Habari za Punde

Sekta Binafsi Yashauriwa Kupeleka Changamoto Zao Serikalini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi, Godfrey Simbeye akifafanua jambo kwa wafanyabiashara waliohudhuria katika Mkutano kati yao na Serikali uliolenga kujadili mafanikio na changamoto za pande hizo mbili, uliofanyika Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti mweza wa mkutano kati ya Serikali na Sekta Binafsi, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage akielezea kuhusu umuhimu wa majadiliano katika kutatua changamoto za kibiashara nchini, mkutano uliofanyika Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akizungumza na wafanyabiashara Jijini Dar es Salaam kuhusu umuhimu wa kupeleka taarifa za changamoto zao Serikalini ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (kulia) akifuatilia majadiliano kati ya Sekta Binafsi na ya Umma yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam lengo likiwa kutatua changamoto mbalimbali.
Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Mwigulu Nchemba (kulia) na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Walemavu, Mhe. Anthony Mavunde (Mb) wakibadilishana mawazo wakati wa Mkutano kati ya Sekta ya Umma na Binafsi.
Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Bw. Salum Shamte akishukuru juhudi za Serikali katika kuzileta pamoja Sekta binafsi na ya umma, wakati wa Mkutano kati ya Sekta hizo mbili Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) akipeana mkono na Mfanyabiashara Mohammed Dewji wakati wa Mkutano kati ya Sekta Binafsi na Umma Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) akipeana mkono na Mfanyabiashara Mohammed Dewji wakati wa Mkutano kati ya Sekta Binafsi na Umma Jijini Dar es Salaam
Baadi ya Wafanyabiashara Jijini Dar es Salaam wakifuatilia Mkutano kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma uliolenga kutatua changamoto za Sekta hizo ili kuharakisha ukuaji wa uchumi.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatibu Kazungu (wa pili kushoto) na  Kamishna Msaidizi wa Sera kutoka Wizara hiyo Bw. Shogholo  Msangi na wafanyabiashara wakifuatilia maelezo kutoka kwa Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hayupo pichani) kuhusu umuhimu wa majadiliano katika kujenga uchumi wenye tija kwa Sekta Binafsi na ya Umma.
Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Medard Kalemani (Mb) akizungumza kuhusu namna Serikali ilivyojipanga katika kutatua tatizo la Nishati ya umeme ili kuweza kuchochea uchumi wa Viwanda wakati wa Mkutano kati ya Sekta Binafsi na Umma uliofanyika Jijini Dar es Salaam.


(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)

Na Benny Mwaipaja
Sekta Binafsi imetakiwa kuwasiliana moja kwa moja na Serikali ili kutatua changamoto zinazoikabili badala ya kupitia wadau wa nje kwanza, kwa kuwa mlango wa Serikali uko wazi kwa ajili ya majadiliano na kutatua matatizo ya Sekta hiyo.
Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) katika Mkutano na Sekta Binafsi nchini (TPSF), Jijini Dar es Salaam.
Waziri Mpango amesema kuwa ni vema Sekta Binafsi ikashirikiana na Sekta ya Umma kwa kuwa zote zinategemeana na hakuna nchi iliyoendelea bila kuwa na Sekta Binafsi ambayo ni imara.
“Sekta Binafsi na Sekta ya Umma hazina budi kufanya kazi kwa kushirikiana kwa karibu, tena kwa kuaminiana kwa faida ya Sekta zote mbili na kwa maendeleo ya Taifa kwa ujumla” aliongeza Dkt. Mpango.
Amesema kuwa, lengo la pande zote mbili ni kuharakisha utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuongeza fursa za ajira, kipato cha mwananchi na kuondokana na umasikini uliokithiri kwa kujenga Tanzania inayoongozwa na uchumi wa Viwanda.
Dkt. Mpango alifafanua kuwa Serikali imeendelea kuyafanyia kazi mapendekezo mengi yaliyotolewa na Sekta Binafsi ikiwemo katika kuboresha mazingira ya biashara nchini ikiwemo kuondoa baadhi ya kodi zilizokuwa kero kwa wafanyabiashara.
Baadhi ya hatua zilizochukuliwa ni pamoja na Serikali kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ili kumpa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Fedha mamlaka ya kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani bila kuhusisha utaratibu wa kulipa kwanza Kodi ya Ongezeko la Thamani na baadaye kuomba kurejeshewa (Refund) kwenye miradi inayofadhiliwa na wadau wa maendeleo (Grants) au mikopo yenye masharti nafuu (Concessional Loans) ambayo mikataba husika ina masharti ya kutoa msamaha wa kodi hiyo.
“Hatua hii itawezesha wakandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini kutopata tena usumbufu katika kutekeleza miradi hiyo na miradi kutekelezwa kwa muda uliopangwa” alisema Dkt. Mpango
Ili kuvutia uwekezaji katika sekta za viwanda, kilimo cha mazao na mifugo nchini, Serikali imesamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye bidhaa za mtaji (capital goods) za viwanda vya mafuta ya kula, nguo, ngozi, madawa ya binadamu na mifugo ili kupunguza gharama za ununuzi/uagizaji wa mashine na mitambo watakayonunua wawekezaji kwa ajili ya kusindika na kutengeneza bidhaa mbalimbali.
“Serikali sasa inatoza Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kiwango cha asilimia sifuri katika huduma zinazotolewa kwenye usafirishaji wa bidhaa/mizigo nje ya nchi (ancillary transport services), hatua itayopunguza gharama za usafirishaji katika bandari zetu na kuifanya Tanzania kuwa njia bora zaidi ya kupitisha bidhaa zinazotoka nje ya nchi kwenda nchi nyingine hususan zisizo na bandari.
Kwa upande wa hali ya Uchumi, Waziri Mpango amesema kuwa robo ya kwanza ya mwaka 2017, uchumi ulikua kwa asilimia 5.7, robo ya pili ulikua kwa asilimia 7.8, hivyo kufanya nusu ya kwanza uchumi kukua kwa asilimia 6.8.
Baadhi ya shughuli za kiuchumi zilizokuwa kwa kasi ni usafirishaji na uhifadhi wa mizigo ambao umekua kwa asilimia 19.8, uchimbaji madini na mawe asilimia 18.0, uzalishaji viwandani asilimia 9.3 na ujenzi asilimia 8.8.
Dkt. Mpango alisema Sekta ya Benki kwa ujumla imeendelea kuwa imara ikiwa na mitaji na ukwasi wa kutosha juu ya viwango vinavyokubalika kisheria. Kwa kipindi cha mwaka  2009 hadi 2017 huduma jumuishi za fedha zimeongezeka kutoka  asilimia 15.8 hadi asilimia 65.3. Upatikanaji wa huduma za kifedha umeongezeka kutoka asilimia 29 kwa mwaka 2009 hadi asilimia 86 kwa mwaka 2017.
Aidha kwa upande wa mikopo kwa Sekta Binafsi ilipungua kutokana na Benki kuchukua tahadhari kutokana na kuongezeka kwa mikopo chechefu (Non-performing loans) ambapo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilichukua hatua kwa kupunguza kiwango cha amana ambacho benki za biashara zinatakiwa kuhifadhi Benki Kuu kama dhamana kutoka asilimia 10 hadi asilimia 8 na riba za mikopo ya benki hizo kushuka kutoka asilimia 16 hadi 12.
Naye mwenyekiti mwenza wa Mkutano huo Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles Mwijage (Mb) amesema kuwa njia bora ya kutatua matatizo ya Sekta Binafsi ni kuendelea kufanyika kwa majadiliano yenye tija.
Mmoja wa wajumbe wa Mkutano huo wa wafanyabiashara ambaye ni wakili wa kujitegemea Bi. Eve Hawa Sinare amesema kuwa ni vema kuangalia mfumo mzuri wa kuweka riba unaofanywa na Benki za biashara ili kuwa na uwiano mzuri.
Vilevile Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Bw. Salum Shamte ameishukuru Serikali kwa kuonesha nia ya dhati ya kushirikiana na Sekta hiyo kwa lengo la kufanikisha ukuaji wa uchiumi wa Viwanda.
Waziri mpango amewahakikishia wafanyabiashara kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha kuna majadiliano ya mara kwa mara na wadau hao ili kutatua changamoto zao na pia ameahidi kuandaa Mkutano mwingine ambao utajikita katika masuala ya kodi kabla ya Sekta Binafsi kuwasilisha mapendekezo ya kodi.
Mkutano huo wa Sekta Binafsi na Umma ni wa pili kufanyika, kwa mara ya kwanza Mkutano kama huo ulifanyika tarehe 11 Aprili, 2017 mjini Dodoma ambapo  ulisaidia kutatua changamoto nyingi ikiwemo kusaidia kuongezeka kwa ufanisi katika huduma za bandari nchini.
Imetolewa na:
                                                   Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.