizi miaka 18 bila Mwalimu Nyerere tukiwa na faraja Kubwa ya kumpata kiongozi mwenye matendo, mawazo, hulka, misimamo inayofanana nae.

Naam! Namzungumzia Rais wa awamu ya tano ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli ambaye Serikali yake inaongozwa kwa misingi ile ile kama aliyokuwa nayo Mwalimu Nyerere.

Rais Magufuli anafufua mashirika ya umma (mfano Reli, ndege na Simu); Anajenga uchumi wa viwanda; Analinda Rasilimali za Taifa (Mfano Madini); Anatoa elimu bure kuanzia shule ya msingi mpaka kidato cha nne; Anapiga vita rushwa na ufisadi; Serikali yake hataki iburuzwe na Mataifa tajiri; Anaijenga CCM isiyokumbatia matajiri; Anaendeleza mapambano dhidi ya Wahujumu uchumi; Kuhakikisha Serikali inahamia Dodoma; Kupigania haki, usawa, amani na mshikamano baina ya Watanzania. Hakika haya yote yalikuwa ni mawazo, fikra na matendo ya Mwalimu Nyerere.

Tukiwa tunaadhimisha kumbukizi ya miaka 18 bila ya Mwalimu Nyerere, ni jukumu letu Watanzania kumuenzi Baba wa Taifa kwa vitendo kwa kuzingatia Yale mema na kukemea Yale maovu ambayo yalikuwa chukizo kwake. Tuendelee kuunga mkono Serikali ya Rais Magufuli ambayo imeonyesha matendo yasiyo na shaka ya kufuata nyayo za Mwalimu Nyerere.

Hakika Dunia inakumbuka Wema, Busara, Upendo, amani, hekima na ucheshi wako Mwalimu Julius Nyerere.

Pumzika kwa Amani Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.
Mungu Ibariki Tanzania.

IMETOLEWA NA;
Emmanuel J. Shilatu
14/10/2017
0767488622 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.