STATE
HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF
THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 21.10.2017
SERIKALI
ya Mapinduzi ya Zanzibar imewaeleza wananchi wake kuwa ujio wa meli ya Sultan
Qaboos hapa Zanzibar haihusiani na masuala yoyote ya kisiasa bali meli hiyo
ilibeba ujumbe wa amani, kukuza ushirikiano na uhusiano uliopo kati ya Zanzibar
na Oman.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa
Ussi Haji Gavu, aliyasema hayo leo huko katika ukumbi wa zamani wa Baraza la
Wawakilishi, Kikwajuni mjini Zanzibar wakati alipofanya mahojiano na waaandishi
wa Habari wa vyombo mbali mbali vya Zanzibar na Tanzania Bara.
Katika maelezo yake, Waziri Gavu alieleza kuwa katika kipindi chote cha
siku nne cha kuwepo meli hiyo hapa Zanzibar ujumbe huo ulipata nafasi ya
kukutana na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo masuala mengi
yaliyozungumzwa yakiwemo uhusiano uliopo pamoja na mashirikiano katika
kuimarisha sekta za utalii, viwanda, elimu,uwekezaji, pamoja na mafuta na gesi.
Waziri Gavu alieleza kuwa katika ziara hiyo miongoni mwa mambo
waliyokubaliana kati ya Serikali ya Oman na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
ni pamoja na matengenezo makubwa ya jengo la Beit-el-Ajab, ukarabati mkubwa wa
jengo la ‘People’s palace’, uwekezaji katika kiwanda cha kusindika samaki,
uwekezaji katika kiwanda cha kutengenezea ‘juice’.
Jengine ni kuitangaza Zanzibar kiutalii na kuanzisha safari za moja kwa
moja za watalii kati ya Zanzibar na Oman kwa wageni wa Oman wanaopendelea
vivutio vya Zanzibar, kutoa msaada wa kiufundi na kisheria katika sekta ya
mafuta na gesi kila inapohitajika kufanya hivyo pamoja na kutoa mafunzo ya muda
mfupi na muda mrefu katika masuala ya mafuta na gesi asilia.
Aidha, Waziri Gavu alieleza kuwa wageni hao baada ya kufanya ziara yao
hiyo katika visiwa vya Unguja na Pemba walikiri kuwepo maendeleo makubwa
yaliofikiwa hapa Zanzibar kwani kati ya miongoni mwa wageni hao yupo alieza
liwa katika Hospitali ya Mkoani Pemba na alishangwaza ilivyo hospitali hiyo
hivi sasa na jinsi alivyoiacha yeye wakati huo.
Pamoja na hayo, ujumbe huo ulisifu amani, utulivu na mshikamano uliopo
kati ya wananchi wa Zanzibar pamoja na kufurahishwa na mapokezi makubwa
waliyoyapata kutoka kwa wananchi pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
hasa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed
Shein.
Pia, Waziri gavu alieleza kuwa hakuna Rais duniani anayefanya kazi kwa
utashi wa mtu au kikundi cha watu ama kushurutishwa na kueleza kuwa uteuzi
anaoufanya Rais Dk. Shein unatokana na azma ya kutaka mabadiliko katika
kuiletea nchi maendeleo na anafanya kwa kuafuata sheria, taratibu pamoja na
Katiba ya Zanzibar.
Waziri Gavu alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa wananchi kwa ushirikiano,
heshima na mapenzi makubwa waliyoyaonesha wakati wa hafla maalum ya kukabidhiwa
na kufunguliwa ‘Masjid Jaamiu Zinjibar’ uliojengwa kwa mashirikiano na Serikali
ya Oman chini ya uongozi wa Sultan Qaboos bin Said Al Said.
Sambamba na hayo, Waziri Gavu aliongeza kuwa kutokana na nchi mbali mbali
duniani kuendelea kuiunga mkono Zanzibar, Ubalozi wa Saud Arabia unatarajia
kufungua Ubalozi wake Mdogo hapa Zanzibar wiki ijayo.
Nae Mshauri wa Rais katika Ushirikiano wa Kimataifa, Fedha na Uchumi Balozi
Mohammed Ramia Abdiwawa akijibu baadhi ya masuali yaliyoulizwa na waandishi
waliohudhiria katika maojiano hayo, alisema kuwa uvumi wa kisiasa hauzuiliki
hapa Zanzibar kwani kabla ya ujio wa meli, wakati meli ipo Zanzibar na baada ya
kuondoka mambo mengi yamesemwa na kuzungumzwa na hasa kwa wale wasioipendelea
mema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Balozi Ramia aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakubaliwa
na inaendelea kuungwa mkono na nchi mbali mbali duniani ikiwa ni pamoja na
mashirika ya Kimataifa huku Rais wa Zanzibar akiendelea kupata mialiko kutoka
sehemu mbali mbali duniani ambapo tayari baadhi yake ameshazitembelea na
nyengine anatarajia kuzitembelea kuanzia mwaka ujao.
Hivyo, Balozi Ramia alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
inafanya vizuri katika Nyanja za Kidiplomasia huku akisisitiza kuwa Zanzibar
ina mahusiano mazuri na nchi za nje hivi sasa.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment